The House of Favourite Newspapers

Dunia uliyoiacha nyuma yako – 60

0

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa, anaponea chupuchupu kufa katika ajali ya kutengenezwa.

Anaokolewa na jasusi wa kimataifa, Grace ambaye anatumia utaalamu wa hali ya juu na kuwafanya watu wote waamini kwamba amekufa. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.

Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.
Kadiri upelelezi unavyozidi kupamba moto ndivyo mambo mengi yanavyozidi kuibuka na sasa watu wengine wanahojiwa kuutafuta ukweli wa tukio zima. Sekretari wa Magesa na yule wa waziri mkuu nao wanahojiwa ambapo mambo ya ajabu yanazidi kubainika na sasa ipo wazi kwamba kuna mkono wa waziri mkuu.

Jitihada za kumfikisha kwenye mikono ya sheria zinazidi kupamba moto lakini ghafla Mandiba anajikuta akiwa matatizoni baada ya kugundua kuna watu wanamfuatilia. Ananusurika kuuawa baada ya kutumia mbinu za hali ya juu za kijeshi.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Upande wa pili, tukio la kuvamiwa kwa Mandiba lilileta mshtuko mkubwa hasa kwa wenzake waliokuwa wakifanya naye kazi, wakahisi huenda kuna uwezekano  mkubwa kuna mtu alikuwa akivujisha taarifa za uchunguzi wao kumhusu waziri mkuu, ikabidi kazi ya ziada ianze kufanywa kubaini ni nani aliyekuwa akivujisha taarifa.
“Nahisi kuna mtu kutoka ndani anayetuhujumu.”
“Ni kweli kabisa, na baada ya Mandiba, na sisi tujiandae, lolote linaweza kutupata.”
“Hatupaswi kuogopa chochote, lazima tupambane kwa udi na uvumba kuhakikisha tunamfikisha kwenye mikono ya sheria,” alisema Kasekwa, wazo lililoungwa mkono na mwenzake.

Walichokubaliana, ni yule mtuhumiwa wa tukio la kutaka kumuua Mandiba ambaye alinusurika kwenye tukio hilo na kujeruhiwa vibaya, aendelee kufuatiliwa kwa karibu na akipata nafuu kidogo, wambane ili aseme ni nani alikuwa amemtuma na kwa sababu gani walikuwa wanataka kumuua Mandiba.

Kitendo cha kunusurika kuuawa, kilizidi kumpa hasira Mandiba, akawa mkali kama mbogo aliyejeruhiwa. Kwa sababu za usalama, aliamua kuihamisha familia yake kwenda mafichoni huku na yeye akiamua kubadilisha makazi yake.
Alijiapiza kwamba ni lazima amjue aliyekuwa nyuma ya tukio la kutaka kuuawa nje ya nyumba yake. Kuna wakati alikuwa anahisi hata wenzake anaofanya nao kazi kwa karibu, wanaweza kuwa wanahusika kutaka kumhujumu ingawa hakutaka kuyapa mawazo hayo nafasi kwenye kichwa chake.

“Grace anaweza kuwa anajua chochote cha kunisaidia?” Mandiba alijiuliza lakini kabla hajaamua kumtafuta mwanamke huyo na kumueleza kilichotokea, aliamua kwanza kwenda hospitalini kumtazama yule jambazi mmoja aliyenusurika.
Haikuwa rahisi kuingia mpaka kwenye wodi aliyokuwa amelazwa kutokana na ulinzi uliokuwa umewekwa lakini kwa kuwa alikuwa akifahamika, aliruhusiwa na kuingia moja kwa moja mpaka kwenye wodi hiyo.

Akawa anamtazama kwa makini akijaribu kukumbuka kama alishawahi kumuona sehemu. Japokuwa alikuwa ameunganishwa na mashine ya kumsaidia kupumua, Mandiba hakujali, akaanza kumhoji kuhusu mtu aliyewatuma kutaka kumuua.
Kutokana na hali aliyokuwa nayo, hakuweza kujibu chochote zaidi ya kuwa anapepesa macho tu.

