Fahamu Kirusi cha Ukimwi Kinavyoishi Mwilini – 2

WIKI iliyopita tulieleza kwa kirefu juu ya kirusi cha Ukimwi kinavyoishi mwilini.  Tunaendelea kuelimisha kuwa kuongezeka kwa wingi wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika mwili, kinga ya mwili huzidi kudhoofika na hii husababisha tezi na tishu zilizoathiriwa na VVU kuharibika kutokana na maambukizi ya muda mrefu.

 

Dawa za kufubaisha VVU yaani Antiretroviral therapy (ARV’s) huanza kutumiwa wakati seli aina ya CD4 zinapopungua na kuwa kiwango cha chini sana. Kupungua kwa seli hizi za CD4 ni kielelezo cha kinga ya mwili kuwa dhaifu.

 

Matumizi ya dawa hizi huboresha kinga ya mwili na kumfanya mgonjwa kuishi kwa muda mrefu bila kuonyesha dalili au viashiria vyovyote vile.

Kama mgonjwa wa VVU hatumii dawa za kufubaisha VVU au anatumia ARV’s ambazo hazimsaidii au hazifanyi kazi vizuri mwilini mwake, basi mgonjwa ataendelea kuingia kwenye hatua ya nne ya Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) au AIDS.

 

Hatua ya Nne: Kama nilivyoeleza hapo juu, hatua hii hujulikana kama Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) au AIDS, ambapo Kupitia dalili zifuatazo unaweza kupata mwanga kama umeambukizwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi.

 

Dalili hizo ni homa za mara kwa mara, kupanda kwa joto la mwili nyuzijoto 38 hadi 39 ambapo joto hili nalo hupanda mara kwa mara. Pia unaweza kupatwa na dalili nyingine zitokanazo na homa hizi kama vile maumivu ya koo, kuvimba kwa baadhi ya tezi za shingo na mwili kukosa nguvu.

Uchovu ni moja ya madhara makubwa ya virusi vya Ukimwi mwilini kwa sababu mfumo wa kinga mwilini hudhoofishwa na virusi. Maumivu ya koo na kichwa yanayodumu, ni moja ya dalili kubwa ya kuwa na maradhi haya, hasa kama yanadumu kwa muda mrefu.

 

Afya ya ngozi kubadilika. Baada ya mfumo wa kinga za mwili kushuka ni rahisi sana kwa ngozi kupata magonjwa ya ngozi ikiwemo chunusi sugu, ngozi kubadilika rangi na kuwa na mabakamabaka. Japo si wote hupatwa na dalili hii. Kichefuchefu, kuharisha na kutapika, ni moja ya dalili za kuwa na Ukimwi.

USHAURI

Ifahamike kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu wote wanaoishi na virusi vya Ukimwi hukumbwa na hali hizo hasa wakati ambao tayari virusi hivyo vimeshatengeneza ugonjwa wenyewe wa Ukimwi kwa hiyo uonapo dalili hizo wahi kumuona daktari akufanyie vipimo.


Loading...

Toa comment