The House of Favourite Newspapers

Godbless Lema Akubaliwa Kukata Rufaa ya Dhamana

lema

ARUSHA: Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imelikubali ombi la  Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema,  la kuongezewa muda wa kuwasilisha Notisi ya nia ya kukata rufaa ya dhamana yake.

Akitoa uamuzi wake leo mchana, Jaji Dk. Modesta Opiyo wa Mahakama hiyo, alisema Mahakama hiyo imeruhusu maombi ya kuwasilisha Notisi ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa ya dhamana yake.
Jaji Opiyo amesema hoja za Upande wa serikali zilizowasilishwa na Wakili Hashim Ngole za kudai waleta maombi hayo walikuwa wazembe na walichelewa siku nne kuwasilisha Notisi baada ya rufaa yao kuondolewa na Jaji Fatuma Masengi Desemba 2 hazina mashiko.
Alisema kuondoa kesi mahakamani haimaanishi kuwanyima fursa ya kupigania nia ya kukata rufaaa, bali milango inakuwa wazi haijafungwa.
Aidha amesema siku nne zinazolalamikiwa kuwa walichelewa kutoa maombi hayo, mahakama inaona hoja hizo hazina mashiko sababu siku mbili kati ya hizo zilikuwa siku za mapumziko Jumamosi na Jumapili, hivyo walitumia siku mbili kuandaa nyaraka na kuleta maombi hayo.
Pia alisema katika maombi hayo wametoa pia sababu za nia ya kutaka kukata rufaa na sababu hizo ziko wazi.
“Katika hili hakuna uvunjifu wowote wa sheria uliofanywa na kutokana na hilo Mahakama hii inatumia busara zake kuruhusu maombi haya ya kutoa Notisi ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa juu ya dhamana yake Mbunge huyu,” alisema Jaji Opiyo.
Amesema Mahakama inatoa siku kumi pekee kuanzia uamuzi huo utolewa mleta maombi (Lema) kuwasilisha Notisi yake ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa hadi tarehe 30 shauri hili likakaposikilizwa tena.
Baada ya kutolewa kwa maamuzi hayo, tayari Wakili Sheck Mfinanga ameshakata Notisi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na kupokelewa.
Mfinanga amesema wanasubiri mahakama ili wapangiwe Jaji waendelee na kesi hiyo ya hatma ya dhamana ya Lema.

Irene Uwoya Afanya Kufuru Birthday Yake, Amkumbuka Samwel Sitta Aliyezaliwa Naye Des. 29

Comments are closed.