The House of Favourite Newspapers

Gomes Awapa Sakho, Banda dk 270 Simba

0

KOCHA Mkuu wa Simba Mfaransa, Didier Gomes amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa viungo wake watatu Ousmane Sakho, Peter Banda na Duncan Nyoni ni wazuri huku akiwapa michezo mitatu dakika 270 ya Ligi Kuu Bara ili kudhibitisha ubora wao.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, kocha Gomes anaamini ugeni wa ligi ndiyo umewafanya washindwe kuonyesha ubora wao katika michezo miwili ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na ule wa ligi dhidi ya Biashara United.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Gomes ana matumaini makubwa baada michezo mitatu ya ligi nyota hao watabadilika na kuzoea ushindani wa ligi na kufanya vema.

 

“Kocha anafurahishwa na viwango vya Banda, Sakho na Nyoni ambao wote usajili wao ulipendekezwa na yeye katika msimu huu. Lakini ameomba wapatiwe michezo mitatu ya ligi kwa ajili ya kuwazoea wachezaji wenzao na mazingira ya timu.

 

“Kwani Simba siyo timu ndogo ni kubwa yenye mashabiki wengi hivyo ni lazima kwanza wazoee vitu hivyo ili waendane na kasi ya timu,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Simba kwa kupitia Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo, Crescentius Magori hivi karibuni alisema kuwa: “Tumefanya usajili bora katika msimu huu, kwani wachezaji wote wana hadhi na ubora wa kuichezea Simba, suala la muda wachezaji hao kuonyesha ubora wao.”

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply