The House of Favourite Newspapers

Pesa za mtaji unamtunza rafiki, ndugu asikuchoke kwa nini?

0

Asalam alaikum wapenzi wasomaji wangu, bila shaka Sikukuu ya Pasaka imeisha salama sasa tuendelee na majukumu yetu ya kulijenga taifa, kwa wagonjwa nawapa pole Mungu awape nguvu tuungane tena, waliofiwa nawaombea subra Ishallah.
Leo nimekuja na mada hii ya wanawake kupenda shughuli kila wiki na kujikuta wakimaliza mtaji wa biashara kwa kuwatuza marafiki au ndugu.

Hivi mwanamke unawezaje kuwa mtu wa shughuli kila kukicha wakati unamte-gemea mume? Yaani kwa kifupi unategemea mtaji kutoka kwa mume, unadhani atakupatia fedha zilezile? Wengi wetu tukishashika mtaji tu tunajisahau na kuona kuwa tumepata hela za kutungua nguo dukani mara za kuwa-onesha watu kuwa unajiweza kwa njia ya kutuza kwa hilo kiukweli tunakosea sana.

Hapa kuna msomaji mmoja kanitumia ujumbe ambao umenisukuma kuandika haya unayoyasoma;
“Mama nimeamua kuachana na mke wangu kwa sababu nilisafiri kwenda nje ya nchi nikamuachia mradi auendeleze lakini cha kushangaza niliporudi nimekuta umekufa na mtaji hakuna tena nilipombana sana hakujibu kitu matokeo yake ndani kumejaa madera mbalimbali ya shughuli na nilipojaribu kuchunguza nikaambiwa kuwa yeye ndiyo mwenyekiti wa kundi la kutuzana pale kunapokuwa na shughuli ya mtu fulani, kiukweli nilishangaa na nilipochunguza zaidi niliambiwa kuwa hakuna shughuli aliyowahi kukosa na kila shughuli inahitaji sare,” alisema msomaji.

Msomaji huyo alieleza kuwa ameamua kusema hapa ili liwe funzo kwa akina mama wengine kwani makundi ya namna hiyo huwasababishia kumaliza pesa kwenye akaunti zao na hata za waume zao ambapo alidai kuwa anamshangaa mkewe hana shughuli aliyowahi kufanya kwake na mbaya zaidi ana watoto wadogo lakini shughuli za wenzake ndiyo zimekomba mtaji wa biashara yao.

Si huyo tu wapo wengi kwani yupo mwingine aliyenilalamikia kumuacha mkewe kwa sababu ya mambo hayohayo ya kumaliza pesa kwa kutuza, huyu alieleza alivyoshtuka kukuta akaunti yake imebaki na fedha kidogo baada ya kumueleza mkewe namba yake ya siri ya akaunti.

Akina mama wenzangu hili ni tatizo kubwa, mwanamke anatakiwa kuwa meneja wa mume ambaye atampangia vizuri matumizi ya pesa anayoipata lakini nyie ndiyo mmekuwa mstari wa mbele kumaliza pesa za waume zenu, mnakosea.
Kumbuka kuwa mtaji na biashara zote ni kwa faida ya familia si kwa faida yenu tu pia kuna baadaye, huenda leo una pesa nyingi kwa sababu mume anafanya kazi benki jiulize je, akiachishwa ghafla itakuwaje?
Wapo akina mama wanaolilia mitaji, wasipopewa wanalaumu na kuwasema vibaya waume zao lakini wapo ambao wakipewa wanamfanya mume kuwa buzi hili ni suala baya ambalo mimi kama mwanamke siwezi kulifumbia macho.

Mwanamke ukiwa wa kupenda shughuli utajikuta una kasoro kwenye kulea familia yako, angalia shughuli ina uzito kiasi gani kwako na je unaowapa watakufaidisha na nini baadaye lakini kikubwa usithubutu kutoa pesa ya mtaji wa biashara kwa ajili ya shughuli, hili litakusumbua.

Bila shaka mmenielewa tukutane siku nyingine kwa mada kali zaidi.

Leave A Reply