The House of Favourite Newspapers

Global Publishers sasa kutoa zawadi ya nyumba mpya

0

nyumba-adBAADA ya kujihusisha na misaada mbalimbali ya kijamii na kiutu, Kampuni ya Global Publishers Ltd, wachapishaji wa magazeti pendwa na lile bora la michezo nchini Tanzania, imekuwa ya kwanza kutoa zawadi ya nyumba kwa wasomaji wake katika promosheni inayotarajiwa kuanza kesho Desemba 11, mwaka huu.

Kumbukumbu zinaonesha kwamba, michezo ya kubahatisha imekuwa ikichezeshwa na kampuni mbalimbali za habari, lakini zawadi kubwa zaidi kutolewa ni magari.

Meneja Mkuu wa Global, Abdallah Mrisho amesema kampuni imeamua kutoa zawadi ya nyumba ikiwa ni shukrani kwa wasomaji wake huku ikiamini shindano hilo litaongeza imani ya wasomaji wa magazeti ya Global na litabadili maisha yao, hasa kwa atakayebahatika kushinda nyumba hiyo.

“Tunaamini maisha bora ni pamoja na nyumba bora. Sasa promosheni hii ni changamoto kwa wasomaji wetu lakini lengo kubwa ni kuwarudishia shukrani kwa sababu tunaamini nao ni sehemu ya mafanikio yetu,” alisema Mrisho.

Global Publishers inayochapisha Magazeti ya Championi, Amani, Uwazi, Ijumaa Wikienda, Risasi na Ijumaa, imekuwa ikijihusisha na mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo zawadi kupitia mashindano na promosheni.

Miongoni mwa misaada ambayo kampuni hiyo imekuwa ikitoa ni kuisaidia jamii kukabiliana na magonjwa mbalimbali huku ikiwa haina uwezo wa kumudu gharama za matibabu kwa kuwapeleka India na hospitali za hapa nchini.

Misaada mingi ya matibabu imekuwa ikiwalenga watoto wenye vichwa vikubwa na uti wa mgongo wazi, wenye vimbe mbalimbali ambazo zimeshindwa kufanyiwa upasuaji hapa nchini.

Global Publishers pia imekuwa ikiunga mkono juhudi za serikali katika suala la maendeleo ambapo imepata kutoa gari la wagonjwa (Ambulance) huko Buchosa wilayani Sengerema, Mwanza.

Aidha, kampuni imekuwa ikitoa misaada kwa jamii maskini nchini kwa kuziwezesha mitaji baadhi ya familia na kugharamia elimu kwa watoto wenye uwezo kielimu na nia ya kujiendeleza lakini wanashindwa kutokana na kukosa ada.

“Sisi siyo matajiri, hatuna fedha za kutosha lakini tunaguswa na maisha ya Watanzania wenzetu ndiyo maana tuko tayari kugawana hata kile kidogo tunachopata,” hayo yanasemwa na Eric Shigongo, Mkurugenzi Mtendaji wa Global.

Shigongo ambaye licha ya kufahamika kwa utunzi mahiri wa hadithi zinazogusa jamii, amefanikiwa pia kuwatia moyo na kuwafundisha wanajamii wengi kuhusu ujasiriamali huku akihimiza kujiamini na kuthubutu katika maisha.

“Lengo letu kubwa ni kuona maisha ya mtu mmojammoja yanabadilika, kwa sababu kadiri jamii inavyokuwa na hali nzuri kimaisha, ndivyo maendeleo yanavyopatikana. Hatuko kwa ajili ya kufanya biashara na kukusanya fedha, tuko kwa ajili ya kuibadili jamii iishi maisha bora na tunapoona mmoja anabadilika, kwetu ndiyo furaha,” anaongeza.

Tangu mwaka 2000 hadi sasa, Global Publishers imekuwa ikifanya Bahati Nasibu na kutoa zawadi mbalimbali kwa ajili ya wasomaji wake.

Jumla ya magari matano, pikipiki kadhaa, safari ya kwenda China kwa msomaji wa Gazeti la Ijumaa Wikienda na pesa taslimu shilingi milioni kumi zimetolewa kwa wasomaji wake hadi sasa.

Magari yaliyowahi kutolewa kama zawadi za juu ni Toyota Starlet, Toyota Vitz, Mitsubishi Pajero, Mercedes Benz, Toyota Noah na Nissan March.

Zawadi ya nyumba inakuwa ya kwanza na ya aina yake nchini kutolewa na Global Publishers Ltd, hivyo wasomaji wanahimizwa kuichangamkia mchezo utakapoanza.

Leave A Reply