The House of Favourite Newspapers

Fahamu tatizo la mzio au allergy-3

0

Je, mzio au aleji inatibika?

Tunamalizia mada ya ugonjwa wa mzio kwa kueleza tiba yake. Njia bora zaidi ya kutibu na kupunguza uwezekano wa kupata aleji ni kutambua kitu au vitu vinavyokusababishia hali hiyo na kuviepuka.

Kama ni chakula au dawa au kemikali, epuka kabisa matumizi yake na kama ni vumbi jitahidi kukaa mbali nalo. Kadhalika shambulio kali la aleji linaweza kusababisha muhusika kulazwa hospitali kwa vile lisipodhibitiwa kifo kinaweza kutokea. Zipo aina mbalimbali za dawa zinazotumika kutibu na kuzuia aleji, kulingana na jinsi daktari atakavyoona inafaa kwa kuzingatia ukali wa tatizo, dalili zake, umri wa mgonjwa pamoja na hali yake ya kiafya kwa ujumla.

Dawa hizi ni pamoja na za jamii ya Antihistamines za jamii ya Corticosteroids ambazo ni maalum kwa kutuliza mcharuko mwilini ambazo huwa katika miundo mbalimbali kama vile krimu, matone ya kuweka machoni au masikioni, za kuvuta au kupulizia, sindano au vidonge.

Kwa wale wenye mafua na kuziba kwa pua, hushauriwa kutumia dawa zinazosaidia kufungua pua, hata hivyo dawa hizi hazina budi kutumiwa kwa uangalifu hasa kwa watu wenye magonjwa ya shinikizo la damu au moyo. Dawa nyingine ni zile zinazosaidia kuzuia vitu vinavyosababisha aleji.

Aina nyingi za aleji hutibika kwa urahisi kwa kutumia dawa. Wapo baadhi ya watu hususan watoto wanaoweza kujenga hali ya aleji dhidi ya aina fulani za vyakula, hali wanayoweza kuendelea nayo mpaka ukubwani. Kwa kawaida, kitu kikimletea mtu aleji utotoni huendelea kumuathiri daima. Madhara ya aleji ni pamoja na kupata shambulio kali ambalo linaweza kusababisha kifo kama matibabu hayatafanywa haraka.

Kuna baadhi ya watu ambao, kwa mfano, wakila baadhi ya vyakula huvimba mwili na kushindwa kupumua mpaka kuhitaji kulazwa hospitali na kusaidiwa kupumua kwa mashine. Madhara mengine ni pamoja na shida ya kuvuta pumzi au kushuka kwa shinikizo la damu (kupata shock).
Namna ya kujikinga na aleji

Kuna baadhi ya watu wanaonasibisha aleji na itikadi za kichawi suala ambalo si sawa, kwani mzio ni tatizo linalojulikana kitiba na pia huweza kutibika. Pindi mtu anapopatwa na aina fulani ya aleji, kinga bora ni kukwepa mambo yote yanayoweza kuchochea kutokea hali hiyo.
Usikose kusoma wiki ijayo ili upate elimu zaidi.

Leave A Reply