The House of Favourite Newspapers

Dunia Ulioiacha Nyuma Yako – 58

2

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.

Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.

Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Baadaye Magesa anagundua kwamba Grace ni jasusi wa kimataifa, akiwa amebadilisha jina na mwonekano wake, jambo linalompa hofu kubwa ndani ya moyo wake. Hata hivyo, msichana huyo anamuelewesha hali halisi.

Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.

Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.

Kadiri upelelezi unavyozidi kupamba moto ndivyo mambo mengi yanavyozidi kuibuka na sasa watu wengine wanahojiwa kuutafuta ukweli wa tukio zima. Sekretari wa Magesa na yule wa waziri mkuu nao wanahojiwa ambapo mambo ya ajabu yanazidi kubainika na sasa ipo wazi kwamba kuna mkono wa waziri mkuu. Jitihada za kumfikisha kwenye mikono ya sheria zinazidi kupamba moto.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Tuanzie wapi? Ipo wazi kwamba mheshimiwa anahusika lakini bila kukusanya ushahidi wa kutosha kumtia hatiani, atatushinda,” alisema Kasekwa mara baada ya kumaliza kuzungumza na mwanamke yule kupitia ‘Video Conference!’

“Safari hii hawezi kutushinda, tukiendelea na umakini huu hawezi kutoka kwenye kumi na nane zetu,” alisema Mandiba kwa kujiamini, akaongeza:

“Kwanza inabidi tuchague vijana maalum wa kuwa wanamfuatilia nyendo zake, tunapaswa kuongeza umakini maradufu, ‘tuna-deal’ na mtu hatari sana. Kama aliweza kuagiza Magesa auawe, hashindwi kuagiza mwingine yeyote kati yetu auawe ili kuficha uozo wake,” alisema Ngai.
Majadiliano yakaendelea kwa muda mrefu na mwisho, walikubaliana kwamba wapeane muda wa kupumzika wa saa chache kisha wakutane tena hapohapo kuendelea na kazi. Kwa jinsi hali ilivyokuwa, hakukuwa na muda wa kupoteza.

Ilikuwa ni lazima kila kitu kifanyike haraka na hatimaye wamalize kazi kwani kwa jinsi ambavyo wangezidi kuchelewesha kumtia hatiani mheshimiwa waziri mkuu, ndivyo ambavyo wangeendelea kuyaweka hatarini maisha ya watu wengine, wakiwemo wao wenyewe.
* * *
“Haloo mheshimiwa!”
“Eeh! Nani wewe.”
“Ni mimi Edwin Mulisa kutoka Control Room hapa sentro.”
“Ooh! Mbona umetumia namba tofauti kijana?”
“Kuna tatizo, naomba tukutane haraka iwezekanavyo. Niambie upo wapi?”

“Mbona unanitisha? Nipo huku Kigamboni, kuna mtu nilikuwa namsubiri kutoka hapohapo, vipi kwema?”

“Siyo kwema mkuu, nakuja. Laptop yako si unayo kwenye gari?”
“Ndiyo! Njoo mpaka jirani na Dege Beach, ukifika nipigie simu.”

Baada ya maelezo hayo, Edwin Mulisa, askari ambaye pia alikuwa mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano, ambaye ndiye aliyemuunganisha Grace kwenye ‘video conference’ muda mfupi uliopita, alizungumza na simu na muda mfupi baadaye, alionekana akichomoa kifaa kidogo kilichochomekwa kwenye ‘server’ iliyokuwa ikihifadhi taarifa zote za kiusalama.

Akageuka huku na kule na alipohakikisha kwamba hakuna anayemuona, alisogea mpaka kwenye mtambo wa kuongozea kamera za usalama (CCTV) zilizokuwa zimefungwa kwenye jengo zima la makao makuu ya polisi, isipokuwa ndani ya chumba cha mitambo (Control Room) pekee.

Akabonyezabonyeza mtambo huo na muda mfupi baadaye, picha za matukio yaliyokuwa yakiendelea ndani ya jengo hilo na nje, zilianza kujifunga moja baada ya nyingine.

“The CCTV System is Restarting, Please Wait!” (Mfumo wa CCTV unajiwasha upya, tafadhali subiri) yalisomeka maneno kwenye skrini kubwa ukutani, harakaharaka Mulisa akatoka huku akiwa na uhakika kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kumuona, hata wakifuatilia kamera hizo kwa sababu alizima mtambo wote na kuuwasha, zoezi ambalo lingechukua sekunde 90 ambazo zilitosha kabisa kumfanya awe ameshafika nje.

Muda mfupi baadaye, muungurumo wa pikipiki ulisikika kutoka kwenye maegesho ya nje, Mulisa akawa amefanikiwa kuondoka kijanja bila mtu yeyote kumuona. Muda mfupi baadaye, mitambo ya CCTV ilikuwa imeshawaka na kazi ya kurekodi matukio yote ikaendelea bila mtu yeyote kushtukia kilichotokea.
* * *
Mandiba alikuwa akirejea nyumbani kwake, baada ya kufanya kazi kwa saa nyingi mfululizo bila kupumzika. Njia nzima, alikuwa akiwaza kuhusu kazi ngumu iliyokuwa mbele yake na wenzake, akawa anajaribu kutafakari ni jambo gani lililomkumba waziri mkuu mpaka awe na roho ya kikatili kiasi hicho.
Akiwa anaendelea kuwaza, huku akiendesha gari lake, Toyota Prado V8, alishtuka alipotazama kupitia kioo cha juu ya siti ya dereva (driving mirror), baada ya kuona kuna watu wawili waliopakizana kwenye bodaboda, wakiwa wamevaa makoti marefu meusi, walikuwa wakija kwa kasi kubwa nyuma yake.

Awali alipunguza mwendo akiamini watapita na bodaboda yao lakini akashangaa kuona nao wakipunguza mwendo, kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa chake. Akakanyaga mafuta na kulifanya gari lake lianze kwenda kwa kasi kubwa lakini alishangaa tena kuona nao wanaongeza kasi.

“Haloo! Kuna watu nahisi wananifuatilia na bodaboda, wanaweza kuwa siyo watu wazuri, mwambie mlinzi afungue geti kabisa na wewe na watoto ingieni kwenye chumba cha chini haraka iwezekanavyo,” alisema Mandiba wakati akizungumza na mkewe ambaye alimuelewa na kutekeleza alichoambiwa.

Gari lilizidi kuchanja mbuga, akawa anabadili barabara kwa makusudi lakini kila alipokuwa akikata kona, nao walikuwa wakikata na kumfuata. Akazidi kuongeza kasi, gari likawa linakwenda kwa kasi kubwa na muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amekaribia nyumbani kwake.

Kama alivyokuwa ameagiza, kwa mbali aliona geti likiwa limefunguliwa lakini katika kile ambacho hakutaka kukiamini, alishtuka kuona watu wengine wawili, waliokuwa kwenye bodaboda na kuvalia makoti meusi kama wale waliokuwa wakimfukuza kwa nyuma, wakiwa wamepaki bodaboda yao katikati ya barabara, mita kadhaa kutoka nyumbani kwake, huku mmoja akiwa ameshuka na kumnyooshea bunduki huku akimuamuru kusimama.

“Mungu wangu!” alisema Mandiba na muda mfupi baadaye, kishindo kikubwa kilisikika eneo hilo.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne kwenye Gazeti la Uwazi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

2 Comments
  1. bahati wilson khombe says

    Huyo waziri balaa tunangoja mtujuze

  2. Paul Fussi says

    Hadithi ni nzuri sana sasa huyo askari anayewauza wenzake anawaza nini?

Leave A Reply