The House of Favourite Newspapers

EXCLUSIVE: Ukweli Juu ya Kijana Aliekutwa Kwenye Kontena,Huu Hapa! (Video)

Taharuki kubwa imetokea visiwani Zanzibar katika bandari ya Malindi ambapo mtu mmoja ameokolewa kutoka ndani ya kontena, analodaiwa kukaa ndani yake kwa siku nne.

 

Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, walianza kusikia kontena moja likigongwagongwa kwa nguvu huku mtu akipiga kelele za kuomba msaada, ikabidi kazi ya kuanza kulitafuta kontena hilo ianze kwani eneo hilo kulikuwa na makontena mengi yaliyopangwa, yakisubiri kupakizwa katika meli.

 

Baada ya kazi kubwa, hatimaye vikosi vya uokoaji na askari wa jeshi la polisi pamoja na wa kikosi cha maji, walifanikiwa kulipata kontena hilo ambapo walipolifungua, mwanaume huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 mpaka 30 alitoka huku akionesha kudhoofika, akachukuliwa na jeshi la polisi mpaka kwenye gari dogo lililokuwa eneo hilo na kuondoka naye.

 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar, kijana huyo ni mvuvi na kwamba, akiwa katika kazi yake hiyo, mvua kubwa ilianza kunyesha hali iliyomfanya kuingia katika moja ya makontena yaliyopo bandarini hapo, lakini baadaye alipitiwa na usingizi.

 

Baadaye, wafanyakazi wa bandari, bila kutambua kwamba kuna mtu ndani ya kontena hilo, walilifunga na kwenda kulipanga mahali yanapohifadhiwa makontena, ambapo siku nne baadaye ndipo ilipogundulika kwamba kuna mtu ndani ya kontena hilo, akaokolewa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya kupata huduma ya kwanza.

 

Comments are closed.