The House of Favourite Newspapers

Dimpoz Umepiga Penyewe, Nini Kinakufanya Uwe Unalala?

Omari Nyembo ‘Ommy Dimpoz’

KWAKO mkali wa Bongo Fleva, Omari Nyembo ‘Ommy Dimpoz’. Habari za kwako? Mambo yanakwendaje?

Kitambo kidogo hatujaonana mwanangu, kwa muda mrefu nimekuwa nikikuona unapiga selfie za kwenye miji mikubwa mikubwa nje ya nchi, bila shaka mambo yako hayakuwa mabaya sana! Ukitaka kujua hali yangu, mimi ni mzima wa afya, naendelea kufanya yangu ndani ya mjengo wa Magazeti Pendwa, Global Publishers.

Hakuchi kunakucha, tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunakabiliana na changamoto za hali ya sasa, si unajua tena mzee mambo si mambo! Madhumuni ya mimi kukuandikia barua hii ni kwanza kutaka kukupongeza juu ya ujio wa wimbo wako mpya wa Yanje, baba umeua!

Ni wimbo mzuri ambao kila mwanadamu mwenye kupenda muziki mzuri, hakika ataupenda na kama hana kinyongo, atakupongeza. Si tu kwamba ni ngoma kali, video yake pia ni nzuri mno halafu hata mwanadada Seyi Shay uliyemshirikisha, amefanya vizuri sana.

Pamoja na pongezi hizo, jingine ninalotaka kukueleza ni kuhusu ukimya wako wa muda mrefu. Kwa muda mrefu ulikuwa ‘umelala’, unatunyima mashabiki wako vitu adimu kama hivi. Simaanishi kwamba kila wakati utoe wimbo mpya lakini unapaswa kufanya muziki kama kazi. Muziki ndio umekutambulisha, muziki ndio umekufanya watu wakujue hivyo ni kazi inayokupasa uipe kipaumbele cha hali ya juu.

Unapokuwa kimya kwa muda mrefu, halafu unakuja unatoa ngoma kama hivi na kisha kupotea tena, watu wanashindwa kukuelewa. Wanajiuliza unafanya muziki kama kazi ya ziada au unafanya muziki kama kazi yako ya kukuingizia kipato.

Nikusihi ndugu yangu, ujio kama huu uliokuja nao tunaamini ni uwezo mkubwa ulionao kimuziki. Sitegemei tena uwe kimya. Hatutarajii tena tuone ukimya katika vyombo vya habari. Nafahamu kwa sasa upo kwenye uongozi mzuri wa Rockstar4000 sasa basi tunataka iwe ‘bampa to bampa’.

Kwa kawaida binadamu wengi huwa ni wepesi sana wa kulewa sifa, sitarajii wewe ulewe sifa maana umekaa kwenye gemu kwa muda wa kutosha sasa. Unafahamu fitna za huu muziki, unajua nini cha kufanya ili kuhakikisha jina lako linaendelea kuwa juu na muziki wako unaendelea kusikilizwa, haukauki kwenye masikio ya watu.

Sio unakaa wee hadi watu wanauliza hivi fulani yupo? Mbona amelala sana hatumsikii kabisa? Maswali kama hayo ukiwa kama mwanamuziki, si mazuri. Watu watafurahia wakikuona unatoa nyimbo kali, unafanya shoo nyingi, wanasikia habari zako za kikazi na si kwenda nje kujiachia tu kwenye viwanja vya mpira nje ya nchi.

Wimbo wako mpya ni mkubwa, tunataka nyingine kubwa zaidi ya huo ili tuendelee kukusapoti katika kazi yako. Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa na utaifanyia kazi barua yangu. Mungu azidi kukubariki na asante kwa kuisoma barua yangu. Mimi ni ndugu yako;

Erick Evarist

Comments are closed.