The House of Favourite Newspapers

Grégoire Kayibanda, Rais wa kwanza wa Rwanda kuchaguliwa

0

 

Rais wa kwanza wa Rwanda, Grégoire Kayibanda.

JAPOKUWA Grégoire Kayibanda huchukuliwa kama rais wa kwanza wa Rwanda, ukweli ni kwamba alikuwa ni rais wa pili wa nchi hiyo baada ya Dominique Mbonyumutwa aliyekuwa ameishikilia nafasi hiyo kwa miezi nane tangu Januari 28, 1961 hadi Oktoba 26, 1961. Grégoire (jina hilo la Kifaransa hutamkwa ‘Gregwar’) Kayibanda kutoka kabila la Wahutu, alikuwa rais wa kwanza nchini humo kuchaguliwa kwa kura.

Aliingia madarakani Julai 1, 1962 hadi Julai 5, 1973 alipopinduliwa na jeshi chini ya Meja-Jenerali Juvénal Habyarimana ambaye naye alikuwa Mhutu. Kiongozi huyo aliyeongoza harakati za kudai uhuru kutoka kwa Ubelgiji na kuung’oa utawala wa kifalme wa Watusi na kuanzisha jamhuri. Alihakikisha Wahutu ambao ndiyo wengi nchini humo, wanashika usukani wa uongozi.

Wahutu walikuwa hawataki kuongozwa na Watusi ambao ni wachache, na waliungwa mkono na Kanisa Katoliki na Wakristo wa Kibelgiji. Kwa upande mwingine, Umoja wa Mataifa, Watusi na wakoloni wa Kibelgiji walipingana na matakwa na matarajio ya Wahutu. Katika kuhakikisha Wahutu wanafanikiwa, Kayibanda alianzisha chama cha kisiasa cha Parmehutu (Parti du Mouvement de l’Emancipation Hutu) kikimaanisha Chama cha Ukombozi wa Wahutu na akaandika ‘Ilani ya Wahutu’ (Bahutu Manifesto) mwaka 1957.

Katika kupambana na hali hiyo, Watusi nao wakaanzisha chama cha UNAR kilichojikuta kinapambana kijeshi na Parmehutu. Hata hivyo, kampeni iliyoendeshwa na Kayibanda ilishuhudia Wahutu wakichukua madaraka kwa mara ya kwanza Rwanda.

Mwaka 1961, ufalme wa Kitusi ulifutwa, Kayibanda akachaguliwa kuwa rais Oktoba 26 na akazidi kuuimarisha utawala wake. Mwaka 1965, Parmehutu kikawa chama pekee halali nchini humo na katika uchaguzi mwaka huo, Kay
ibanda alijitokea peke yake. Alichaguliwa tena mwaka 1969 akiwa mgombea pekee na ambapo wagombea wengi wa Parmehutu walipita bila upinzani.

Akiwa madarakani, Kayibanda alifuata msimamo wa mataifa ya Magharibi na mpinzani wa Ukomunist. Hata hivyo, Rwanda ilikuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Watu wa China japokuwa ilipinga sera za nchi hiyo barani Afrika.

Julai 5, 1973, waziri wa ulinzi wa Rwanda, Meja Jenerali Juvénal Habyarimana, aliiangusha serikali ya Kayibanda kwa kutumia jeshi. Japokuwa mapinduzi hayo hayakumwaga damu, watu wapatao 55, wengi wao maofi sa serikalini, wanasheria na wafanyabiashara waliokuwa karibu na utawala wa Kayibanda,wanasemekana waliuawa. Pia ilidaiwa familia za watu hao zilipewa fedha ili zikae kimya. Serikali hiyo mpya pia ilimkamata Kayibanda na mkewe na kuwapeleka sehemu ya siri – inasemekana katika nyumba moja karibu na Kabyagi — ambako walikufa kwa kunyimwa chakula. Inafaa pia kukumbuka kwamba tangu utawala wa kwanza wa Dominique Mbonyumutwa, viongozi wengine wote Rwanda walikuwa ni Wahutu; ni Paul Kageme tu, rais wa sasa, ndiye Mtusi! Huyo ndiye Grégoire Kayibanda aliyeingia madarakani Rwanda akiwa na umri wa miaka 38 tu akiwa alizaliwa Mei 1, 1924 na kufariki Desemba 15, 1976 akiwa na umri wa miaka 52.

Nakujuza zaidi Mwandishi: Walusanga Ndaki na Mitandao +255 715 439853

Live: Gwajima Aliamsha Dude Kushambuliwa Kwa Tundu Lissu

Leave A Reply