Familia ya Kichawi -25

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Lakini akiwa amesimama hajafanya lolote, tukasikia mlango mkubwa ukifunguliwa. Tukakimbia na kwenda kusimama mbali kidogo, tukaangalia atakayetoka.

SASA ENDELEA MWENYEWE…

Ghafla, alitoka binti Ngomeleki mwenyewe, akasimama nje na kusema kwa sauti:

“Mimi siyo kama wale. Mimi ninga Mungu wa kweli. Kama mnataka kufa endeleeni tu.”

Alipomaliza kusema hayo akageuka na kuzama ndani huku akifunga mlango. Baba akasema twendeni tu ilimradi amefunga mlango.

Mama alitangulia mbele hadi pale, akasimama palepale pa mwanzo, akasema maneno, wote tukazama ndani.

Kufika ndani tu, mama akanasa miguu chini halafu moto mkali sana ukazuka ndani, mimi nikakimbilia mlango mkubwa, nikaufungua na kutoka mbio. Sikusimama hadi nyumbani.

Ile naingia tu, mara, akaingia baba, kaka na dada. Dada alikuwa akilia sana huku akisema mama amekufa. Tukaanza kulia watoto wote sasa. Baba alitutuliza akitaka kuongea mawili matatu.

“Hebu nyamazeni basi tuongee kidogo,” alisema baba kwa sauti iliyojaa uchungu.

Tulinyamaza huku tukimwangalia kwa sura yenye matumaini kwake.

“Sikilizeni wanangu. Si muda wa kulia huu, tuangalie mbele. Kama kimetokea ina maana tayari kimetokea, nini kingine?” alisema baba.

Hatukumwelewa kwa kweli. Tulimuuliza ana maana gani kusema vile na nini hatima ya mama yetu kule kwa binti Ngomeleki.

“Mama yenu ni kweli ameshafariki dunia lakini maiti yake ipo chumbani, amekufa ghafla.”

Tuliangua tena kilio, baba akafanya kazi ya ziada kututuliza akisema kuwa, kama tutatumia muda ule kulia vile, kuna madhara kwa vile tumo ndani ya vita nzito kati yetu na watu wa mitaani.

Hapa naomba niseme kidogo kuhusu kauli ya baba kwamba, mama alifia nyumbani kwa binti Ngomeleki lakini baba akasema maiti ipo ndani.

Siku zote, mchawi anapopigwa au kukumbwa na z                  ahama nzito ya kiuchawi kama vile kunaswa anapokuwa amekufa maana yake mwili hauwezi kuwa pale alipofia. Hii inatokana na ukweli kwamba,  mchawi anapoondoka nyumbani kwake na kwenda kuwanga, kitandani anaacha alama yenye kuonesha yeye yupo.

Hata sisi tulikuwa tukitoka kwenda kuwanga, vitandani tulikuwa tukiacha vitu. Vitu hivyo ni kinu, mgomba au mtwangio.

Inapotokea ukaingia kwenye chumba anacholala mchawi akiwa ameondoka kwenda kuwanga, kitandani pake utamkuta amelala na hata ukimfunua shuka kama atakuwa amejifunika gubigubi, utamwona ni yeye. Kasoro ni moja tu, wao huwa hawazungumzi zaidi ya kuangalia tu.

Kwa hali hiyo sasa, ndiyo maana inapotokea mchawi kanaswa kwenye kuwanga, amekufa, maiti yake inakuwa ipo kitandani nyumbani tu na si kule alikonasiwa.

Basi, baba alisema iwe isiwe ni lazima kifo cha mama kiwe cha siri, majirani wasijue kwani hata wakijua hakuna atakayefika kumzika.

“Baba inawezekana mama afe tusiseme kwa majirani, mbona itakuwa vigumu sana baba?” aliuliza dada akimjia juu baba.

“Mimi nimesema. Sasa kama mnataka kubishana na baba yenu endeleeni kubisha,” baba naye alimjibu dada.

Lakini mimi pia nilikubaliana na baba kuhusu kuficha kifo cha mama kwani kusema kungetoa picha mbaya zaidi kwa majirani, kwanza wangetususia.

“Halafu tutamzikaje baba?” nilimuuliza baada ya kuona hoja yake ni ya kweli.

“Hatazikwa. Mnajua kule kwenye kilinge mama yenu alikuwa anadaiwa mtu mmoja. Sasa kifo chake tutakitumia kulipa mtu aliyekuwa akidaiwa,” alisema baba huku akituangalia sana nyuso zetu zinasomekaje!

“Baba ina maana mama aliwe nyama?” dada alidakia.

“Asipoliwa yeye kati yenu mmoja wenu anaweza kutakiwa kutolewa kwa ajili ya deni. Hapa ninapoongea na nyie muda wowote watakuja wenzetu  kwani wameshajua kuna mmoja katika kundi ameaga dunia.

“Na lengo la kuja ni kutaka kuhakikishiwa kwamba deni la marehemu litalipwaje na nani atalisimamia?”

Hapa nataka kusema kidogo kwamba, katika mambo ambayo wachawi wapo makini nayo ni suala la deni la mtu.

Kama mchawi alitakiwa kumtoa mmoja wa watu wake wa karibu kwa ajili ya kuliwa nyama halafu akawa hana, akasema anakopa, yaani ale nyama za wenzake yeye atakuja kulipa, lazima atalipa. Awe amekufa, awe hajafa.

Ndiyo maana, umewahi kusikia mchawi amekufa mahali baada ya siku chache, mtoto wake naye anafuatia.

Ili kujua kilichoendelea, usikose kusoka kwenye gazeti hili wiki ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS
GLOBALBREAKINGNEWS.JPG

Toa comment