The House of Favourite Newspapers

Dogo Mfaume na Simulizi ya Majonzi Madawa ya Kulevya

0

DOGO MFAUME (1)Msanii Mfaume Selemani ‘Dogo Mfaume’

MAKALA: Imelda Mtema na Hamida Haasan

KWA wanaoufuatilia Muziki wa Mchiriku, Kazi ya Dukani ni moja kati ya ngoma kali zilizowahi kutikisa, ni utunzi mahiri wa msanii aitwaye Mfaume Selemani ‘Dogo Mfaume’.

Mkali huyo alipotea kwenye ulimwengu wa muziki baada ya kutopea kwenye madawa ya kulevya. Kipaji chake kikapotea, sasa yupo Rehab kwa ajili ya kupata tiba ya madawa ya kulevya.

Waandishi wetu walimtembelea kwenye kituo cha kuzuia matumizi ya madawa ya kulevya (Rehab) cha Pillimissana Foundation kilichopo Kigamboni jijini Dar na kuzungumza naye. Yupo kituoni hapo takriban miezi minne, mahojiano yalikuwa hivi:

DOGO-MFAUMEEBMM: Mashabiki wako wangetaka kujua ulianzaje kujiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya?

Dogo Mfaume: Unajua sisi vijana tunapenda kujichanganya kwenye makundi mbalimbali hivyo siku moja rafiki yangu mmoja alinichanganyia kwenye bangi.

BMM: Ikawaje sasa alivyokuchanganyia?

Dogo Mfaume: Siku hiyo niliona ni ya tofauti sana na ladha ya kipekee hivyo kila siku nikawa namtuma akaninunulie bangi japokuwa alikuwa akiniambia kuwa hiyo bei yake ni tofauti na mwisho kabisa nilijua nini kinafanyika nikaendeleza.

BMM: Ni mwaka gani ulianza rasmi kutumia madawa ya kulevya?

dogo_mfaumeDogo Mfaume: Ilikuwa mwaka 2009 kwa hiyo hadi hivi sasa ni takriban miaka saba.

BMM: Kipindi hicho ulikuwa umeshatoa wimbo wako wa Kazi ya Dukani?

Dogo Mfaume: Hiyo ndiyo ilinipa wazimu kwa sababu nilijiona nishakuwa maarufu hivyo nikaanza kufanya mambo ambayo siyo kabisa.

BMM: Vipi, baada ya kuanza kutumia madawa uliweza tena kukaa na kutunga nyimbo na kuwa na uwezo wa kufikiria kama zamani?

DOGO MFAUMEDogo Mfaume: Hapana, nilipoteza dira kabisa na hata hela sikuwa nayo kazi yangu ilibaki ni kumdangaya mama kuwa natakiwa kuchoma sindano ili nianze tiba ya kuzuia uvutaji wa madawa na yeye alikuwa hajui alikuwa anatafuta na wakati mwingine anakopa ananipa akifanya hivyo tu naenda kuyanunua nabwia.

BMM: Vipi kuhusu shoo ulikuwa unapata kama kawaida?

Dogo Mfaume: Zilianza kupotea taratibu mpaka nikawa sipewi kabisa na hakuna anayenikumbuka hapo ndipo maisha yalipoanza kuwa magumu zaidi.

DOGO MFAUME (2)BMM: Wazazi wako walikuwa wakiongeleaje suala hilo?

Dogo Mfaume: Yaani kama mama yangu alikuwa anaumia sana na mpaka akatoa kiwanja pale kwetu lijengwe kanisa lakini kila walipokuwa wakiniita nisali angalau nitakuwa

 sawa niliona wananizingua tu.

BMM: Sasa umeanza kubadilika, shavu linakuja, mama anajisikiaje?

Dogo Mfaume: Naumia maana mama yangu amefariki dunia kabla hajaona kitu ambacho alikuwa akikililia kila siku, niache madawa lakini ndiyo hivyo tena, ameondoka kabla ya kuona mabadiliko yangu. Alitangulia mbele ya haki Januari, mwaka huu.

BMM: Ni nani alikushauri kuja kituo hiki cha Pillimissana?

Dogo Mfaume: Dada Pili ambaye ni mmoja wa wamiliki wa kituo hiki alikuwa anafahamiana na watu wangu wa karibu hivyo aliwaelezea nia ya kutaka kunisaidia.

BMM: Walitumia mbinu gani kukushawishi maana inajulikana waliotopea kwenye madawa ni ngumu sana kuwaleta huku?

Dogo Mfaume: Mimi kwanza walinidanganya naenda kurekodi nyimbo na watanilipia bure hivyo nilipofika wakaniambia

 hapa ndiyo umefika huwezi kutoka kwenda popote.

BMM: Hukuweza kutumia ubabe au akili hata ya kuruka ukuta?

Dogo Mfaume: Hapa wako makini maana kuna ulinzi wa kutosha na kila unachowaza wenzako wameshakijua hivyo inabidi unakuwa mpole.

BMM: Kuna tofauti gani ulipokuja na sasa kwa kipindi ulichokaa humu?

Dogo Mfaume: Kwa kweli kama unavyoniona niko vizuri sana siyo yule aliyekuwa ameshateketea kabisa, nimerudi kabisa namshukuru Mungu.

BMM: Unawahusia nini mastaa wenzako kuhusiana na madawa?

Dogo Mfaume: Jamani siyo mazuri yanatuaibisha na kutudhalilisha, yanaondoa thamani yetu kwa jamii maana hata kama unataka kumtembelea mtu wako wa karibu anajua umekwenda kumpiga mizinga.

 BMM: Una mchumba?

Dogo Mfaume: Kwa sasa sina, nilikuwa naye zamani akaondoka kutokana na tabia yangu, nimemsababishia kauza mpaka vitu vyake ili tu awe ananipa hela maana niliishiwa.

Risasi: Utajilinda vipi ukishatoka ili usizame tena?

Dodo Mfaume: Hapa kuna mafunzo mazuri sana ya kukuelimisha vitu gani vya kuepukana navyo ili usije ukarudi tena kwenye matumizi ya madawa kwa hiyo niko vizuri.

BMM: Nini ambacho hutakaa ukisahau kilikuumiza sana kipindi cha utumiaji wa madawa?

Dogo Mfaume: Kuna siku kulikuwa na shoo wakanipa dili la kuimba nilipopanda jukwaani tu nikasikia mtu mmoja anasema ‘mshushe teja huyooo’, aisee niliumia sana, tena sana.

BMM: Ulibahatika kuwa na mtoto?

Dogo Mfaume: Hapana maana wanawake wenyewe walikuwa ni waongo sana anabeba mimba anakuambia ya kwako kumbe siyo.

Dogo Mfaume aliyefanya vizuri katika muziki hadi kupewa tuzo ya Muziki Bora wa Asili mwaka 2009, alitamba na ngoma kali ikiwemo Hereni ambapo watu wengi walimsifu kwa kujua kutunga nyimbo ambazo zinawakilisha maisha ya kawaida ya watu wa hali ya chini.

VIDEO: DOGO MFAUME AZUNGUMZA ALIVYOACHA MADAWA YA KULEVYA AKIWA PILLI MISSANA FOUNDATION

Leave A Reply