The House of Favourite Newspapers

Hadithi Mpya ya Eric Shigongo – I miss My God! (Namkumbuka Mungu Wangu)

 

I miss My God! (Namkumbuka Mungu Wangu)

Mtunzi: Eric Shigongo;

“Oh My God! It is a ruptured pregnancy!”(Mungu wangu! Kumbe mfuko wa uzazi umepasuka!) aliongea kwa sauti Dk. Namshitu Fundikira, bingwa wa upasuaji wa matatizo ya wanawake .
“Kweli?” Daktari mwingine aliyekuwa karibu aliuliza.
“Kabisa, tunachohitaji kufanya hivi sasa ni kumkimbiza haraka sana chumba cha upasuaji ili tujaribu kuokoa maisha ya mama na mtoto, tukizidi kuchelewa tutapoteza wote wawili au mmoja wao.”
Yalikuwa ni maongezi ya kundi la madaktari ndani ya chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Good Samaritan iliyopo eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, mwanamke alikuwa amelala kitandani, ujauzito wake ukionekana bayana, mtu mwenye akili timamu hakuhitaji shahada yoyote kuelewa ukali wa maumivu aliyokuwa nayo, jasho jingi lilikuwa likimtoka na kulowanisha mashuka huku akitupa miguu yake huku na kule.
“Sasa sijui ni kwa nini alichelewa hivi kuja hospitali, uchungu umechukua muda mrefu kuliko kawaida!” Muuguzi aliongea huku akisogea kwenye meza iliyokuwa kando ili apate kupiga simu chumba cha upasuaji kuwataka wafanye maandalizi.
“Ana CPD!” Dk. Fundikira alitamka maneno hayo akimaanisha Cephalo-Pelvic-Disproportion, yaani hapakuwa na uwiano kati ya kichwa cha mtoto na nyonga ya mama, pengine mtoto alikuwa mkubwa na nyonga ndogo hivyo alikuwa ameshindwa kutoka nje kwa njia ya kawaida, akapasua mfuko wa uzazi.
Maisha ya mama yalikuwa katika hatari, hapakuwa na muda wa kupoteza kama kweli nia ya kuokoa maisha ilikuwepo. Madaktari walikimbia haraka chumba cha upasuaji kumsubiri mgonjwa, ambaye dakika kumi tu baadaye aliingizwa, timu yote ya watu wasiopungua kumi ikaingia kazini.
“Unaitwa nani?” Dk. Pascal Rwezaura, bingwa wa dawa za usingizi alimuuliza mgonjwa wakati akimchoma sindano kwenye mshipa.
“ Jackline!”
“Jackline nani?”
“Manyilizu.”
“Mume wako yuko wapi?”
“Sina mu…” hakuweza kujibu swali hilo hadi mwisho, akaingia usingizini na upasuaji ukaanza dakika tano baadaye kila kitu kilipokuwa tayari, Dk. Fundikira, binti wa miaka ishirini na sita, mwenye elimu ya kutosha juu ya upasuaji aliongoza jopo la madaktari kuokoa maisha ya mgonjwa na mtoto.
Upasuaji ulifanyika kwa saa nne, ndipo taarifa zikapatikana kuwa mama na mtoto wake wote walikuwa wamenusurika kifo, ingawa mfuko wa uzazi uliondolewa, hiyo ilimaanisha mwanamke huyo asingepata mtoto tena maishani, huyo ndiye alikuwa wa kwanza na wa mwisho, wote wawili wakarejeshwa wodini.
“Hongera sana daktari!” muuguzi alimwambia Dk. Fundikira.
“Nakushukuru sana Diana, muujiza umetokea, mtoto ni mzima kabisa wala hajaumia sehemu yoyote, nilikuwa na wasiwasi kwamba ubongo wake kuwa umeathirika lakini la! Ana afya njema mno, nasikitika tumelazimika kuuondoa mfuko wa uzazi kwani umepasuka vibaya mno!”
“Kwani kulitokea nini?”
“Ninahisi huko alikotokea, walimchoma sindano ya Oxytocin, kwa lengo la kumwongezea uchungu bila kufahamu kuwa mtoto alikuwa ameshindwa kupita kwenye nyonga ndogo, mfuko ukapasuka!”
“Uzembe wa hali ya juu!”
“Sana!”
***
Saa sita baadaye Jackline Manyilizu akiwa wodini alizinduka usingizini, mtoto alikuwa kando yake, machozi ya furaha yakamtoka. Alionekana haamini alichokuwa akikishuhudia kwa macho yake, kwamba ni yeye aliyekuwa amezaa mtoto mzuri kiasi hicho.
Mtoto alikuwa mchanganyiko wa Mwafrika na Mzungu, kwa kasi taswira za baba wa mtoto zikamwijia akilini na maonyo yote aliyopewa kwamba kamwe asifungue mdomo wake kusema chochote, akambusu mwanaye kwenye paji la uso, kisha kuonyesha ishara ya msalaba kifuani kwake kama ishara ya shukurani.
