Ester Bulaya Amvaa Sirro Bil 4 Zilizopotea kwenye Mfuko Kufa na Kuzikana – Video
Mbunge wa Viti Maalum Esther Bulaya amedai kuwa zaidi ya shilingi Bilioni 4.8 zimepotea kwenye Mfuko wa Tuzo na Kufa na Kuzikana wa Jeshi la Polisi nchini.
Bulaya amesema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Amesema kipindi ubadhirifu huo unafanyika Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini alikuwa Simon Sirro.
“Kwenye mfuko huu umetajwa ufisadi, anayeidhinisha fedha hizi alikuwa Simon Sirro [IJP], mleteni kokote alipo aje apambane na hali yake, hamuwezi mkafumbia macho hivi vitu”. amesema Bulaya
Ameongeza kuwa mfuko huo umeanzishwa kwa dhamira ya kusaidia askari wadogo wa Jeshi la Polisi ambao wakifiwa na wenza wao zisaidie familia.
“Wanaopambana kwa jasho katika kulinda nchi hii kupambana na Majambazi, wakipata madhara hizi fedha ndio ziende zikawasaidie na mfuko huu wanaochangia ni Askari wenyewe kwa kufanya kazi ya ziada kulinda kwenye migodi, kulinda kwenye mabenki, kulinda kwenye taasisi mbalimbali halafu wanatokea viongozi wao wanatumia mwanya kwa ile nidhamu ya kijeshi kwamba huwezi kuhoji wanawadhulumu Askari wa kawaida”.- amesisitiza Bulaya.