The House of Favourite Newspapers

Donald Trump Atamani Kufanya Mdahalo wa TV na Rais Joe Biden

0

Donald Trump amempa changamoto Rais Joe Biden kufanya naye mdahalo utakaokuwa unarushwa moja kwa moja na televisheni, katika kipindi hiki ambacho wababe hao wawili wa siasa za Marekani wanaelekea kwenye ‘mechi ya marudiano’ ya kuwania kuingia Ikulu ya White House kufuatia matokeo yao ya kura zilizopigwa Jumanne, maarufu Super Tuesday.

Mgombea urais huyo mtarajiwa kupitia chama Republican amesema anatamani muda wowote kufanya mdahalo wa TV na Rais Biden anayegombea tena urais kupitia chama cha Demokrati “wakati wowote na mahala popote.”

Hata hivyo, hakuna mdahalo wowote uliopangwa kufanyika hadi sasa kabla ya uchaguzi wa Novemba mwaka huu.

Hatua ya Trump kutaka mdahalo na Biden imekuja saa chache baada ya mpinzani wake aliyekuwa amebaki kupambana naye katika chama cha Republican, Nikki Haley, kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho cha kuwa mgombea urais kupitia chama cha Republican.

“Ni muhimu, kwa manufaa ya nchi yetu, mimi na Joe Biden tujadili masuala ambayo ni muhimu sana kwa Marekani na watu wa Marekani,” ameandika Trump kwenye tovuti yake, maneno yote akiandika kwa herufi kubwa.

Amependekeza kwamba mdahalo huo unaweza kuendeshwa na Kamati ya Kitaifa ya Kidemokrasia au Tume ya Mijadala ya Rais, ambayo imesimamia mijadala ya urais kwa miaka 30 sasa.

Leave A Reply