The House of Favourite Newspapers

Hawana Jipya Lakini Wanawika

0

TUMEKUWA tukiona wasanii wakiwa maarufu kwa kazi wanazofanya huku wengine wakiupata umaarufu huo kwa skendo au kutokana tu na muonekano na mavazi wanayotupia.

 

Katika makala haya leo tunakuletea mastaa ambao ni habari ya mjini; yaani wanazungumziwa na jamii inayowazunguka, lakini kwa muda mrefu hawajaonekana na kazi mpya.

 

IRENE UWOYA

Ni msanii wa filamu za Kibongo. Licha ya kwamba hajaonekana kwenye filamu muda mrefu, lakini bado jina lake halijapotea kwenye akili za watu.

 

Uwoya kwa sasa hajulikani anafanya kazi ya biashara ya baa, lakini amekuwa akionekana kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram akijiachia kwa mavazi tofauti na kusababisha watu kusema kuwa huenda amegeukia kazi ya kutangaza nguo.

 

KAJALA MASANJA

Ni muda mrefu sasa Kajala hajaonekana na kazi au kwenye filamu mpya, lakini bado maisha yake yako vilevile, anakiki ileile.

 

Kwa sasa Kajala anaonekana zaidi kwenye kipindi cha runinga hivyo huenda kazi hiyo ndiyo inayomuingizia kipato cha kumwendeshea maisha.

 

WEMA SEPETU

Mwanadada huyu ambaye ni Miss Tanzania 2006, alipata umaarufu mkubwa baada ya kuingia kwenye ulimwengu wa sanaa ya filamu za kibongo.

 

Ni muda mrefu sana Wema hajaonekana kwenye filamu, lakini bado umaarufu wake upo palepale.

Wema kwa sasa anazungumziwa zaidi kwenye suala la mwili wake kwani amepungua kupindukia na kupoteza kabisa muonekano wake ule wa zamani wa utipwatipwa na umbo la kuvutia.

 

OMMY DIMPOZ

Mwanamuziki huyu wa Bongo Fleva ambaye jina lake halisi ni Omary Nyembo ameingia kwenye orodha hii baada ya kukaa muda mrefu sana bila kutoa ngoma mpya, lakini bado jina lake lipo midomoni mwa watu.

 

Baada ya kukaa muda mrefu sana, Januari mwaka huu ndiyo alitoa ngoma akishirikiana na msanii mwenzake, Faustina Charles ‘Nandy’ inayokwenda kwa jina la Kata.

 

SHAMSA FORD

Ni msanii wa filamu. Siku kadha wa kadha zimepita bila kuonekana kwenye filamu mpya jambo ambalo linatafsiriwa huenda baada ya soko la filamu kukataa, wengi waliamua kuipa mgongo.

Shamsa ameendelea kuwa maarufu sana hasa mitandaoni kutokana na biashara ya madira anayofanya hivyo yanaonekana kumweka juu.

 

ZUWENA MOHAMMED ‘SHILOLE’

Kwa upande wa filamu ambazo ndizo zilizomtambulisha kwenye ulimwengu wa mastaa Shilole ni miaka mingi hajaonekana na akiulizwa anasema bado yupo.

 

Kwa upande wa muziki mara ya mwisho alitoa wimbo mpya wa Nikagongee Remix mwisho mwa mwaka jana na mpaka sasa hajatoa kazi mpya.

 

JACQUELINE WOLPER

Msanii huyu wa filamu ni muda mrefu sana hajaonekana na kazi mpya lakini bado jina lake linatajwatajwa sana na mashabiki yaani umaarufu wake haujapotea bado.

Wolper anawika zaidi kwenye biashara zake za nguo ambapo anatangaza zaidi kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram.

 

ELIZABETH MICHAEL ‘LULU’

Haikumbukwi ni lini alionekana kwenye filamu mpya licha ya kwamba umaarufu wake umetokana na sanaa hiyo.

Tangu apitie kwenye changamoto ya kifungo jela na kile cha nje kwa kumuua Steven Kanumba bila kukusudia mpaka leo hajawahi kuonekana kwenye filamu mpya zaidi anaonekana Instagram na jina lake bado ni maarufu.

 

Makala: Gladness Mallya

Leave A Reply