The House of Favourite Newspapers

HATA KAMA UPO NAEYE KWENYE NDOA, UNAPASWA KUMPA UHURU WAKE

HATA Jinsi tulivyoumbwa, kila mmoja anapenda sana kuwa na ule uhuru wake wa faragha au kwa Kingereza wanaita privacy. Huu ni muda ambao mtu anakuwa peke yake na kufanya mambo yake peke yake bila kuingiliwa na mtu yeyote. 

 

Watu wengi wanashindwa kulielewa hili, wanaamini kwamba mkishaingia kwenye ndoa, basi hakuna mwenye uhuru wa kumficha mwenzake chochote. Ni kweli kwamba mkishakuwa mwili mmoja, mnatakiwa kushirikishana kwa kila kitu, lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba ‘privacy’ ni haki ya kila binadamu.

 

Haina maana kwamba mwenzi wako anapohitaji kuwa na muda wa kufanya mambo yake peke yake, basi kuna jambo baya anataka kulifanya, hapana. Wakati mwingine unahitaji muda wa kuwa peke yako, kujitafakari wewe ni nani, umetoka wapi na unakwenda wapi.

Ipo hivi, mnapokuwa kwenye uhusiano wa kudumu, iwe ni ndoa au uchumba, unatakiwa kuelewa kwamba mwenzi wako ni binadamu huru, anao uhuru wake na anatakiwa kuutumia pale anapohitaji. Haina maana kwamba kwa sababu umemuoa, basi tayari amekuwa mtumwa kwako, haina maana kwa sababu amekuoa, basi muda wote anatakiwa kuwa pamoja na wewe.

 

Uhuru ninaouzungumzia hapa, ni kwa mfano; mwenzi wako anaweza kutamani kutoka ‘out’ peke yake au na marafiki zake bila uwepo wako. Anaweza kutamani kushinda nyumbani tu akiwa amejifungia chumbani peke yake, akitafakari maisha yake au anaweza kutamani kusafiri kwenda kwenye mazingira tofauti akiwa peke yake.

 

Anaweza pia kutamani kuwa na vitu vyake ambavyo hakuna mtu anayevigusa, kwa mfano anaweza kuwa na begi lake ambalo anahifadhi vitu vyake tu na hataki uwe unalipekuapekua na kadhalika. Achana na hilo, kuna wakati pia anaweza kuwa hapendi ushikeshike simu yake na kuipekua bila sababu za msingi, hakuna chochote kibaya lakini anataka awe huru!

Hapa watu wengi sana huwa wanashindwa kulielewa hili na mwisho wanaishia kwenye matatizo makubwa, mmoja akimshuku mwenzake kwamba pengine ana mambo maovu anayoyaficha. Kama na wewe ni miongoni mwa watu wa aina hii, unapaswa kubadilika. Wakati mwingine siyo lazima akuombe ruhusa, unaweza kumfanyia sapraiz kwa kumpa kwa mfano fedha kisha ukamwambia nataka leo utoke out na marafiki zako, utakuwa umeugusa moyo wake kwa namna ya kipekee mno.

 

Kama huwa unapenda sana kukaguakagua simu yake, hebu muoneshe tofauti kidogo, acha kushikashika simu yake, hata akiiacha na ukiona inaita, achana nayo! Ukiweza kufanya hivi, utamfanya ajisikie amani kubwa ndani ya moyo wake na hisia za mapenzi zitazidi kuongezeka juu yako.

 

Acha kuwa unampekuapekua vitu vyake, mpe uhuru wa kufanya mambo yake peke yake bila kumuingilia, utamsaidia sana kumjengea nguvu kubwa ya kujiamini na akishajiamini atakuamini na wewe na mapenzi yatazidi kunoga.

 

Na wewe unayepewa huu uhuru, muoneshe mwenzi wako kwamba hajakosea kukupa uhuru wako, utumie vizuri. Kama kweli amekuruhusu utoke out na rafiki zako mkafurahi pamoja, isiwe tena ndiyo nafasi yako ya kwenda kufanya mambo ya hovyo, isiwe ndiyo ‘fungulia mbwa’, utakuwa unakosea. Jiheshimu na mpe sababu ya kukuamini! Hakuna mapenzi kama hakuna kuaminiana na uaminifu huwa hauji tu, bali unajengwa.

Comments are closed.