“Nitamwita mwanangu Theresia!” aliongea akijifuta machozi.
***
Nyumba ya Jackline Manyilizu ilikuwa jirani kabisa na Parokia ya Mwenge ya Kanisa la Redemption Church Of God, ambalo watu wengi waliufananisha mfumo wake wa utendaji kama Kanisa Katoliki, tangu kuanzishwa kwake na watu waliojitenga na Kanisa Katoliki miaka ya sitini dhehebu hilo lilikuwa limekua na kujipatia wafuasi wengi sana nchini Tanzania.
Lilikuwa na Askofu mkuu, mapadri, watawa, makatekista kama tu ilivyokuwa kwa Kanisa Katoliki, tofauti pekee ambayo dhehebu hili lilikuwa nayo na Kanisa Katolini ni namna ya kuendesha ibada, ndani ya Redemption Church ibada iliendeshwa Kilokole zaidi, watu wakiimba mapambio na kurukaruka wakimsifu Mungu jambo ambalo ndani ya Kanisa Katoliki halikufanyika.
Kwa sababu ya umasikini mkubwa, Jackline, alikuwa mwanamke mrembo lakini mchafu na aliajiriwa na Parokia hiyo kama mfagizi na mpishi wa mapadri, kazi aliyoifanya kwa miaka mingi kwa uaminifu mkubwa, akapumzika tu alipopatwa na ujauzito.
Aliporuhusiwa kutoka hospitali alirejea kwenye kibanda chake kidogo akiwa na mtoto wake, wafanyakazi wenzake ndiyo walimsaidia kumtunza mpaka alipopata nguvu za kujisimamia mwenyewe, hakutaka watu wengi sana wafike nyumbani kumwona mtoto wake, rangi ya Theresia ingeweza kuzua maswali mengi ambayo hakuwa tayari kuyajibu.
Miezi mitatu baadaye akiwa amemleta mtoto wa shangazi yake kutoka kijijini kwao Msowelo, wilayani Kilosa, aliamua kurejea kazini, wiki moja tu baadaye Padri Antonio Slivanio, alirejeshwa na shirika lake nchini kwao Ufaransa, sababu haikueleweka na wengi lakini Jackline alielewa kilichokuwa kikiendelea.
“Never open ya maut’ and say anyting’” Maneno hayo ya Padri Antonio yaliendelea kuzunguka kichwani mwake.
Theresia alikuwa mtoto mrembo mno, mchanganyiko wake wa mama Mtanzania na baba Mzungu ulitia ganzi akili za watu wengi kila walipomwona, haikuwa rahisi hata kidogo kuamini mtoto huyo alikuwa wa Jackline, mwanamke mfagizi parokiani ambaye alishakula kiapo cha kutomtaja baba wa mtoto wake.
Kwenye umri wa miaka miwili na nusu, Theresia alilazimika kupelekwa shule ya awali iliyokuwepo hapo hapo parokiani, haikuwezekana tena kuendelea kumficha mtoto ndani, jina aliloanzishwa nalo shule ni la Theresia Manyilizu, wengi walijiuliza maswali mengi bila kupata majibu juu ya baba wa mtoto.
“She is very cute”(Ni mtoto mrembo)
“Oh my God look at her eyes”(Mungu wangu, angalia macho yake)
“Don’t forget the legs”(Usisahau miguu)
Aina hii ya mazungumzo ndiyo yaliyotokea kila watu walipomwona mtoto huyo, hakika alikuwa mrembo, haikuwa rahisi kupita bila kusema chochote na hakuna aliyedhani mtoto huyo angeweza kuwa wa Jackline, mfagizi wa parokiani! Wengi walishindwa kuelewa nini kingetokea mbele ya safari maishani, Theresia akitimiza umri wa miaka kumi na nane.
“Magari yatagongana nyumbani kwao, kweli Tanzania tumebarikiwa kuwa na wanawake warembo lakini sijawahi kuona mtoto mzuri kama huyu, ona pua yake utafikiri Mtusi, shingo utadhani Muethiopia, midomo utafikiri Msudani, masikio utafikiri Msomali, kidevu utafikiri Msukuma! Huyu mtoto mrembo wacha mchezo bwana!” dereva mmoja wa parokia alisikika akititirika maneno bila kituo huku wenzake wakimsikiliza.
Theresia aliendelea kukua kwa kimo na akili bila yeye kutambua urembo aliokuwa nao, watu wengi aliwasikia kwa masikio yake wakimsifia lakini hakuelewa, swali lililomsumbua kichwani mwake lilikuwa ni moja tu; nani alikuwa baba mzazi? Ambalo hata siku moja mama yake hakuwahi kulijibu.

Hii ni simulizi yangu mpya katika Gazeti la Spoti Xtra ambalo litaanza kutoka kesho. Nina uhakika ukiisoma simulizi hii, hutojuta. Ni simulizi yenye mafunzo mengi mno.

Comments are closed.