The House of Favourite Newspapers

Fakhi Atua Dar Kuichinja Simba

0
Wachezaji wa timu ya Kagera Sugar wakifanya maombi.

Said Ally, Dar es Salaam, Championi Jumatatu
MAMBO yanazidi kuwa mazito katika sakata la Simba kupewa pointi tatu za bwerere, kwani timu ya watu watatu kutoka Kagera, akiwemo beki Mohammed Fakhi, inatua Dar ikiwa na ushahidi kamili kwa ajili ya kuhakikisha Simba inapokwa pointi hizo na Kagera Sugar inarudishiwa ushindi wake.
Simba ilipewa pointi tatu na mabao matatu na Kamati ya Saa 72 kwa kutumia kanuni ya 42 (11) ya Ligi Kuu Bara 2016, inayosema: “Klabu itakayomtumia mchezaji anayetumikia adhabu ya kuonyeshwa kadi tatu za njano au kadi nyekundu kwa mujibu wa kanuni ya 37: 1,2,3,4 itapoteza mchezo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu, endapo klabu haina uhakika na inataka taarifa ya idadi ya kadi zake, itaomba kwa maandishi toka TFF.”

Beki Mohammed Fakhi

Kamati ya Saa 72 ilijiridhisha kwamba Fakhi alicheza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba hivi karibuni ambao Simba walifungwa 2-1 mjini Bukoba akiwa na kadi tatu za njano alizozipata katika michezo dhidi ya Majimaji, Mbeya City na African Lyon. Kagera Sugar na Fakhi mwenyewe wanakataa mchezaji wao kuwa na kadi tatu za njano, wanadai katika mchezo dhidi ya Lyon hakupewa kadi ya njano.
Kagera Sugar ilikata rufaa kwa Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji.
Sasa kamati hiyo imewaita watu watatu kutoka Kagera Sugar ambao watatakiwa kuwasilisha nyaraka na uthibitisho wao katika kikao cha rufaa hiyo kinachotarajiwa kufanyika kesho Jumanne jijini Dar.
Fakhi alitua Dar mapema tangu Jumatano iliyopita akiwa na hasira ya kuichinja Simba akipania kueleza uthibitisho wote kwamba hana kadi tatu za njano lakini viongozi wengine wawili wa Kagera Sugar, walisafiri jana hadi Dar wakiwa na ‘rundo’ la mafaili kwa ajili ya kuieleza ukweli Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji kwamba mchezaji wao hana kadi tatu za njano, hivyo warudishiwe pointi zao tatu na Simba itoke kapa. Waliosafiri ni Meneja wa Kagera Sugar, Mohammed Hussein, ambaye ndiye anatunza kumbukumbu zote za klabu hiyo, pamoja na Mussa Mbaya ambaye ni mmoja wa makocha wasaidizi klabuni hapo.
Hussein alizungumza na gazeti hili akiwa safarini jana mchana na kusema: “Leo (jana) ndiyo tumeianza safari ya kuja huko Dar kwa ajili ya kuitikia wito ambao tuliupata kutoka kwa Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ambayo itakaa Jumanne (kesho) kupitia maombi yetu.
“Sisi katika kikao hicho nitakuwepo mimi mwenyewe, kocha wetu wa makipa (Mbaya) na mhusika mkuu ambaye ni Mohammed Fakhi.”
Kwa upande wake Mbaya alisema: “Tunasafiri na vielelezo vyote, likiwemo daftari maalum la kutunza kumbukumbu za kadi za wachezaji. Mfano, kwa msimu huu wachezaji wetu waliopata kadi tatu ni Seleman Mangoma, George Kavila na Mwita Albert na Ame Ally ambaye mechi iliyopita alipewa kadi ya tatu ya njano, kwa hiyo tuko makini. Tunaamini kama haki ikifanyika, tunachukua pointi zote tatu kwa kuwa hakuna kumbukumbu inayoonyesha Fakhi ana kadi tatu za njano.”
Wakati viongozi hao wa Kagera wakiwa safarini, viongozi wa Simba wameonekana kuanza kuogopa kwamba huenda pointi zao zitapokwa na kupoteza dira ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Akizungumza na Championi Jumatatu juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, alisema anashangazwa kuona Kamati ya Saa 72 inapingwa kwa kuwa maamuzi yaliyotolewa na kamati hiyo yamefuata sheria na kanuni za ligi na kudai kuwa iwapo kamati hiyo haiaminiki ni vyema ikafutwa.
“Kama Kagera wamekata rufaa, hujui wamekata kwa kipengele gani, kwani Kamati ya Saa 72 imefanya maamuzi kwa kufuata sheria na kanuni, nashangaa sasa kuona TFF wanapinga kamati yao wenyewe na kwenda kukaa tena kujadili, basi kama hawaiamini kamati hiyo ni vyema basi ikavunjwa na isiwepo kabisa.
“Mpira wa nchi hii ni upuuzi kabisa huwezi kuunda kamati mwenyewe kisha ukaja kuipinga, tunachojua sisi hiyo ni kamati ya mwisho,” alisema Hans Poppe.
Kama Simba itanyang’anywa pointi tatu za bure na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji, itakuwa na pointi 59, zikiwa ni tatu tu mbele ya Yanga huku Yanga wakiwa na michezo miwili mkononi.
Hiyo itamaanisha kwamba ndoto zao za kuchukua ubingwa msimu huu zitakuwa zinafifia kama siyo kupotea kabisa.

SHOO YA HARMORAPA, JUMA NATURE, MSAGA SUMU, DULA MAKABILA DAR LIVE

Leave A Reply