The House of Favourite Newspapers

Haya Ndiyo Niliyoyaona Baharini-7

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
Tuliondoka na giza bado kuelekea Papua. Meli ilikuwa ikakata maji huku ikionekana kuwa nzito sana kiasi kwamba nilijaribu kumuuliza Nurdin kama hali ile ilitokana na mzigo mkubwa au nini, akasema si mzigo na meli ziko makini, haziwezi kuzidisha mzigo bali zinaweza kupwelea huo mzigo.
ENDELEA NAYO MWENYEWE…

Akasema: “Hapa tunapita kwenye maji mazito ya bahari. Maji haya unaweza kutupa kitu kama kipande cha sabuni kisizame kwa sababu yana aina fulani ya chumvi tofauti na maji ya Bahari ya Hindi kule kwetu.”
Ghafla nahodha alipiga simu kwenye chumba cha mipango na kututaka wote tujue kuwa, tunaingia kwenye pori la baharini.

Hapo napo nikafungua akili ili kujua zaidi. Lakini Nurdin kama sijamuuliza pori la baharini ni nini, akaniambia kwa sauti ya chini:
“Hapo sasa, hatutakiwi kusema kwa sauti. Hata nahodha hatakiwi kupiga honi eneo hili, ni pori la bahari. Inadaiwa kuwa ni maeneo ambayo majini hukutana kushitakiana na kupeana adhabu mbalimbali.”
Nilibaki nikitetemeka lakini sikumuuliza kitu Nurdin kwani aliniwahi kwa kuniambia kwamba, kama nina maswali kuhusu maelezo yake hayo, tusubiri tuvuke pori la bahari. Nilimkubalia kwa kutingisha kichwa kwamba nimemwelewa.
Tulitumia dakika kumi kuvuka eneo hilo na jambo moja ambalo ni la kushangaza sana ni kwamba, wakati tunapita pori la bahari, tulifunikwa na giza totoro japokuwa ilikuwa kweupe na jua likiwaka.
Wakati tunaingia, mimi nilishtukia tuko gizani, baadhi ya taa kwenye meli zikawashwa ili kusaidia mwanga, hasa taa za nje.

Na tulipolipita pori la bahari, tulitokea kwenye mwanga wa ghafla huku jua likionekana. Nilishindwa kujua pale kwenye giza, juu, kulia, kushoto, nyuma na mbele tulikuwa tumefunikwa na kitu gani mpaka kukawa giza. Nilijikuta nimezama kwenye mawazo na ghafla Nurdin akasema:
“Bwana Tolu najua hapo una mambo kibao kichwani unataka kuniuliza, uliza tu ndugu yangu.”
Swali la kwanza nilitaka kujua ile sehemu ambayo majini wanashitakiana na kupeana adhabu mbalimbali ni adhabu gani na wanashitakiana kuhusu nini!
“Wanashitakiana kuhusu wale wanaokaidi maagizo. Unajua majini hawafi?” aliniuliza Nurdin kabla hajaendelea mbele.
“Nimekuwa nikisikia hivyo,” nilimjibu.

“Hawafi ndiyo. Sasa kuna majini hutumwa duniani kwa kazi mbalimbali. Sasa wanapofika huku, baadhi yao huacha yale waliyotumwa na kuishi duniani. Wengine hutokea kuwapenda wanawake wa duniani, wengine hutokea kuwapenda wanaume wa duniani.

“Sasa kama waliambiwa waje duniani kuchukua damu, pengine kwa watu f’lani halafu wao walipofika kwa hao watu, wakajikuta wanawapenda sana na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi.
“Kama ni mwanamke ndiyo jini, akampenda mwanaume binadamu, anapobeba mimba hurudi ujinini ndipo anapokutana na mashitaka yake ya kukaidi agizo la wakubwa wake kwamba akachukue damu.

“Katika hili bwana Tolu, wewe hujaoa, ogopa sana kumpata mwanamke kwenye baa, kumbi za muziki au barabarani mkapendana lakini ikatokea hata siku moja hakupeleki kwa ndugu yake yeyote yule, wengi wanakuwa majini, sasa watakupeleka wapi!”
Baada ya maelezo hayo ya Nurdin ambayo kwangu yalikuwa mazito sana, niliguna kwanza. Akasema:
“Najua unajua mengi ya baharini bwana Tolu, lakini mimi nasema bado hujui wewe kama inavyotakiwa kujua.”
“Nurdin, umesema kuna majini wanakuja duniani wanaishi?”
“Ndiyo. Na wanafanya kazi za kibinadamu ili kupata pesa. Inaonekana wao hufurahia maisha yetu sisi binadamu.”
“Kumbe baharini kuna mambo mengi sana Nurdin.”
“Sawa. Kuna wakati fulani meli hupiga nanga bandarini halafu inashusha majini lakini hakuna mtu anayejua. Watu wa bandarini wanajua ni meli ya kawaida na wanaoshuka ni abiria wa kawaida, kumbe majini wamekuja kuutembelea mji wenu,” Nurdin aliniongeza kitu kingine tena, nikashangaa na kumuuliza:
“Ina maana hata bandari ya Dar es Salaam inaweza kutokea?”
“Kwa nini ishindikane bwana Tolu. Kwanza labda nikwambie kitu, hizi fukwe ambazo watu hupenda kwenda na kupata upepo mwanana, ogopa sana. Unaweza kukaa kwenye kiti pembeni ya fukwe na kuangalia baharini, ukashangaa kuwaona watu wanaogelea muda mrefu majini lakini hawaji nchi kavu na wala huwaoni wanapoingia au waliochoka wanapotoka majini.”
“Ina maana pale wale wanakuaga ni majini?” nilimuuliza Nurdin ili kutaka kujua mambo ya ajabu yanayoendelea kujiri baharini.

“Wengi wao bwana Tolu wanakuwa ni majini na wanachanganyana na wanadamu. Ndiyo maana unaweza kukuta mtu anaogelea kila siku majini, lakini siku moja anatoweka katika mazingira ya kutatanisha, unadhani ni nini kama siyo kuchukuliwa na majini kwenda nao kwao,” alisema Nurdin, nikakumbuka swali moja la adhabu mbalimbali wanazopewa majini mara baada ya kushitakiana.
“Na vipi kuhusu adhabu Nurdin? Maana siamini kama majini wanaweza kushitakiana.”
Je ni jambo gani hilo? Usikose kusoma mkasa huu kwenye Gazeti la Ijumaa kesho.

Leave A Reply