The House of Favourite Newspapers

Gabo; Unaweza kuvaa viatu vya Kanumba, lakini chunga!

Gabo Zigamba

NIMEKUKUMBUKA leo mkali wa sinema za Kibongo, Gabo Zigamba. Mambo vipi kaka? Pole na hongera kwa mihangaiko ya kila siku. Mwanaume lazima ujitume ili mkono uende kinywani.

Ukitaka kujua hali yangu, mimi ni mzima wa afya. Namshukuru Mungu naendelea kupambana na hali yangu ndani ya mjengo wa Global Publisher. Baada ya salamu hizo, moja kwa moja niende kwenye madhumuni ya mimi kukuandikia barua hii ambayo kila wiki nimekuwa nikimuandikia mtu mmoja maarufu.

Gabo, kwanza nikupongeze, mimi ni mfuatiliaji mzuri wa sinema zako. Naamini uwezo ulionao ni wa hali ya juu na kila anayesoma barua hii ambaye ni mfuatiliaji mzuri wa Bongo Movies, basi ataungana na mimi.

Gabo unajiamini, unajua kutamka maneno yenye mantiki kwenye ‘sini’ ambayo yanaleta ladha kwa msikilizaji.Unajua kubadilika kulingana na sini husika. Ikiwa ni kijijini, unajua, mjini unajua. Kuwa bosi, kuwa mtu wa hali ya chini kwako ni jambo la kawaida kabisa, hongera sana. Namna unavyojua kuuvaa uhusika, naona kabisa ukiziba pengo la marehemu Steven Kanumba ambaye kiukweli alikuwa anajua kwenda na soko la filamu.

Mbali na pongezi hizo, Gabo nataka nikukumbushe kwamba nimekuwa nikifuatilia nyendo zako na kugundua kwamba yawazekana ukawa kidogo na nyodo kama si maringo. Kama mwanahabari, nimepata kusikia waandishi wengi wakikulalamikia kwa kuwa mzito kutoa ushirikiano, jambo ambalo mimi naliona ni tatizo.

Kama hiyo haitoshi, umekuwa mzito sana kutokea kwenye events za watu hususan zile ambazo zinakuhusu wewe mwenyewe moja kwa moja. Nakumbuka hivi karibuni, Kampuni ya Startimes iliwapa shavu la ubalozi wa michuano ya Kombe la Dunia watu maarufu mbalimbali ukiwemo wewe pamoja na muigizaji Wema Sepetu.

Kilichonisikitisha ni kitendo cha wewe kufika kwa kuchelewa katika hafla ya kuwatangaza mabalozi hao, hafla muhimu kwa kuzingatia uzito wa michuano hiyo mikubwa ya dunia. Kwa msanii yeyote mwenye kutazama mbali, hawezi kupuuzia kwa namna yoyote ubalozi wa michuano hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni, mwaka huu.

Watu wamejiandaa, naamini kabisa walikupa mualiko na muda muafaka wa wewe kufika pale Slipway, lakini ukachelewa. Mabalozi wenzako wote waliheshimu na kufika kwa wakati, lakini wewe ukachelewa. Hukuleta picha nzuri Gabo maana jina lako limeitwa mara mbili, kadamnasi iliyohudhuria hafla hiyo ikabaki inatafuta.“Gabo… Gaboo…Gaboo…” uliitwa, lakini mzee hukuonekana eneo la tukio. Kitendo cha wahusika kukuita halafu wewe usiitikie kinadhihirisha kwamba hukuwa umetoa udhuru hivyo waliamini kwamba utakuwa umefika.

Matokeo yake kumbe wewe hukuwa umefika. Hukuona pia hata umuhimu wa kutoa taarifa kwamba utachelewa labda kwa sababu fulani. Hiyo inaonesha ishara ya dharau au kutojali kitu kilichokuwa mbele yako. Hata ulipotokea, hafla ilikuwa inaelekea ukingoni na hata ingia yako mwenyewe uliona jinsi ilivyokuwa ya tabu. Ukawa unajishtukia. Gabo wewe ni msanii mkubwa, unastahili kuwa na nidhamu ili uweze kufika mbali zaidi. Maringo na majivuno yamewafanya watu wengi kufeli kwenye maisha.

Rekebisha hiyo kasoro, naamini utakuwa msanii mkubwa sana huko tuendako kama utaishi katika misingi ya nidhamu na kutokulewa sifa. Ni matumanini yangu utakuwa umenisoma, kila la kheri katika kazi zako.

Mimi ni nduguyo;

Erick Evarist

 

Comments are closed.