The House of Favourite Newspapers

ELEWA CHANZO CHA FIGO KUSHINDWA KUFANYA KAZI (KIDNEY FAILURE)

FIGO ni miongoni mwa viungo muhimu sana katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu. Wiki iliyopita nilieleza jinsi kiungo hiki kinavyopata mawe na jinsi ya kujikinga na tatizo hili. Nashukuru wengi wamepiga siku kushukuru kwa elimu ile. Kwa kawaida, mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana kama yale ya maharage, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu za chini.

Kazi kuu za figo ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu katika damu na hivyo kusaidia katika kuhifadhi na kuthibiti kiwango cha maji na madini (electrolytes) mwilini. Katika kutekeleza hayo, figo huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika.

Kazi nyingine za figo ni kurekebisha na kuthibiti kiasi cha vitu mbalimbali katika damu pamoja na kiasi cha maji katika mwili, husaidia kutengeneza kiasili cha erythropoietin ambacho ni muhimu sana katika utengenezaji wa chembe nyekundu za damu, husaidia uzalishaji wa vitamini D na husaidia pia katika kuthibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure). Kwa kawaida damu inayozunguka mwilini hatimaye huingia kwenye figo kwa ajili ya kuchujwa, kutoa uchafu pamoja na sumu nyingine zisizohitajika mwilini. Kitendo hiki cha utengenezaji mkojo hufanyika katika hatua kuu zifuatazo;

Hatua ya kwanza ni uchujaji. Damu kutoka nje huingia ndani ya mafigo na kupita kwenye glomeruli, lenye umbo kama chekeche/chujio ambalo limeundwa na mishipa mingi midogo ya damu iliyojizungusha pamoja. Vitu mbali mbali, maji pamoja na sumu zilizo katika damu inayopita kwenye vimishipa hivi na kisha kuingia katika mirija mingine mikubwa kwa ajili ya uchujaji zaidi.

Mirija inayofuata huendelea kuchuja damu na kunyonya baadhi ya vitu vilivyo chujwa kimakosa kuvirudisha mwilini, mpaka kiasi sahihi cha uchafu kinachotakiwa kuchujwa kinapokuwa kimefikiwa. Mara baada ya mkojo kutengenezwa na kutolewa kwenye figo, husafiri kuingia kwenye kibofu cha mkojo kwa kupita kwenye mirija ijulikanayo kama ureta. Kutoka kwenye kibofu, mkojo hutolewa nje ya mwili kupitia kwenye mrija wa urethra.

Kushindwa kufanya kazi kwa figo hutokea iwapo sehemu ya figo au figo lote litapoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kutoka katika damu na kutengeneza mkojo. Kitendo hiki husababisha kusanyiko la uchafu pamoja na sumu kadhaa katika damu ambazo ni hatari kwa afya ya mhusika.

Figo kushindwa kufanya kazi kumeganyika katika makundi yafuatayo, Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF), Figo kushindwa kufanya kazi kwa kiasi (Mild renal/kidney insufficiency) na tatizo sugu la figo kushindwa kufanya kazi (Chronic renal failure).

Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF) Hii ni hali inayotokea kwa ghafla, na kudumu kwa saa chache mpaka siku chini ya 14, na kusababisha ongezeko la kiwango cha creatinine na urea katika damu. Hali hii huwapata karibu asilimia 5 ya wagonjwa waliolazwa hospitali kwa sababu ya matatizo mbalimbali. Aidha hali hii hutokea zaidi kwa wagonjwa mahututi na wale wanaohitaji uangalizi wa kipekee, yaani waliolazwa ICU.

SABABU ZAKE

Visababishi (au aina) vya ARF vinaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu: Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal causes/failure), matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure), matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/ failure)

Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal causes/failure) Aina hii hutokea kwa takribani asilimia 60 mpaka 70 ya ARF zote. Katika kundi hili, figo hukosa damu ya kutosha kwa ajili ya kuchuja na hatimaye hushindwa kufanya kazi yake  ipasavyo. Mambo yanayoweza kusababisha pre-renal failure ni pamoja na:

Upungufu wa maji mwili unaosababishwa na kutapika kupita kiasi, kuharisha, au kupoteza damu kupita kiasi (kwa sababu ya ajali au kuumia), kuvurugika kwa mtiririko wa damu inayoingia kwenye figo kwa sababu ya: Kushuka kwa ghafla kwa shinikizo la damu kwa sababu ya kupoteza damu nyingi wakati wa upasuaji mkubwa, kuumia au kuungua sehemu kubwa ya mwili, au maambukizi katika mfumo wa damu (sepsis) yanayoweza kufanya mishipa ya damu kutanuka na kushusha shinikizo la damu, kuziba au kusinyaa kwa mishipa inayopeleka damu kwenye figo.

Figo inaweza kufeli pia kutokana na moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) au shambulio la moyo (heart attack) linalosababisha kushuka kwa shinikizo la damu na ini kushindwa kufanya kazi (liver failure) kunakoweza kusababisha mabadiliko katika mfumo wa homoni zinazoathiri shinikizo la damu pamoja na mtiririko wa damu kwenda kwenye figo.

Mwanzoni kabisa mwa pre-renal failure huwa hakuna athari yoyote inayotokea kwenye figo, na mara nyingi, figo laweza kurudi katika hali yake ya kawaida iwapo chanzo cha tatizo kitagunduliwa na kushughulikiwa ipasavyo.

Mambo yanayosababisha madhara katika figo husababaisha karibu asilimia 25 mpaka 40 ya vyanzo vyote vya ARF. Visababishi vilivyo katika kundi hili hujumuisha vile vinavyoathiri uchujaji, mtiririko wa damu ndani ya figo na seli za figo zinazoshughulika na uchujaji na ufyonzaji wa chumvi na maji.

Visababishi hivyo ni pamoja na: Magonjwa katika mishipa ya damu, kuwepo kwa damu iliyoganda ndani ya mishipa ya damu inayopita katika figo, ajali/ Kuharibika kwa tishu na seli za figo, magonjwa ya mzio katika glomeruli na figo kwa ujumla (glomerulonephritis). Magonjwa yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na maambukizi (infection) ya bakteria jamii ya streptococci.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.