The House of Favourite Newspapers

GGM, TACAIDS Kuzindua Kilimanjaro Challenge Ili Kutokomeza Ukimwi

Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inatarajia kuzindua zoezi la upandaji wa mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro Challenge 2019), na kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa mwaka 2019 kwa ajili ya afua za UKIMWI nchini.

 

Kilimanjaro Challenge ni mfuko muhimu unaoshirikiana na taasisi za nje na ndani ya nchi katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI kwa jamii ya Kitanzania na Dunia kwa ujumla ili kuwapa matumaini ya kuhakikisha jamii inabaki bila kuathiriwa na VVU/UKIMWI katika miaka ijayo.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Leonard Maboko alisema takwimu zilizotolewa na Tume ya Kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), zimeonesha kupungua kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka asilimia 5.1 % mwaka 2011/ 2012 hadi asilimia 4.7% mwaka 2016/17.

 

Alisema mwaka wa 2016, inakadiriwa kuwa watu milioni 1.5 nchini wanaoishi na VVU na UKIMWI hadi sasa watu 225 wanapata maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa siku. Ugonjwa huu umewaathiri zaidi vijana na watoto yatima zaidi. Tunahitaji kubadilisha hali hii.

 

Aidha, aliongeza kuwa lengo la kukusanya fedha ni kuweza kusaidia serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia sifuri tatu. Sifuri katika maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa, sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.

 

“TACAIDS kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na wadau wengine kwa kupitia mpango huu wa Kili Challenge tunapenda kutoa mchango na ushirikiano wetu kwa Taifa ili kutunisha mfuko utakaowezesha kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Tuna matumaini ya kujenga timu imara yenye hamasa ya kupambana na janga hili.

 

“Tunatoa wito kwa makampuni na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, wajitokeze ili tusaidiaane kutunisha mfuko wa Kili Challenge na mwishowe kufikia malengo yetu ya kuhakikisha tunakuwa na kizazi kisicho na maambukizi ya VVU/ UKIMWI,” alisema Dkt. Leonard Maboko.

 

Makamu wa rais miradi endelevu wa kampuni ya AngloGold Ashanti, GGM, Simon Shayo alisema shughuli hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 4 Juni mwaka huu na kuzinduliwa na Waziri wa Uwekezaji Angellah Kariuki ambapo atafanya zoezi la ugawaji wa fedha zilizokusanywa mwaka jana 2018 zilizopatikana baada ya wadau mbalimbali kupanda na kuendesha baiskeli na kuzunguzuka Mlima Kilimanjaro.

 

Alisema kuna tatizo linaloikabili jamii sasa ambapo baadhi yao wanawatenga na kukataa kuishi na watu wenye maambukizi ya VVU/ UKIMWI, kutokana na tatizo hilo Mgodi wa Dhahabu wa Geita, umeamua kuwekeza katika mradi huu kwa kuuwezesha kuwa mradi wa kitaifa na si wa GGM.

 

“Huu ni mwaka wa 18 sasa tangu Kili Challenge ianze. Pia zaidi ya watu 800 kutoka pande mbalimbali za dunia wameshiriki. Taasisi zaidi ya 40 zimefaidika kutokana na utunishaji wa mfuko huu kwa sababu taasisi ambazo hazina fedha za kuendesha kampeni na shughuli mbalimbali za mapambano dhidi ya VVU/ UKIMWI zimekuwa zikifaidika na mfuko huu. Pamoja na mambo mengine, watoto waliopoteza wazazi wao sasa wanaweza kutabasamu tena kutokana na uangalizi pamoja na upendo wanaoupata kutokana na mfuko huu.

 

“Tunapenda pia kutambua ushirikiano wa kampuni na taasisi mbalimbali kama vile ACACIA, AKO, Mantrac, NSSF, PUMA, TOYOTA, Prime Fuels, Coastal Aviation, Airtel, Capital Drilling, PPF, Serena Hotel, Geita Power Limited, SGS na wadau wengine tunaoshirikiana nao. Tunawashuruku kutokana na ushirikiano wenu katika mapambano dhidi ya VVU/ UKIMWI hivyo, tunaweza kufurahia mafanikio haya kwa kuwa na mradi endelevu,” aliongeza Simon Shayo.

 

Balozi wa Kili Challenge ambaye pia ni mwanamuziki maarufu nchini Tanzania, Mrisho Mpoto alisema jamii inapaswa kuacha kuwa tegemezi kwa sababu ina uwezo wa kujisimamia kwa kutumia vyombo vya habari, na watu wenye ushawishi mkubwa na kwa pamoja; UKIMWI unaepukiki.

NA MWANDISHI WETU

 

BREAKING: Askofu GWAJIMA Atinga IKULU “LAZIMA mayai YAVUNJIKE”

Comments are closed.