The House of Favourite Newspapers

Eric Shigongo: Namshukuru Mungu Kwa Muujiza Wa Mama Yangu Na Kujiandikisha Chuo Kikuu

0

 MWISHO wote wa wiki iliyopita, yaani Oktoba  21 na 22,  2017, ulikuwa ngumu kwangu, mama yangu alikuwa mgonjwa, moyoni nilikuwa nikimshukuru Mungu sikusafiri kwenda Singida kwenye semina, vinginevyo moyoni ingekuwa ni kujilaumu  na majuto tupu. Hali ya mama yangu mpendwa haikuwa nzuri hata kidogo, mwili wake haukuwa na nguvu na mapigo ya moyo yalikuwa yakienda kwa kasi huku akipatwa na maruweruwe! Dk James Mabula ni mtoto wa dada yangu, anafanya kazi Hospitali ya TMJ, huyu ndiye huwa ni daktari wa mama yangu anapokuwa nyumbani, uamuzi alioufikia ni kuchukua damu ya bibi yake siku ya Jumapili kwenda kuipima ili kujua kiwango cha madini ya Sodium katika damu, kwani hili ndilo huwa ni tatizo la mama mara kwa mara.

 

Majibu yalipotoka yalionesha kiwango cha madini hayo kilikuwa kimeshuka mpaka 104 mlq/L, chini kabisa, kuliko hata ilivyotokea katika Hospitali ya Aga-Khan alipolazwa wiki tatu zilizopita, mara moja tukaamua kuwasiliana na Dk Kaduri, mmoja wa madaktari bingwa wa magonjwa ya mwili (Physician) ambaye amejipatia umaarufu mkubwa sana jijini Dar es salaam, huyu pia humtibu mama yangu. Uamuzi alioufikia daktari ilikuwa ni mama awekewe mara moja dripu za Sodium 3% ili kurejesha madini hayo kwenye kiwango cha kawaida ndani ya damu, kumbuka ilikuwa ni siku ya Jumapili, upatikanaji wa dawa hiyo adimu ulikuwa mgumu, hata hivyo, kwa neema ya Mungu zilipatikana chupa nne, akaanza kuwekewa taratibu chini ya usimamizi wa Dk James Mabula.

Eric Shigongo akiwa na mke wake Veneranda, anapenda anapenda asome sana  wakiwa pamoja baada ya kujiandikisha chuo kikuu tayari kuanza mwaka wa kwanza.

Jumatatu ya Oktoba 23, 2017, asubuhi kama kawaida niliwapeleka watoto wangu shule, ndani ya gari tukafanya mambo yaleyale ambayo hufanya kila siku; kufundishana mambo mbalimbali ya maisha, kutoka shuleni nilipita nyumbani kwa mama yangu, nikakuta hali ilikuwa bado hairidhishi. Nilipowasiliana na Dk Kaduri, alifikia uamuzi wa kumlaza mama wodini ili amfuatilie kwa karibu, tukamchukua  ndani ya gari huku akilalamika maumivu mwili mzima hadi Hospitali ya TMJ ambako alipewa kitanda katika chumba namba 207 na matibabu yakaanza chini ya usimamizi wa madaktari wawili; Dk Kaduri na Dk Kapteni ambaye ni mzoefu zaidi katika hospitali hiyo.

 

Wiki nzima ilikuwa ya matibabu katika hospitali hiyo, hali ya mama ikiwa bado haiimariki, hakuna kitu kigumu duniani kama kumshuhudia mtu unayempenda akiteseka kitandani, mara kadhaa nilikuwa nikilazimika kutoka chumbani kwenda nje ambako nilijifuta machozi nikimwomba Mungu atende muujiza. Sista Theodora Faustine Oisso ambaye ni Mkuu wa shule

ya Sekondari ya St. Joseph na Mchungaji Elisha wa Kanisa la AICT-Chang’ombe walikuwa ni miongoni mwa watu waliofika chumbani kwa mama yangu tukasali pamoja tukimwomba Mungu atende muujiza. Mungu akajibu maombi, hali ya mama ambaye alikuwa hawezi kuzungumza ikabadilika, akawa na uwezo wa kutambua watu na kuongea! Dawa pamoja na sala zetu kwa Mungu zilikuwa zimejibiwa, moyoni mwangu nilijawa na furaha mno, nikamshukuru Mungu kwa wema wake na upendeleo ambao kwa mara nyingine tena alikuwa amenipa. Ninauita upendeleo kwa sababu si watu wengi sana

kwenye umri kama wangu wana mtu wa kumwita mama, hii ni bahati, ndiyo maana huwa ninafanya kila kinachowezekana kuona kwamba ninamsaidia mama

yangu! Watu wengi wakija wageni kumwona huniambia: “Eric mama amekua, lolote linaweza likatokea” kama njia ya kuniandaa kwa kinachokuja mbele. Huwa sikubaliani kabisa na maneno haya, siwezi kukata tamaa hata kama mama yangu amezeeka kiasi gani, lazima nipiganie uhai wake mpaka dakika ya mwisho, anayeufahamu mwisho wa uhai wa mwanadamu ni Mungu peke yake, vijana wengi sana katika kipindi cha miaka zaidi ya kumi ambayo mama yangu amekuwa mgonjwa wamefariki dunia na kumwacha, hakuna anayejua mwisho wa maisha ya mwanadamu.

