DAR ES SALAAM: Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson Mwansasu, Jumamosi Februari 23, 2019 alitembelea ofisi za Kampuni ya Global Group na kueleza namna alivyoguswa na utendaji kazi wake unaozingatia weledi wa utoaji wa habari.
Global Group yenye makao yake makuu Sinza-Mori jijini Dar ni wachapishaji wa magazeti yanayosomwa zaidi nchini Tanzania ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani, Championi na Spoti Xtra. Pia ni wamiliki wa runinga na redio za mtandaoni za Global TV Online na +255 Global Radio.
Akizungumza na wafanyakazi wa Global Group, Dk Tulia aliipongeza kampuni hiyo kwa kazi kubwa ya kuwahabarisha wananchi ndani na nje ya nchi huku akiahidi kwamba akikutana na Rais Dk John Pombe Magufuli (JPM) atamweleza mambo makubwa aliyokutana nayo ndani ya kampuni hiyo.
Mbali na pongezi, Dk Tulia alisema atamweleza kuwa Global Group wanafanya kazi kubwa ya kuhabarisha watu, lakini kubwa zaidi ni kuzingatia weledi.
Kwenye eneo hilo la weledi, Dk Tulia aliwataka waandishi wa Global kutokubali kutumika kupeleka jambo la upotoshaji kwa wananchi kwani kwenye siasa kuna mambo ambayo huzungumzwa kisiasa tu bila kujali ukweli wake.
Pia alisema Global Group ni kampuni iliyojipanga kwa uhakika kuwahudumia wananchi kutokana na vifaa vya kisasa alivyovishuhudia.
“Unapokuwa nje ya Global huwezi kujua yaliyomo ndani, lakini nimeshuhudia mambo makubwa mno.
“Kwa kweli hongereni kwa kazi kubwa mnayoifanya. Nimeona vifaa vya kisasa, nimekubali mmejipanga vilivyo. Lakini kikubwa zaidi ni namna mnavyotumia weledi wenu kwenye habari, muendelee hivyohivyo kuzingatia weledi,” alisema Dk Tulia.
Kiongozi huyo alisema alishuhudia namna ambavyo kampuni hiyo ilivyotoa ajira nyingi kwa vijana.
“Nikikutana na Rais Dk John Pombe Magufuli hayo ndiyo mambo ambayo nitamweleza kuhusu Global Group. Lakini kubwa zaidi ni namna ambavyo Global Group imetoa ajira kwa vijana wengi.
“Siyo kwa Magufuli tu, lakini pia nikikutana na mtu yeyote nitawaeleza hayo ambayo nimeyashuhudia na niwapongeze tena kwa kazi kubwa mnayoifanya,” alisema Dk Tulia.
Mbali na kuzungumzia aliyoyashuhudia Global, Dk Tulia alizungumzia namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojikita katika kufanya kazi kwa kutaka matokeo.
Alisema Serikali chini ya Rais Magufuli ni Serikali sikivu ambayo inafanya kazi nzuri mno kwa wananchi wake.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano haitaki mazoea na ni Serikali ya tofauti inayotaka kuona matokeo na mambo yakifanyika.
“Rais Magufuli hataki mambo ya makaratasi, hataki mambo ya vikao na kuwa kwenye mchakato, anataka kuona vitu vinafanyika ndiyo maana unamuona kwenye hafla mbalimbali za kupokea ndege mpya au kuona mataruma kumi yameongezeka na kuwa 11,” alisema mwanamama huyo ambaye ni mbunge wa kuteuliwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Comments are closed.