The House of Favourite Newspapers

Fedha za Majini Zilivyoniendesha Puta-2

0

ILIPOISHIA

“Sasa sijajua bado, tukio lenyewe limetokea ghafla sana. Nahitaji kwanza kushauriana na mama yake.

“Basi ngoja nimpe simu uzungumze naye.”

“Haya mpe.”

Baada ya sekunde chache nikasikia sauti ya mke wangu kwenye simu. Alikuwa bado analia.

“Hebu nyamaza kwanza tushauriane. Shemeji ameniuliza kuhusu mazishi lakini sikuwa na jibu.”

“Mimi nitakuja kesho asubuhi. Msizike mpaka nifike,” mke wangu alijikaza akaniambia.

“Kama utaondoka asubuhi, kila ilivyo utafika huku usiku. Kwa hiyo tutazika usiku utakapofika.”

“Nadhani nitakuja peke yangu. Huku baba amezidiwa tena. Kaka atabaki.”

 SASA ENDELEA…

Sawa.”

 “Basi ni hivyo.”

 “Vizuri, nakutakia safari njema.”

 Baada ya kuzungumza na mke wangu nilimueleza baba kuwa tutazika usiku wa kesho yake baada ya mke wangu kuwasili kutoka Dodoma.

 “Amekwambia atawasili saa ngapi?” akaniuliza.

 “Atafika usiku huo huo.”

 “Watu wengi wananiuliza kuhusu mazishi lakini nimekuwa sina jibu, sasa nitawaeleza kuwa mazishi yamepangwa  kufanyika kesho usiku.”

 “Waeleze hivyo. Na tumeyapanga muda huo kwa sababu ya kumsubirisha mama yake, vinginevyo tungeweza hata kuzika kesho mchana.”

 Ilipofika saa tano usiku, mke wangu alinipigia simu tena akaniuliza kilichokuwa kinaendelea nikamueleza. Akaendelea kunisisitizia kuwa tusizike mpaka atakapowasili.

 “Tumeshapanga kuwa mazishi yafanyike baada ya wewe kufika.”

 “Sawa. Mimi nimeshajiandaa, kesho asubuhi naondoka,” mke wangu akaniambia.

 Usiku wa siku ile hatukulala. Mimi na baba tulikuwa tukitafakari kuhusu msiba ule uliotutokea ghafla.

 Asubuhi kulipokucha tuliendelea kupokea wageni waliokuja kuomboleza kwenye msiba huo. Baadhi ya watu walitoka katika vijiji vingine vya karibu.

 Matayarisho ya mazishi yaliendelea hapo nyumbani hadi jioni. Mke wangu alifika na basi lililowasili saa moja usiku. Alinipigia simu kunijulisha kuwa alikuwa ameshawasili Stendi ya Manundu Korogwe. Nikawaagiza wifi zake waende wakampokee.

 Wakaenda kumpokea na kuja naye lakini walipofika tu hapo nyumbani kilio kikaanza upya. Mke wangu alianza kulia na wifi zake nao wakalia pamoja naye.

“Mwanangu umepatwa na nini…mwanangu umepatwa na nini…mbona mwanangu umenitoka ghafla…” Ndiyo maneno aliyokuwa akitamka mke wangu.

 Ndugu na jamaa walijaribu kumnyamazisha. Akanyamaza na kuingia katika chumba kilichokuwa na mwili wa marehemu lakini alipouona mwili wa mwanawe akaanza tena kulia.

 Kwa vile tulipanga atakapofika mke wangu, mwili wa marehemu utolewe kwa ajili ya kwenda kuzikwa, shughuli hiyo ikafanyika.

 Mpaka inafika saa tatu usiku, jeneza lilikuwa limeshafikishwa makaburini. Baada ya mazishi tukarudi nyumbani.

 Mke wangu aliendelea kubaki hapo Korogwe kwa wiki nzima kabla ya kurudi tena Dodoma.