Mwaka 1996, mjomba wangu alikuwa mgonjwa sana, daktari aliyekuwa akimtibu mjini Mwanza alituita na kutuambia: “Mzee anaumwa mno, hawezi kupona, mrejesheni nyumbani mkasubirie huko” alisema maneno hayo akiwa hajui ya kwamba yeye ndiye angekufa kabla ya mjomba wangu kwani daktari huyo kijana  alisafiri kwenda Bukoba siku chache baadaye tukiwa tumeshamwondoa mjomba hospitali, akirejea Mwanza alikufa ndani ya meli ya MV Bukoba.

 

Hii siyo hadithi ni maisha ya kweli, jambo hilo lilinifundisha kwamba hutakiwi kumkatia tamaa mtu anapokuwa mgonjwa na kuona wewe mzima utaishi maisha marefu kuliko yeye, mwisho wa uhai wetu ni Mungu pekee anayefahamu! Nilishazugumza huko nyuma juu ya kifo cha

baba yangu mzazi, Mzee James Bukumbi, ambaye aliugua kwa muda mrefu sana, akawa anapungukiwa Protini iitwayo Albumin katika damu, hali iliyomfanya akawa  anavimba mwili mzima. Chupa moja ya Protini ya Albumin iliuzwa shilingi laki tatu na alitumia chupa moja kila baada ya  siku moja, asipowekewa, mwili ulivimba na kumsababishia mateso makali, kumpunguzia mateso nililazimika kuwa ninanunua dawa hiyo kwa muda wa miezi isiyopungua mitatu mpaka alipofariki dunia.

 

Nakumbuka daktari mmoja aliniita baada ya kunionea huruma kwa jinsi nilivyokuwa nikitumia fedha nyingi kununua dawa za baba na kuniambia: “Eric unatumia fedha nyingi sana, lakini baba yako hatapona!” Lengo lake lilikuwa ni kuniambia niache kununua dawa ili baba aage dunia, nilishindwa kufanya hivyo, sikutaka mateso na mashtaka moyoni mwangu baadaye kwamba nilisababisha kifo cha mzazi wangu aliyenizaa, kunitunza na kunifundisha kufanya biashara. Hicho ndicho kitu ninachokifanya kwa mama yangu, mimi na ndugu zangu tunapambana kadiri tuwezavyo   kumpunguzia mateso, ni kweli ana miaka themanini na sita, lakini wapo watu wana umri mkubwa kuliko

yeye na wanaishi vizuri, hivyo hatutakiwi kukata tamaa, hilo tunalielewa na Mungu atusaidie. Kwa mnaokumbuka miezi miwili iliyopita niliwataarifu kwamba, darasa la saba miye, nilikuwa nimefanikiwa kufaulu mtihani wa kuingia Chuo Kikuu, narudia tena CHUO KIKUU! Siyo cha mtaani, Tumaini University! Kuchukua shahada, narudia tena SHAHADA ya Mawasiliano ya Umma, muujiza mwingine kutokea katika maisha yangu. Novemba 3, 2017 siku ya Ijumaa, mke wangu alinisindikiza kwenda Chuo Kikuu cha Tumaini kukamilisha usajili, maana leo (siku ya Jumatatu) nipo darasani, siku ya kwanza Chuo Kikuu ninasoma, wengi wanashangaa nimerudi tena shuleni kufuata nini? Swali la ajabu kabisa, hakuna kitu muhimu katika maisha ya mwanadamu kama elimu, kamwe asiwepo mtu wa kupuuza elimu, itabaki kitu cha kwanza katika ukombozi wa mwanadamu hasa ikitumiwa.

 

Mstari ulikuwa mrefu sana kwenye dirisha la usajili, wakati huohuo nilikuwa ninatakiwa kurejea hospitalini kuendelea kufuatilia matibabu ya mama yangu, baada ya kusimama kwa muda mrefu hatimaye alipita mama  mmoja akiwa na mafaili mkononi, alipotabasamu tu nikamchangamkia, ikatokea kwamba siku moja nilipokwenda chuoni hapo  nilidondosha picha zangu, yeye ndiye akaziokota.

 

“Nilipoziokota tu nikaziweka kwenye Biblia yangu, nikajua siku moja utarejea hapa nikupe!” Moyoni mwangu nikaamini kuweka picha zangu kwenye Biblia ndiko kulikofanya nifaulu mtihani wa kuingia Chuo Kikuu, nikamshukuru sana mama huyo mwisho nikamweleza juu ya shida niliyokuwa nayo ya kurejea hospitalini, akakubali kuchukua karatasi zangu zote ili anisaidie kufanya usajili, nikamshukuru Mungu na mimi na mke wangu tukaondoka kurejea Hospitali ya TMJ.

 

Mpaka leo siku ya Jumamosi nikiwa ninaandika kumbukumbu hizi, mama yangu yupo Hospitali ya TMJ akiendelea kupata matibabu, ninamshukuru Mungu hali yake inaendelea vizuri, siku ya Jumatatu anaweza kuruhusiwa, jina la Bwana libarikiwe na Mungu wetu apewe sifa milele na milele, amina. Nawashukuru sana watu wote walioshirikiana nasi katika maombi, kutupigia simu na kufuatilia hali ya mama yetu, Mungu awabariki sana na kuwafungulia milango ya Baraka katika maisha yenu. Kesho ni siku ya Jumapili, Mungu akituamsha salama ni siku ya ibada, nitakuwa ninazungumza na vijana wa Kanisa la Victory Christian Center katika ibada ya mchana juu ya somo liitwalo USIWE CHUKIZO KWA MUNGU BAADA YA KUBARIKIWA! Ahsanteni na Mungu awabariki sana. Itaendelea wiki ijayo…

Leave A Reply