The House of Favourite Newspapers

Hausigeli akutwa na maiti ya Kichanga cha Siku 2

0

Makongoro Oging’ na Issa Mnally, UWAZI

DAR ES SALAAM: Hii kali! Mfanyakazi wa ndani ‘hausigeli’ Hadija Yusuf (23), mkazi wa Makumbusho anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Kawe jijini Dar kufuatia kukutwa na maiti ya kitoto kichanga cha siku mbili.

Taarifa kutoka vyanzo makini zinadai kuwa Hadija alitiwa mbaroni Desemba 22, mwaka huu baada ya polisi kumkagua na kumkuta na maiti hiyo akiwa ameifunga na khanga kiunoni kisha kuvaa gauni (dela) ili asijulikane.

Inadaiwa kuwa dada huyo alikuwa akifanya kazi kwa mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la Hawa maeneo ya Kawe na tangu afike hapo alishamaliza miezi miwili.
Siku ya tukio, Hadija alijifungia chumbani kwa muda mrefu, hali iliyomfanya mwajiri wake kuwa na hofu na kumgongea mlango.

“Alipomuuliza kama ana tatizo, alisema anajisikia vibaya na alipoambiwa apelekwe hospitali alikataa, kitendo kilichomfanya bosi wake huyo kuzidi kuwa na wasiwasi.
“Kutokana na hali hiyo, bosi huyo aliamua kumpeleka kwa ndugu yake mmoja lakini kabla ya safari kuanza, alimtilia shaka na kumchukua hadi kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano,” kilisema chanzo.

Ilizidi kudaiwa kuwa polisi wakati wanamhoji, pia walimtilia shaka na kuamua kumkagua ndipo walipokuta maiti ya kichanga ikiwa imefungwa kwa kanga kiunoni.
Alipohojiwa, alisema maiti hiyo ni ya mtoto wake aliyejifungua kwa bahati mbaya na kufariki dunia.

“Hata mwajiri wake hakujua kama Hadija ni mjamzito kwa kipindi chote alichofanya kazi kwake. Alishangaa kumwona msichana wake amekutwa na maiti ya kichanga kinachodaiwa alijifungua kwa siri,” kilisema chanzo kingine cha habari.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa polisi walimwandikia fomu maalum ya matibabu (PF3) kisha kumpeleka Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu kisha kurudishwa Kituo cha Polisi Kawe ambapo anaendelea kushikiliwa. Maiti ya mtoto huyo ipo Muhimbili kwa uchunguzi kama alizaliwa na kunyongwa au alifariki dunia mwenyewe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Camillus Wambura alikiri kupokea taarifa hiyo na kusema Hadija anashikiliwa katika kituo cha Kawe wakati uchunguzi ukiendelea.

Leave A Reply