The House of Favourite Newspapers

Diamond…Kama Kawa Ana Copy Na Ku-Paste

0

 

Msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz.

SOKO la nyimbo katika dunia ya sasa linakuzwa na video za muziki, ubora wa video umekuwa ukichangia kuufanya wimbo kuwa mkubwa hata kama ni wa kawaida.

Kuna vitu vingi vinavyochangia video kuwa bora, baadhi ni ubora wa picha, ubora wa mandhari na ubora wa ubunifu wa kile kinachoonekana katika video husika.

Msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz anajulikana kwa kuwekeza nguvu kubwa kwenye kutengeneza video zenye kiwango cha juu, hilo halina ubishi.

Pamoja na sifa hizo, imekuwa ni kawaida kuona Diamond akiiga matukio kadhaa ya video za wasanii wa Marekani na kuziingiza kwenye video za nyimbo zake.

Mfanano wa video au jambo lolote ni kitu cha kawaida lakini kuna mazingira ambayo yanaweza kumfanya mpaka shabiki au mtazamaji wa video akaelewa kuwa hakuna mfanano wa bahati mbaya bali ni makusudi.

Gazeti hili limewahi kuandika mara mbili tofauti juu ya Diamond ambavyo amekuwa akiiga video za wasanii wa nje na kutumia kwenye video za nyimbo zake, tukukumbushe.

Aliiga Got Money wa Lil Wayne

Februari, 2016 ilikuwa ni katika video ambayo Diamond aliyoshirikiana na AKA wa Afrika Kusini kwenye Wimbo wa Make Me Sing, waliiga matukio mengi ya video ya Wimbo wa Got Money wa Lil Wayne.

Matukio ya uvamizi ndani ya benki, kuimbia benki, kupora, Diamond anavyopanda juu ya meza ya ‘cashier’, wanavyoingia ndani ya gari baada ya kupora ni sehemu ya mfanano wa wazi. Yapo matukio mengi tu zaidi ya hayo yanayofanana kwa kila kitu.

Ikumbukwe video ya Lil Wayne ilitoka mwaka 2008 wakati hiyo ya Diamond ilitoka mwaka 2016.

Video ya Kidogo nayo aliiga Julai, 2016, kwa mara nyingine Diamond ndani ya wimbo wake wa Kidogo aliowashirikisha P Square aliiga video tatu tofauti za Marekani.

Baadhi ya alivyoiga ni mavazi na maudhui kutoka kwenye video tatu tofauti za wasanii wakubwa wa Marekani.

Baadhi ya alivyoiga ni kukaa na simba pembeni ya kiti cha kifalme kama ilivyo katika kava ya ‘series’ ya Empire.

Pia Paul Okoye wa P Square anaonekana katika meza ya chakula akiwa na mavazi meupe, kama ilivyo katika video ya For The Road ya Tyga. Kuna sehe-mu waki-wa na mbwa mwitu mwe-upe, kui-mba juu ya spika kama ilivyo kwenye video ya That’s Me Right There ya Jasmine V.

Yapo mengi yaliyoigwa katika video hiyo, lakini kwa mara nyingine kupitia video ya wimbo wake wa Fire aliomshirikisha Tiwa Savage, kuna mfanano mkubwa na video ya Swalla ya msanii Jason Derulo aliyowashirikisha Nicki Minaj na Ty Dolla $ign.

Alivyo kopi na kupesti video ya Fire

Video ya Fire wa Diamond ambayo imetoka wiki iliyopita, Tiwa anaonekana akiwa kwenye kichumba kidogo kilichochorwa rangi ya mistari, pia kuna wakati Tiwa amekaa kwenye kiti kama cha kifalme, vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa Nick Minaj katika video yao iliyotoka miezi mitatu iliyopita.

Katika Fire ambayo hadi jana ilikuwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 1, mamodo wamepaka rangi za mdomoni nyingi zenye madoamadoa kama ilivyo pia kwenye video ya Swalla iliyotazamwa zaidi ya mara milioni 414. Miwani kubwa ya Minaj inaendana na ile waliyovaa mamodo wa Diamond.

WAANDISHI: JOHN JOSEPH & OMAR MDOSE

Leave A Reply