The House of Favourite Newspapers

Fahamu kwa Undani Tatizo la Ugumba (Infertility)

0

 

KUNA aina mbili za ugumba;

Ugumba wa asili (Primary infertility) – Hii ni pale ambapo mwanaume na mwanamke hawajawahi kutungisha mimba kabisa maishani mwao hata baada ya kujamiiana au kukutana kimwili kwa muda wa mwaka mmoja bila ya kutumia njia yoyote ile ya kuzuia kupata mimba.

 

Ugumba unaotokea baadaye maishani (Secondary infertility) – Hii ni pale ambapo wote wawili, mwanamke na mwanaume wameshawahi kupata ujauzito au kutungisha mimba angalau mara moja maishani mwao na baada ya hapo hawajafanikiwa kupata au kutungisha mimba tena.

 

Asilimia 30-40 ya tatizo la ugumba huwakumba wanaume na asilimia 40-50 ya tatizo hili huwakumba wanawake, wakati asilimia 10-30 zilizobaki za tatizo hili husababishwa kwa pamoja na matatizo kati ya wanaume na wanawake, hapa sababu halisi hazijulikani.

 

Kwa wale wenye afya njema, uwezekano wa kupata au kutungisha mimba iwapo watajamiiana mara kwa mara kwa mwezi, ni asilimia 25-30. Wanawake hufikia kilele cha kupata ujauzito (peak fertility) wakiwa kwenye miaka ya ishirini.

Mwanamke aliye na umri wa zaidi ya miaka 35 (au baada ya miaka 40) ana uwezekano wa kupata ujauzito kwa asilimia 10.

 

Je, mimba hutungwa vipi?

Mimba hutungwa baada ya mwanamke kutoa yai kutoka katika moja ya viwanda vyake vya mayai ya kike yaani ovaries, kitendo hiki hujulikana kama ovulation. Yai husafiri hadi kwenye mfuko wa uzazi ujulikanao kama uterus (womb) kupitia kwenye mirija ya uzazi inayojulikana kama mirija ya fallopian.

 

Mbegu moja ya kiume (sperm) ni lazima itungishe au iungane (fertilize) na yai au mayai ya kike (ovum au ova) wakati yai likielekea kwenye uterus. Baada ya mbegu ya kiume na yai la kike kuungana, muunganiko uliotengenezwa yaani kiinitete (embryo) hushuka mpaka kwenye mfuko wa uzazi na kujiwekeza hapo ili kiendelee kuwa kiumbe.

 

Tatizo la ugumba linaweza likawa ni la nwanaume au mwanamke pekee ingawa wakati mwingine wote wawili wanaweza kuwa na tatizo hili.

Sababu zinazoleta tatizo la ugumba (infertility) ni kwa wanawake;

 

Tatizo la ugumba linaweza kutokea wakati wa; Yai au kiumbe kilicho ndani ya mfuko (uterus) wa uzazi kushindwa kukua hadi kufikia kuwa mtoto, Mayai yaliyo ndani ya mfuko wa uzazi kushindwa kujishikiza kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi (uterus lining), matatizo kwenye njia ya kupita yai au mayai wakati yanakwenda kwenye mfuko wa uzazi (uterus), matatizo ya mayai ya uzazi (ovaries) kushindwa kutoa mayai (eggs).

 

Tatizo la ugumba kwa wanawake husababishwa na; matatizo ya autoimmune disorders kama antiphospholipid syndrome (APS), matatizo katika uterus na shingo ya kizazi (cervix) kama uvimbe (fibroids or myomas).

 

Matatizo katika mfumo wa kuganda wa damu (clotting disorders) husababisha ugumba, pia mazoezi kupita kiasi, afya iliyodhoofika, na matatizo ya kula, baadhi ya madawa au sumu, msongo wa mawazo, tatizo la kukosekana kwa usawa wa mfumo wa vichocheo mwilini (hormonal imbalance), uzito uliopitiliza (obesity) na unywaji pombe kupindukia.

 

Wengine hupata ugumba kwa sababu ya magonjwa ya muda mrefu kama kisukari (diabetes), magonjwa ya kina mama, magonjwa ya zinaa, Saratani, Uvutaji sigara, madawa ya kulevya kama kokeini, bangi, hashishi nk.

 

Au matatizo ya hedhi – wanawake wanaopata hedhi bila kutoa mayai (anovulatory menstrual cycle), kuwepo kwa cervical antigens ambazo huua manii za mwanamume na hivyo kusababisha kwa mwanamke kutopata ujauzito.

 

Tatizo la ugumba – linaweza kutokea kwa mwanamume kwa kupungua idadi ya manii, Kwa mwanamume, tatizo la ugumba husababishwa na; Mazingira yaliyo na kemikali zinazoathiri uwezo wa mwanaume kumbebesha mimba mwanamke, kukaa sehemu zenye joto kali sana kwa muda mrefu, matatizo kwenye mfumo wa viashiria vya asili (genetic abnormalities), unywaji pombe kupindukia, matumizi ya madawa ya kulevya kama kokeini, bangi, hashishi nk, hupunguza idadi na kiwango (quality) cha manii, kuzeeka, kutumia dawa za vichocheo vya mwilini ama kukosekana kwa baadhi ya vichocheo mwilini (hormonal deficiency) nk.

Itaendelea wiki ijayo.

Na Dk. Marise Richard

Leave A Reply