The House of Favourite Newspapers

Fahamu tatizo la mzio au allergy

0

Hives_on_backLeo tutatungumzia tatizo la mzio au aleji. Ili kufahamu tatizo hilo na kujua jinsi ya kukabiliana nalo.

Mzio au aleji (allergy) ni matokeo ya mpambano uliopitiliza kati ya kinga ya mwili na kitu chochote ambacho kwa ujumla huwa hakina madhara kwa mwili pale inapotokea kimeingia ndani ya mwili au kimegusa sehemu fulani ya mwili.

Mpambano huu ndiyo husababisha mtu kuwa na dalili za aleji au mzio. Kwa kawaida kinga ya mwili huulinda mwili dhidi ya vitu mbalimbali hatari kwa afya kama vile vimelea vya magonjwa kama bakteria na virusi, lakini wakati mwingine inaweza kupambana pia na vitu ambavyo havina madhara yoyote kwa mwili ambavyo huitwa Allergens.

 Baadhi ya vitu vinavyosababisha mzio ni pamoja na vumbi, baadhi ya dawa, baadhi ya vyakula, kung’atwa na wadudu kama vile nyuki, aina fulani ya uyoga, vumbi vumbi la maua (pollens) na kadhalika. Kuwa na mzio ni jambo la kawaida.

Haishangazi kuona kuna baadhi ya watu wanaopatwa na mafua karibu kila siku au wengine kushindwa kuvaa baadhi ya nguo, vitu kama saa au cheni za dhahabu kwa vile tu huvimba mwili au kuwashwa pindi wanapofanya hivyo. Watu wenye aleji au mzio huwa na hisia zisizo za kawaida za mwili dhidi ya baadhi ya vitu.

 Mwili unapokumbana na vitu vinavyosababisha aleji mfumo wa kinga ya mwili huzalisha kemikali mbalimbali ikiwemo histamine ambayo hupambana na Allergens hizo. Matatizo ya kijenetiki pamoja na hali tofauti tofauti za kimazingira zote zinahusika katika kusababisha mtu kuwa na mzio.

Wapo baadhi ya watu ambao hukumbana na mzio pindi wanapokuwa katika mazingira ya joto au baridi, huku wengine hupatwa na mzio pindi wanapopigwa na jua kali. Wakati mwingine, hata msuguano mdogo tu wa ngozi unaweza kuwasababishia baadhi ya watu dalili fulani za mzio.

Kwa kawaida, mzio wa aina fulani huwa haurithishwi miongoni mwa wanafamilia. Kwa mfano kama mzazi ana aleji na baridi si lazima watoto wake pia wawe na aleji hiyo ya baridi ingawa wanaweza kuwa na aina nyingine ya aleji. Uwezekano wa mtoto kupata aleji huongezeka zaidi iwapo wazazi wote wana aleji na vitu fulani na huwa zaidi iwapo mama ndiye mwenye aleji.

 

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply