The House of Favourite Newspapers

Hatimaye Godbless Lema Awasili Tanzania, Akabidhiwa Biblia na Wazee wa Chadema – Video ya Mapokezi Ipo Hapa

0

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini na aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, leo Jumatano Machi 1, 2023 amewasili nchini akitokea Canada, alikokuwa akiishi tangu 2020 baada ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka huo.

Lema amewasili Tanzania mchana wa leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambapo anatarajiwa kusafiri hadi jijini Arusha, kwa ajili ya kushiriki mkutano wa hadhara wa Chadema.

Mwanasiasa huyo machachari nchini, amepokewa na umati wa watu waliofika uwanjani hapo, ambao walikuwa wamevaa sare za Chadema.

Baada ya kuwasili uwanjani hapo baadhi ya wazee ambao ni wafuasi wa Chadema, walimkabidhi biblia ya lugha ya kimachame, kama ishara ya kumpokea.

Mwakilishi wa wazee hao alimkabidhi biblia hiyo, huku akimkaribisha nyumbani baada ya kuishi ughaibuni nchini Canada kwa miaka zaidi ya miwili.

Lema ni miongoni mwa wanasiasa wa Tanzania waliokimbia nchi baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2020, kwa madai ya kupokea vitisho vya kiusalama. Viongozi wengine waliokimbia nchi kwa madai hayo walikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu na Ezekiel Wenje na wote wamerejea Tanzania.

Mamia ya wafuasi wa Chadema jijini Arusha na mkoani Kilimanjaro, wamejitokeza kwa wingi kumpokea Godbless Lema.

Leave A Reply