The House of Favourite Newspapers

Gomes Awekewa Mtego Simba SC

0

KOCHA Mkuu wa Simba Mfaransa, Didier Gomes, ana kibarua kigumu katika kupanga kikosi chake cha kwanza kutokana na ushindani wa namba uliopo katika kuelekea msimu ujao.

 

Hiyo ni kutokana na usajili bora uliofanywa kuelekea msimu ujao ambayo imefanya usajili wa wachezaji nane ambao imewasajili katika kuhakikisha wanafanya vema katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara katika msimu ujao.

 

Hii unaweza kusema kuwa ni kama amewekewa mtego wa kuhakikisha kikosi hicho kinatwaa tena mataji yote makubwa sambamba na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kwani wachezaji aliohitaji amesajiliwa na uongozi wa timu hiyo hivyo hakuna kisingizio.

 

Wachezaji hao iliowasajili Simba ni Peter Banda, Ousmane Sakho, Duncan Nyoni, Sadio Kanoute, Inonga Baka ‘Varane’, Jeremiah Kisubi, Denis Kibu na Yusuf Mhilu. Wengine ni Israel Mwenda, Jimmyson Mwanuke na Abdulsamad Kassim Ali.

 

Usajili huo utampa ugumu kocha huyo katika kupanga kikosi cha kwanza kutoka kwa wachezaji wa zamani walioonyesha ubora katika msimu uliopita na hao wapya waliosajiliwa.

 

Ushindani huo unatarajiwa kuwa hivi, safu ya magolikipa inatarajiwa kuwa na Aishi Manula na Kisubi ambaye amesajiliwa kwa ajili ya kumpa changamoto Manula baada ya akina Beno Kakolanya na Ally Salim.

 

Mabeki wa kulia yupo tayari mkongwe Shomari Kapombe ambaye katika msimu ujao atapata ushindani kutoka kwa Mwenda aliyesajiliwa kutoka KMC ni baada ya David Kameta ‘Duchu’ kushindwa kutoa ushindani kabla ya kutolewa kwa mkopo.

 

Huku kwenye beki ya kushoto, yupo Mohammed Hussein ‘Zimbwe’ ambaye katika msimu huu atakutana na ushindani kutoka kwa Gadiel Michael ambaye msimu uliopita alijiuliza, hivyo msimu ujao ataonyesha mabadiliko makubwa.

 

Beki namba nne, yupo Joash Onyango, Kennedy Juma na Baka ambaye ameletwa kwa ajili kwa kuiboresha safu ya ulinzi hapo kuna kibarua kigumu kwa Gomes.

 

Namba tano, wapo Pascal Wawa na Erasto Nyoni mmoja ndiye anatakiwa kucheza katika kikosi cha kwanza. Hivyo kipo kibarua kigumu.

 

Kiungo mkabaji namba sita, Abdulsamad aliyesajiliwa anatarajiwa kukutana na upinzani kutoka kwa Taddeo Lwanga, Jonas Mkude na Mzamiru ambaye hivi sasa yupo katika kiwango bora. Winga wa kulia, namba saba atakuwepo Banda akichuana vikali na Mhilu ambao wote wamesajiliwa na timu hiyo.

 

Namba nane, kiungo mchezeshaji Kanoute atakuwepo na Rally Bwalya ambao wote wapo katika kiwango kizuri. Na namba tisa, yupo nahodha John Bocco, Meddie Kagere na Kisubi aliyejiunga na Simba katika msimu huu, anatarajia kuwapa ushindani wakongwe hao.

 

Kumi yupo Sakho atakayepambana na Chriss Mugalu ambaye katika msimu uliopita alionyesha kiwango bora. Na kumi na moja atakuwepo Duncan na Mwanuke ambao wote wapya wanapambania nafasi ya kucheza katika kikosi hicho.

 

Kuhusu kambi ya Simba huko Karatu, Arusha, Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema: “Kwa upande wa kambi kila kitu kinaendelea vizuri na wachezaji wanaendelea na mazoezi ambapo kila siku wanafanya mazoezi mara mbili, asubuhi na jioni na muda mwingine itategemea mwalimu anahitaji kitu gani.

 

“Jambo la msingi ambalo tunahitaji kufanya ni kuona kwamba kuelekea Simba Day mambo yanakuwa na utofauti mkubwa. Mashabiki nao wameonyesha muitikio mkubwa kwa ajili ya tamasha lao hivyo ni suala la kusubiri na kuona wale ambao hawajapata tiketi basi wafanye jitihada kuzipata.”

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

 

 

Leave A Reply