The House of Favourite Newspapers

Haya Ndiyo Niliyoyaona Baharini-9

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
“Bwana Tolu usifanye kitu chochote kile. Usipunge mikono juu wala usishuke kwenda chini. Wewe waangalie tu. Basi, niliwaangalia kweli kwani wenzangu wote walitulia wakiwaangalia tu. Waliendelea kutupungia mikono kama vile watu wanavyofanya pale kiongozi fulani anavyotembea eneo akiwa ndani ya gari.
SASA ENDELEA MWENYEWE…

Tulipomaliza kwa kulipita eneo lile, nilimuuliza Nurdin kisa cha wale wanawake tena wazuri kabisa.
“Bwana Tolu mambo ni yaleyale. Wale wanawake wote ni majini tu. Kwa wanaofanya kazi baharini kuona majini wanawake au wanaume ni jambo la kawaida sana na siyo tishio kwao.
“Kuna siku tutakuja kupita kwenye bahari ambayo hutaamini yatakayotokea. Majini hawa wanaingia mpaka ndani ya meli na kukaa huku juu. Wanakuwa marafiki kabisa na sisi lakini tatizo lao wakija kwa mtindo huo huwa hawasemi au niseme hawatoi sauti zaidi ya kuachia matabasamu muda wote.”
Basi, meli iliendelea kukata maji. Ukimya ulitawala kwani kuchoka pia kulichangia. Ndani ya saa mbili tulifika eneo moja ambalo kwa mbele tuliona kisiwa. Nilimuuliza Nurdin kama na yeye ameona kisiwa kile!
“Kile ni kisiwa kinachotembea. Kwa mfano hapa kipo mbele yetu, siku nyingine tutakikuta kushoto, wakati mwingine kulia,” alisema Nurdin.
“Tutakigonga?”
“Hapana, kitatukwepa chenyewe.”
“Ina maana kinajua kwamba kuna meli inakuja?”
“Hilo ndilo linalotushangaza sana sisi. Kwa nini kile kisiwa kinahamahama wakati tunajua hakina miguu.”
“Kuna watu wanaishi?” nilimuuliza Nurdin.
“Hapana, hakuna hata mnyama. Sisi habari za kile kisiwa tuliambiwa na wenyeji wa Sumatra. Ndiyo tukajua duniani kuna maajabu.
Wakati Nurdin anayasema hayo, meli yetu ilikuwa imekaribia sana kile kisiwa nacho kikawa kinasogea mbele sasa. Yaani meli ikawa haikifikii. Tukawa tunakwenda nacho sambamba.
Ilifika mahali kikaanza kuelekea kulia kwetu, nikaweza kukiona vizuri. Ni kisiwa chenye ukubwa wa kuweza kujengwa nyumba kama kumi na tano hivi.

Kilikuwa na majani tu, tena madogomadogo kama vile yanafyekwa na mtunza bustani mahiri. Ni kweli ndani ya kisiwa hicho sikuona binadamu wala kiumbe. Kilipokwenda kulia kwetu, kikaanza kurudi nyuma polepole mpaka tukakiacha.
Nilibaini kweli watu wanaofanya kazi ya ubaharia wanaona mambo mengi ya ajabu kwani wakati mimi nimeshikwa na mshangao, wenzangu walikuwa wakiendelea na mambo yao mengine.

“Bwana Tolu inaonekana kwako una mshangao mkubwa sana?” Nurdin aliniambia.
“Sanasana.”
Haikupita hata nusu saa tangu kisiwa kitutokee mbele yetu na kurudi nyuma, tukakutana na maajabu mengine. Tuliona baharini shamba la pamba. Pamba kabisa pamba. Lilikuwa lina ukubwa wa kama uwanja wa mpira.
Lile lilikuwa ajabu kubwa kwani hata wenzangu niliwaona wanasimama na kuanza kuliangalia lile shamba.
“Si pamba zile?” alisema mfanyakazi mwenzangu mmoja anaitwa Martin lakini tulizoea kumwita ‘Wa Ubani’. Ni Mkenya.
Naamini hata nahodha wa meli yetu alishangazwa na lile shamba, kwa vyovyote vile. Mimi nilitumbulia macho. Pamba ilikuwa imekomaa. Kwa hiyo kwa mbali, shamba lilionekana jeupe sana. Lakini ndani ya shamba lile hakukuwa na watu wala shughuli iliyokuwa ikiendelea.

Kwa sisi kwenye meli, shamba lile lilikuwa upande wa kushoto kwetu. Tulikuwa kimya wote tukiangalia tukio lile linavyoendelea na maajabu yake Mungu ya hapa duniani. Tulilipita lile shamba mpaka tukaliacha.
Wakati tunakaa, Nurdin aliniangalia na kuachia tabasamu lake. Akanisogelea na kuniambia kwa sikioni.
“Usiogope bwana Tolu.”
“Siogopi, maana hata nyie nawaona hamuogopi,” nilimjibu. Akacheka.
Baada ya hapo, safari ilikuwa salama mpaka tukafika Papua New Guinea. Hii nchi imepakana na nchi nyingine inaitwa East Timor au Timor ya Mashariki.

Pale kazi ya kupakiza mizigo ilikesha usiku kucha lakini siyo sisi, kuna watu tuliwakuta, wakaifanya kazi hiyo mpaka mzigo wote ukaingia ndani ya meli na meli ikawa imebeba mzigo unaotakiwa kwa mujibu wa uzito wake sasa.
Tulilala pale Papua, kesho yake asubuhi kabla ya kuondoka, nahodha wetu alisema anatupa masaa matatu kwenda mjini ili kama kuna kitu cha kununua tufanye hivyo kisha turudi na kuanza safari.
Nurdin aliniambia raha ya kutembelea nchi mbalimbali kwa kazi ya ubaharia ni hiyo. Kwani unaweza kununua kitu ambacho nchini mwako hakuna mtu hata mmoja aliyenacho kwa hiyo ukaonekana ni pekee.
Tulikwenda mjini. Mimi niliongozana na Nurdin. Wengine nao walikwenda kwa makundimakundi. Wengine wawili, wengine watatu. Ikawa hivyo.

Tuliingia kwenye duka moja la nguo kwani mimi nilikuwa nataka kununua suruali za jinsi na t-shirt. Ndani ya duka lile, tulikutana na wanawake watatu, kama Waraabu hivi, walivaa baibui ambao nao walikuwa wakinunua nguo za kike. Mwanamke mmoja akaniangalia sana kisha akaniambia: “Wewe nakufahamu ni Mtazania, unaitwaaa…”
Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma mkasa huu kwenye Gazeti la Ijumaa, kesho Ijumaa.

Leave A Reply