The House of Favourite Newspapers

Dube Nje Wiki Sita, Mwenyewe Afunguka

0

HUKU ikiwa na mwendelezo wa matokeo mabaya kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara, Azam imepata pigo jingine baada ya taarifa rasmi za kitabibu kutoka Afrika Kusini kuthibitishwa kwamba kinara wao wa mabao Mzimbabwe, Prince Dube atakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita baada ya kuvunjika mkono wake wa kushoto.

 

Dube alipata jeraha hilo Novemba 25, mwaka huu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Yanga baada ya kuanguka vibaya akiwa kwenye harakati za kuwania mpira dhidi ya beki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto.

 

Mshambuliaji huyo mwenye mabao sita aliondoka nchini alfajiri ya Novemba 29, kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu kwenye hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo Cape Town, chini ya daktari bingwa wa mifupa,
Robert Nicolas.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Azam, Zakaria
Thabith ‘Zaka za Kazi’ alisema: “Tumepokea taarifa rasmi kutoka kwa madaktari wanaomhudumia Dube nchini Afrika Kusini ambao wameweka wazi kuwa mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita.

 

Baada ya kipindi hiko cha wiki sita kukamilika ndipo ataruhusiwa tena kuanza mazoezi mepesi ili kurejea uwanjani,” alisema Thabith. Kwa upande wake Dube aliwatakia kila la kheri Azam na kuahidi kurejea akiwa bora zaidi: “Nawashukuru wale wote ambao wamekuwa wakinitumia salamu za pole hasa familia yangu ya Azam.

Na pia nawatakia kila la kheri katika michezo ijayo, naamini nitarejea nikiwa bora zaidi,” alisema Dube.

Stori na Joel Thomas

 

Leave A Reply