The House of Favourite Newspapers

Djuma Shabani Aukubali Muziki wa Nabi Yanga

0

BEKI mpya wa Yanga Djuma Shabani ameangalia mbinu za kocha wake wa Yanga, Nasreddine Nabi kisha akasema kuwa huyu jamaa ni kocha na ataifanya Yanga kufika mbali katika mashindano ambayo inashiriki msimu huu.

 

Djuma Shabani anayecheza katika nafasi ya beki wa kulia jana alikosekana katika mchezo wa Yanga dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria wa ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kukosa kibali cha kuitumikia klabu hiyo katika michuano hiyo.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Djuma alisema kuwa tangu amefika katika klabu hiyo amekuwa ni mwenye kufurahia mbinu za kocha Nabi anazowapatia kwenye uwanja wa mazoezi huku akiamini kuwa zitawasaidia kuifanya Yanga kuwa klabu tishio katika kila michuano ambayo watashiriki msimu ujao.

 

“Kocha Nabi ana uwezo mzuri sana haswa kwenye mbinu, tangu nimefika ndani ya Yanga tayari kupitia katika viwanja vya mazoezi nimeutambua uwezo wake kuwa ni wa hali ya juu,nimekutana na vitu vipya vingi ambavyo vitaniongezea kitu ndani ya uwanja.

 

“Faida kubwa inakuwa katika timu ndio maana kama yeye anahitaji kupata muda mrefu wa kukaa na wachezaji ili kufundishana mbinu mbalimbali, tayari tunaelewa nini anahitaji na hilo yeye kama kocha anatamani kuona sisi tukielewa nini anahitaji ili tukatekeleze, naamini kupitia mbinu zake itaifanya Yanga kuwa tishio,” alisema beki huyo.

ISAYA DANIEL, Dar es Salaam

Leave A Reply