The House of Favourite Newspapers

EXCLUSIVE…Harmo Aukimbia Mjengo Wa Kifahari

0

EEH bwana namuogopa Mungu wanafuata wazazi…Nikimuacha bosi anafuata mwenye nyumba…Mwenye nyumba nitakulipa mwezi ujao…Eeh bwana nauza feni, nauza jiko…Mwenzenu nimeishiwa kodi ya mwenye nyumba…Nauza godoro nataka nikalipe kodi ya mwenye nyumba…Kodi yako inaisha lini?

Yangu keshokutwa…Yako inaisha lini?” Hii ni sehemu ya mashairi kutoka kwenye Wimbo wa Mwenye Nyumba kutoka kwa Kundi la Mabantu.

 

MAMBO SI MAMBO

Taarifa ikufikie kwamba, hivi karibuni kumeibuka jambo zito kwenye ulimwengu wa mastaa Bongo kuwa, ule mjengo wa kifahari aliokuwa akiishi staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na aliyekuwa mkewe, Sarah Michelotti, mambo yamekuwa si mambo.

 

Mjengo huo upo ushuani Mbezi-Beach (Goigi) jijini Dar na sasa kuna madai mazito kwamba, jamaa huyo amehamia kwa mpenzi wake, mwigizaji Kajala Masanja anayeishi maeneo ya Mbezi-Salasala jijini Dar.

DALALI MZIGONI

Awali, zilianza kuvuma taarifa kuwa, kuna dalali yupo mzigoni akitangaza kuipangisha nyumba hiyo baada ya Harmonize au Harmo ambaye ni Mkurugenzi wa Lebo ya Konde Gang Worldwide kudaiwa kushindwa kulipa kodi.

Kufuatia taarifa hizo zilizokuwa zikisambaa mithili ya moto wa kifuu, baadhi ya mashabiki walianza kumwaga maneno ya kila aina wakiyaelekeza kwa jamaa huyo.

 

“Konde boy mpaka atakimbia mjini, slow but sure, sasa hivi anaishi kwa mwanamke, haya maisha ya wasanii siyawezi,” aliandika Jamal for Love kwenye Instagram.

 

“Oya si nyumba ya Harmonize mmekosea nyumba. Nyumba ya Harmonize alilipia insurance (bima) kwenye Wimbo wa Never Give Up,” aliandika officiallyvanhanball kwenye Instagram.

 

TATIZO NI NINI?

Ilidaiwa kwamba, baada tu ya kuachana na mkewe, Sarah mwaka jana alishindwa kulipa kodi na ndiyo chanzo cha yeye kutimuliwa kwenye nyumba na kutafutiwa mpangaji mwingine.

 

IJUMAA KAZINI

Kama ilivyo desturi ya Gazeti la IJUMAA, baada ya kunyetishiwa taarifa hizo liliingia kazini ili kupata ukweli wa ishu hiyo.

Gazeti la IJUMAA limefunga safari hadi kwenye nyumba hiyo na kujionea mjengo huo ambao kwa sasa Harmo ameondoka.

 

JIRANI AELEZA ANACHOKIJUA

Baada ya kubisha hodi kwa muda mrefu kwenye geti la nyumba hiyo bila mafanikio, hatimaye alitoka jirani wa nyumba ya pili ambapo alieleza kile ambacho anakijua kwa sharti ya kufichwa jina gazetini;

 

IJUMAA: Habari yako…

JIRANI: Salama, karibuni…

IJUMAA: Asante, samahani tunaulizia nyumbani kwa msanii Harmonize?

JIRANI: Ni hapo kwenye hilo geti la mbele, lakini kwa sasa ameondoka…

 

IJUMAA: Ameondoka?

JIRANI: Ndiyo, ameondoka tangu tarehe 15, mwezi huu (Machi) na ameshabeba kila kitu, nasikia amehamishia studio kwake.

IJUMAA: Sasa yeye anaishi wapi kwa sasa?

 

JIRANI: Nasikia anaishi kwa huyo mpenzi wake mpya (Kajala).

IJUMAA: Tangu ameanza kuishi hapa alikuwa na muda gani?

JIRANI: Kama sijakosea ni miaka miwili.

 

IJUMAA: Hapa ndipo alikuwa anaishi na yule mwanamke wa kizungu?

JIRANI: Ndiyo, yule Sarah siyo kwamba alikuwa akiishi naye, yule ni mke wake wa ndoa kabisa ila kwa sasa wameachana ingawa bado hajampa talaka, nasikia ana huyo mwanamke mwingine muigizaji jina lake silifahamu vizuri (Kajala).

 

IJUMAA: Sasa nani anaishi humu ndani maana tumeambiwa tukija hapa tutamkuta mama yake? JIRANI: Mama yake alishaondoka baada ya Harmonize kushindwa kulipa kodi.

IJUMAA: Kwani ni nani aliyekuwa akilipa kodi hapa? JIRANI: Nasikia ni yule mwanamke (Sarah) ndiye alikuwa akilipa kodi.

MLINZI SASAIli kupata ukweli juu ya ishu hiyo, Gazeti la IJUMAA liliweka kambi nyumbani hapo hadi alipotokea mlinzi wa nyumba hiyo ambaye anafunguka kuwa ni kweli Harmonize ameondoka mahali hapo ila kuhusu ishu ya kushindwa kulipa kodi, hajui.

“Nimekuwa nikilinda hapa kwa muda mrefu, lakini kuhusu ishu ya Harmonize kuondoka kwa sababu ya kushindwa kulipa kodi, hilo mimi silifahamu kabisa ila ninachojua ni kwamba mtu ameamua kutoka kwenye nyumba kwa ajili ya kubadilisha mazingira.“Labda ngoja niwafanyie mpango wa kuzungumza na baba mwenye nyumba hii, naamini yeye atakuwa na ukweli wote,” anasema mlinzi huyo.

 

MWENYE NYUMBA AANIKA UKWELI

Katika mazingira kama hayo, Gazeti la IJUMAA lilizungumza na mwenye nyumba kwa njia ya simu ambapo hakuwa tayari kuzungumza jambo lolote kuhusu mteja wake huyo, lakini akaanika ukweli kwamba aliamua kubadilisha mazingira, lakini hana tatizo naye.

 

“Mimi nadhani Harmonize aliamua tu kubadilisha mazingira na sidhani kama kuna jambo lingine tofauti na hilo,” anasema baba mwenye nyumba huyo bila kutaja jina.Jitihada za kumpata Harmo ziligonga mwamba baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa hivyo zinaendelea.

USHAURI WA BURE

Kwa sasa hali ya Maisha ni ngumu hivyo ili kuwekeza na kuwa na akiba, lazima mtu utafute nyumba za bei rafiki, lakini nzuri.

Kwa nini mtu uendelee kulipa kodi kubwa?Kuna taarifa kwamba, nyumba hiyo ilikuwa inalipiwa Dola za Kimarekani 1,000 kwa mwezi ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 2 hivyo alichokifanya Harmo ni uamuzi mzuri.Harmo alitengana na Sarah mwaka jana na tangu hapo kumekuwa na tetesi kuwa huwenda yeye ndiye aliyekuwa akimsapoti kwa suala la pesa.

STORI: KHADIJA BAKARI NA MEMORISE RICHARD, DAR

Leave A Reply