The House of Favourite Newspapers

FURAHA KWA ZARI, HUZUNI KWA MONDI

NILISIKILIZA mahojiano ya Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ mara baada ya kutua Bongo juzikati katika ziara yake ya kibalozi. 

 

Alipoulizwa kuhusu suala la watoto wake aliozaa na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tiffah na Nillan kuja Bongo kwa baba yao, alionekana kuwa mzito kidogo kulizungumzia.

 

Alipoulizwa kuhusu suala la watoto wake hao aliozaa na Diamond kuwa raia wa Sauz, alisema ilitokea tu. “Tiffah alizaliwa hapa (Bongo), lakini kwa sababu mimi naishi Sauz na ndiye mama yake, nikaona ni bora tumpe uraia wa Sauz, iwe rahisi katika suala zima la malezi. Kuhusu Nillan yeye ilitokea kabisa akazaliwa kulekule Sauz hivyo moja kwa moja akawa raia wa Sauz,” alisema Zari. 

TUJIFUNZE KIDOGO

Kwa namna yoyote ile, kutokana na kuwa Zari na Diamond kwa sasa hawana tena uhusiano wa kimapenzi, maana yake ni kwamba, watoto hao wawili watakuwa wanakuja Tanzania kama vile wanakuja kutembea.

 

Si kwamba wanakuja nyumbani kwao kwa maana ya nyumbani kwa baba yao bali watalazimika kufuata taratibu za kuingia nchi nyingine kama ambavyo wageni wengine hufanya wanapoingia nchini au kama vile Diamond anavyofanya anapokwenda Sauz au nchi nyingine kutembea.

 

MALEZI YAO

Ukweli wa mambo unaonesha kwamba, asilimia 90 ya malezi ya watoto hao yatakuwa Sauz kwa mama yao (Zari). Haina ubishi kwamba watoto hao watakuwa na muda mwingi zaidi wa kuishi na mama kuliko baba yao. Hapa ndipo tatizo linapoanza kuchipukia.

Mazingira yanaonesha itakuwa ni nadra sana Diamond kukutana na watoto wake kutokana na ubize wake binafsi kama msanii, lakini pia mazingira ya Zari kuwa na maisha yake mapya na mwenza wake. Naona zaidi atakuwa akiwasiliana nao kwa njia ya simu, tena hata simu yenyewe itakuwa na masharti kwani Zari sasa hivi ana mtu wake mwingine ambaye ana mipango naye ya kufunga ndoa.

 

Kwa kuwa mwanaume wa sasa wa Zari atakuwa anamtambua Diamond kama zilipendwa wa Zari, hawezi kufurahishwa sana na simu za mara kwa mara za Mondi hata kama itakuwa anataka kuzungumza na watoto. Anaweza kuheshimu kwa maana ya kuwapa, lakini wivu kwenye mapenzi nao upo, anaweza akazuia.

MALEZI YA UPANDE MMOJA

Mara nyingi watoto wanaolelewa na upande mmoja hususan kama hivi mama, hujikuta kwenye matatizo kadhaa. Kwa kupenda au kutokupenda wanaweza kujikuta tu wanampenda zaidi mama na baba akawa kama mtu wa ziada. Diamond asipofanya jitihada za makusudi za kuwaona mara kwa mara wanaye hao, ni rahisi sana watoto nao kujikuta wamejenga chuki tu dhidi yake. Chuki inaweza kuja yenyewe au ya kupandikizwa.

 

Bahati mbaya au nzuri, Zari haoneshi sana uhitaji wa mahitaji kutoka kwa baba yao, hivyo watoto wanaweza kukua wakiamini kila kitu wanakipata kutoka kwa mama. Mimi na wewe hatujui atawaeleza nini watoto kuhusu baba yao, lakini matukio mengi tumeshuhudia juu ya watoto wanaolelewa na upande mmoja. Wengi wanakutana na changamoto ya kuuchukia au kutoujali upande wa pili.

Kama ilivyokuwa kwa Diamond na baba yake, ndivyo inavyoweza kuwatokea Tiffah na Nillan kwa Diamond. Wanaweza kujikuta tu hawana mapenzi naye na mwisho wa siku msanii huyo anayetamba na Ngoma ya Inama asiwe na furaha na wanawe.

 

Diamond anaweza kujikuta hana furaha na watoto wake, wanasoma Sauz, wana uraia wa kule na mama yao pia. Usisa-hau mama yao yuko vizuri kifedha, unategemea nini? Bahati mbaya zaidi, mama yao ameanza ukurasa mwingine wa maisha ya uhusiano hivyo nguvu na akili yote itahamia huko. Hatuombei yatokee mabaya, lakini Diamond anayo nafasi ya kutengeneza ukaribu na wanaye, lakini asipofanya hivyo, naiona hatari ya kuwa mbali na wanaye. Siioni furaha ya watoto kwa baba yao!

Comments are closed.