The House of Favourite Newspapers

Gerald Mdamu Mchezaji wa Polisi Tanzania Afunguka Kurudi Uwanjani Msimu Ujao

0
Mchezaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu.

 

GERALD Mathias Mdamu, ni mchezaji wa Polisi Tanzania ambaye msimu huu hajafanikiwa kucheza kwenye timu hiyo kutokana na ajali aliyoipata Julai, mwaka jana iliyosababisha kuvunjika miguu yote miwili.

 

Ajali hiyo ilitokea Julai 9, 2021 wakati kikosi cha timu hiyo kikitoka mazoezini wakati kikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar.

 

Mdamu ambaye anacheza nafasi ya ushambuliaji, kwa sasa yupo nyumbani kwake Tabata Kimanga, Dar es Salaam akiuguza majeraha yake hayo.

 

Ikiwa imepita takribani miezi kumi tangu apate majanga hayo, Spoti Xtra limemtembelea kwa ajili ya kujua hali yake ambapo kwenye mahojiano, amefunguka haya. “Kwa sasa hali yangu inaendelea vizuri, kilichobaki ni mazoezi na baadhi ya vidonda ambavyo havijakauka vizuri ndio navihangaikia.

 

“Nafanya mazoezi ya kutembea kwenye mchanga bila gongo ila kwenye maeneo ambayo ardhi ni ngumu natumia gongo.

 

BADO UNAENDELEA NA MATIBABU KWENYE HOSPITALI YA MUHIMBILI?

“Kliniki ya Muhimbili nilishaiacha muda mrefu, kwa sasa naendelea na matibabu ya tiba asili. “Unajua mnapokaa watu wengi mnapata kitu, mimi nilipata ushauri wa watu kutokana na huduma iliyokuwa hapo kwenye kliniki inayoitwa Kigoma iliyopo Vingunguti.“Wakati nimeanza kwenda ndio ikaanza kuingiliana na tarehe ya kwenda Muhimbili, nikatumia zile dawa za tiba asili kwa wiki moja, hivyo nikaona bora niendelee na tiba asili niache kwanza Muhimbili.

 

“Sisemi kwamba Muhimbili hawajui ila niliona matibabu ya tiba asili yamenisaidia kwa haraka zaidi na mishipa iliwahi kuunga kwani nilikuwa siwezi kunyoosha mguu lakini baada ya kuanza kutibiwa huku kwingine ndio nikaona kutanisaidia kwa haraka zaidi. “Kwa sasa ni muda wa miezi minne nimekuwa nikifanya matibabu ya asili lakini nilikaa hospitali kwa miezi sita hadi saba nikaona bado mambo magumu wakati kule nilitumia mwezi mmoja tu nikaona mabadiliko sana.

KLINIKI UNAENDA KILA BAADA YA MUDA GANI NA MALIPO YAPOJE?

“Huwa naenda kuosha kila baada ya siku mbili, wakati naanza nilitoa hela yote ila kinachonipa shida sasa hivi ni usafiri kwani kila ninapoenda natoa elfu nane na hicho kitu kinanisumbua sana.

 

POLISI TANZANIA WANAHUSIKA KWENYE MATIBABU YA SASA?

“Kwa huku ninapofanyia kliniki kusema kweli hawajanichangia kitu chochote ila wananilipa mshahara tu ndiyo huohuo ambao nautumia kwa ajili ya matibabu.

 

VIONGOZI WA POLISI TANZANIA HUWA WANAKUJA KUKUTEMBELEA AU KUPIGA SIMU KUJUA HALI YAKO?

“Kwenye suala la uongozi kunipigia simu kiukweli hawapigi, siku ile walikuja kuniona, lakini baada ya hapo sikuongea na mtu yeyote wala kutembelewa.

“Suala ambalo lipo siku ile waliyokuja walisema watanifanyia sapraizi, ila hakuna kitu mpaka sasa hivi, sio kwamba naongea kwa ubaya, nasema ukweli, siwezi kuficha kitu kama hicho.

 

 

MKATABA WAKO UNAMALIZIKA MWISHONI MWA MSIMU HUU, JE VIONGOZI WAMEWAHI KUKUTAFUTA JUU YA HILO?

“Najua mkataba wangu unaelekea mwishoni ila viongozi wa Polisi Tanzania hawajawahi kuniita juu ya suala hilo, lakini

ninamshukuru Mungu kwa hatua niliyofikia kwa sasa imebaki kidogo tu nina uhakika msimu ujao nitakuwa kwenye ligi labda itokee ishu nyingine.

 

“Kama tutakaa na viongozi wa Polisi Tanzania kwa msimu ujao nitakuwa tena huko kwani najua mashabiki wa Moshi wamenimisi sana, pia nawashukuru Wa­tanzania wote kwani wao wamenipa moyo sana wa kuona kwamba sipas­wi kukata tamaa, naweza kusimama tena na kuwa kama mwanzo au zaidi ya hapo. Sina cha kuwalipa ila Mungu atawalipa.

 

 

DOKTA AMEKUAMBIA UTAANZA LINI MAZOE­ZI MAGU­MU?

“Kwa dokta kuniambia mazoezi ya kuanza kukimbia alisema kuan­zia mwezi wa sita hadi wa saba nitaanza mazoezi ya nguvu tofauti na sasa am­bapo nafanya mazoezi me­pesi.

 

 

ULIPATA NAFASI YA KUCHEZA NA GEORGE MPOLE POLI­SI TANZANIA, NI MTU WA AINA GANI?

“Mpole ni mtu wa kushauriana na wenzake, nilikuwa na­pata nafasi ya kucheza yeye hapati, alikuwa hakati tamaa, lakini mimi nilimsifia sana kwenye suala la upigaji wa faulo na anajua sana kuipiga mipira hiyo.

“Nilikuwa namui­ga sana na sasa hivi ninavyomuona ana­fanya vizuri hata sis­hangai, nina uhakika hata akipata nafasi ya kwenda kwenye hizi timu kubwa atafanya vizuri endapo atapata nafasi ya kucheza muda mwingi.

 

 

NI MCHEZAJI GANI AMBAYE AMEKUWA KARIBU SANA NA WEWE KATIKA KIPINDI HIKI?

“Mtu ambaye ananitafuta sana ni Awesu Awesu, wengine nilikuwa hata sina mawasiliano nao walikuwa sio marafiki zangu, lakini nafurahi sana wanavyonitafuta, sio kwamba nasema marafiki zangu wananikataa, hapana, najua labda ni kwa sababu ya ubize kwenye ligi,” alimaliza Mdamu.

HAJI MANARA AANIKA UKWELI WOTE – “FEI TOTO BADO YUPO SANA, MORRISON MALI ya SIMBA”

Leave A Reply