 Hazikupita hata wiki mbili baba yangu naye akapatwa na homa ghafla. Nilimpeleka hospitali nikidhani alikuwa na malaria lakini baada ya kuchukuliwa vipimo aligundulika hakuwa na malaria. Hata hivyo, alipewa tembe za kwenda kumeza nyumbani.

 Baada ya kutumia tembe hizo alipata nafuu kidogo lakini zilipita  karibu wiki mbili baba alikuwa ndani akijiuguza.

 Usiku mmoja akaniita na kuniambia.

 “Mwanangu naona kiza mbele yangu. Kuna kitu nataka kukwambia.”

 Aliponiambia hivyo nilishituka nikamkazia macho na kumuuliza.

 “Unataka kuniambia nini baba?”.

 “Cha kwanza ninachotaka kukwambia ni kuwa endapo nitafumba macho siku yoyote, urithi wako uko chini ya mvungu wa kitanda nilicholala,” akaendelea kuniambia huku akielekeza mkono wake chini ya mvungu wa kitanda.

Mimi nilikuwa nimenyamaza nikimsikiliza kwa makini.

 “Sasa kuna majukumu ambayo nataka nikukabidhi lakini si hapa. Itabidi tutoke usiku huu twende mahali fulani.”

 Hapo nikamuuliza.

 “Ni majukumu gani hayo baba na hapo mahali unapotaka twende usiku huu ni wapi?”

 “Nifuate tu.”

 Baba alikuwa ameshainuka kwenye kitanda. Kitu ambacho kilinishangaza ni kuwa alipoinuka alikuwa na nguvu mpaka nikahisi kuwa alikuwa amepona.

 Nikapata matumaini. Na mimi nikanyanyuka na kumwambia.

 “Haya twende.”

 Nikatoka naye pale nyumbani. Nakumbuka ilikuwa saa saba usiku.

 “Ni usiku huu, chukua silaha,” akaniambia.

 “Kwani ni mbali sana baba?”

 “Ni mbali kidogo.”

 “Kwa nini tusiende kesho?”

 “Mimi nataka twende leo.”

 Nikarudi ndani na kuchukua sime. Nilipotoka, nikamwambia.

 “Haya twende.”

 Tukaanza safari.

 “Acha mimi niwe mbele yako,” baba akaniambia wakati tunakwenda.

 Aliponieleza hivyo licha ya kwamba nilitamani sana nitangulie mbele, nikamuacha atangulie.

Hata hivyo, nilitamani kujua lengo la baba kunipeleka huko tulikokuwa tukienda usiku ule lakini sikupata jibu.

Njia tuliyokwenda ilikuwa ikielekea lilikokuwa shamba lake. Nikahisi tulikuwa tunakwenda shambani kwake. Lakini tulipolikaribia shamba hilo tuliliacha upande wa kushoto tukashika njia ya upande wa kulia.

 Kimoyomoyo nilikuwa nikijiuliza, baba alikuwa ananipeleka wapi usiku ule. Kwa mbali tulikuwa tukisikia milio ya fisi pamoja na ya wanyama wengine.

 Kile kitendo cha baba kuwa mbele yangu kilinizuia nisimuulize maswali mengi yaliyokuwa yakipita akilini mwangu.

 Baada ya muda kidogo tukawa tumeingia kwenye njia iliyoelekea kwenye pori. Ilikuwa njia nyembamba ya kupita kwa miguu.

 Sehemu yenyewe ilikuwa inatisha lakini baba alikuwa akitembea bila kuonesha wasiwasi wa aina yoyote.

“Mh! Sijui tunaelekea wapi na baba mbona hana hofu yoyote?” nilijiuliza bila kupata majibu.

Mimi niliyekuwa nyuma yake nikiwa nimeshika sime mkononi ndiye niliyekuwa nikitazama kila upande kwa wasiwasi.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia hapahapa Jumanne ijayo.

Kitabu changu cha “NILIVYOGEUZWA PAKA” sasa kipo mitaani. Usikose uhondo uliomo kwenye kitabu hicho. Kwa mawasiliano ya kukipata piga namba 0712 777 737.

Leave A Reply