The House of Favourite Newspapers

Dkt. Biteko: Watendaji Wazembe Tanesco Kuanza Kuchukuliwa Hatua Kila Mwezi

0

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dkt. Doto Biteko ameagiza ripoti ya taarifa kila wiki ya Kituo cha Huduma kwa Wateja ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ianze kutolewa kila mwezi ili kufahamu maeneo yenye changamoto ya umeme nchini na kurahisisha watendaji wazembe kuchukuliwa hatua kwenye maeneo hayo.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati wa ziara kwenye kituo hicho cha huduma kwa wateja leo tarehe 4 Aprili, 2024 jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo mbalimbali yenye lengo la kuongeza ufanisi wa kituo hicho muhimu kwa wananchi nchini.

“Wateja wote wanaopiga simu kwa sababu mnaletewa matatizo ya wananchi ni lazima mtengeneze kila wiki tupate ripoti ni mkoa gani wanahudumiwa wateja kwa haraka na mkoa upi haupewi huduma kwa haraka ili tuchukue hatua,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Ameagiza kila mkoa nchini uliopo chini ya TANESCO ufanyiwe tathmini kujua umeme umekatika mara ngapi na kufahamu sababu zilizopelekea umeme kukatika katika maeneo hayo ili kama ni uzembe umefanyika Serikali iweze kuchukua hatua haraka.

“Mimi ninafahamu kuna wakati umeme unakatika sio kwa sababu ya matatizo makubwa bali ni kwa matatizo madogo madogo ya kiusimamizi kwenye laini zetu. Unakuta kuna mahali mti umedondoka kwenye njia zetu na unachukua muda mrefu kuondolewa, au mteja amepiga simu anachukua muda kuhudumiwa, tunahitaji hiyo ripoti,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine Dkt. Biteko ameagiza, kituo kuangalia utaratibu wa namna nzuri ya wateja kutogharamia malipo kipindi wanapopiga simu kuhudumiwa na kituo.

Leave A Reply