“Lazima uniambie ukweli, vinginevyo nakuua, nitachomoa mashine ya kukusaidia kupumua ufe, niambie,” alisema Mandiba kwa sauti iliyojaa jazba, mtu huyo akawa anatingisha kichwa akimsihi Mandiba asimuue.
“Upo tayari kunieleza ukweli?” alihoji Mandiba, akawa anatingisha kichwa kuonesha kukubali lakini mpaka apate kwanza nafuu ndiyo atamwambia ukweli. Nitarudi baadaye,” alisema Mandiba, akatoka wodini humo na kwenda mpaka makao makuu kwa lengo la kuzungumza na Grace.
“Nimefikiria kwa kina naona tumshirikishe Grace kwenye hili, labda anaweza kuwa na msaada kwetu.”
“Wazo zuri, apigiwe simu sasa hivi,” alisema Kasekwa akionesha kuunga mkono kilichosemwa na Grace.
*   *   *
Muda mfupi baada ya kumaliza kuzungumza na yule jambazi aliyenusurika katika jaribio la kumuua, Mandiba alitoka wodini humo lakini akiwa hajafika kwenye mlango mkubwa wa wodi hiyo, mahali palipokuwa na askari kadhaa wenye silaha, alipishana na muuguzi aliyevaa kitambaa cheupe usoni kama wavaavyo madaktari wanapokuwa kwenye chumba cha upasuaji.

Mkononi alikuwa amebeba sinia dogo, likiwa na mabomba mawili ya sindano na kichupa chenye dawa. Mandiba hakujali chochote akiamini ni muuguzi wa siku zote anayesimamia matibabu ya mgonjwa yule.

Dakika kadhaa baadaye, akiwa na wenzake makao makuu, wakijiandaa kumpigia simu Grace, simu yake ilianza kuita mfululizo, awali hakutaka kupokea simu hiyo lakini alipoona inaendelea kuita kwa muda mrefu ilibidi aipokee.
“Mkuu, huyu mgonjwa wako imekuwaje tena?”
“Imekuwaje kwani vipi?”
“Kabla hujaingia kumuona hali yake ilikuwa inaendelea vizuri lakini tangu ulipoondoka, hali imebadilika ghafla na hivi tunavyoongea, madaktari bingwa wamemzunguka na hakuna dalili kama anaweza kupona,mapovu yanamtoka kila sehemu.”
“Mungu wangu, nakuja sasa hivi,” alisema Mandiba huku akiwa tayari ameshaelewa kilichokuwa kimetokea. Ilibidi awaambie na wenzake, kila mmoja akapigwa na butwaa. Wakatoka harakaharaka mpaka kwenye maegesho ya magari na kuingia kwenye gari la Kasekwa, safari ya kuelekea hospitalini ikaanza kwa kasi kubwa.

Walipofika hospitalini, walipitiliza moja kwa moja wodini ambako walipokelewa na milio ya mashine kadhaa alizokuwa ameunganishwa mtu huyo, zikitoa milio iliyoashiria kwamba alikuwa kwenye dakika za mwisho za uhai wake, povu jingi lililochanganyikana na damu likimtoka mdomoni na puani.
Mandiba alisogea mpaka kwenye dripu aliyokuwa ametundikiwa, akawa anaitazama kwa makini kama anayechunguza kitu, kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa chake.

“Hebu mchomoeni hii dripu haraka,” alisema Mandiba, madaktari wakatazamana kwani ilikuwa kinyume na utaratibu kuelekezwa nini cha kufanya na mtu ambaye hakuwa daktari. Hata hivyo, kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo mgonjwa, ilibidi mganga mkuu awape ishara wenzake, wakatii walichoambiwa.

“Naomba mkachunguze kwa makini kilichopo ndani ya dripu hii,” alisema Mandiba kwa kauli iliyojaa mamlaka.
“Hapa si kuna kamera za usalama za CCTV?”
“Ndiyo mkuu.”
“Nipeleke kwenye chumba cha kuongozea kamera haraka,” alisema Mandiba, akawapa wenzake maelekezo kwamba ulinzi uimarishwe eneo lote la hospitali na kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayeondoka.

Utekelezaji ukafanyika mara moja, muda mfupi baadaye, magari kadhaa ya polisi yaliwasili eneo hilo, wagonjwa na watu wengine wakawa wanashangaa kumetokea nini kwani haikuwa kawaida ya hali hospitalini hapo kuwa hivyo.
Mandiba alienda moja kwa moja kwenye chumba cha kuongozea kamera za usalama, akisaidiana na mganga mkuu pamoja na mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano hospitalini hapo, walianza kufuatilia kamera zote na kurudisha nyuma picha za matukio yaliyotokea kwa kipindi cha nusu saa iliyopita.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye Gazeti la Uwazi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply