The House of Favourite Newspapers

Hii Sasa Ndiyo Yanga Yenyewe

Obrey Chirwa akijaribu kumtoka kipa wa timu ya Azam Fc.

LICHA ya Yanga jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC lakini kikubwa ambacho kilionekana kuwafurahisha mashabiki wengi wa soka ni namna beki wa kushoto wa vijana wao wa Jangwani, Gadiel Michael alivyofunga bao zuri.

 

Baada ya ushindi huo kwa Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo sasa wamepunguza pengo dhidi ya vinara Simba ambao wao wana pointi 32 dhidi ya zile 28 za Yanga. Kocha George Lwandamina jana alikaa kwenye benchi la Yanga baada ya kupata kibali kipya cha kazi.

 

Yanga ikicheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, walianza mchezo huo kwa kasi na baadaye Azam walionekana kutawala na kufanikiwa kuandika bao la kwanza katika dakika ya tatu kupitia kwa Shaban Chilunda ambaye aliunganisha krosi kutoka kwa Bruce Kangwa kutoka upande wa kulia.

 

Baada ya bao hilo, Yanga walikuja juu na kufanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Obrey Chirwa ambaye hili sasa linakuwa bao lake la saba akiunganisha pasi ya mbali kutoka kwa Ibrahim Ajibu katika dakika ya 30.

Pasi hiyo ilitokana na mpira wa faulo ambao ulitokana na mchezaji wa Yanga kufanyiwa faulo hivyo Ajibu akapiga moja kwa moja na kumzidi ujanja kipa bora wa Azam, Razack Abalora ambaye alitokea kujaribu kuuokoa lakini ikashindikana.

 

Yanga ambayo ilipata kadi za njano kwa wachezaji wake Kelvin Yondani na Papy Kabamba Tshishimbi, kutokana na kucheza faulo, ilipata bao lake la pili dakika ya 43 kupitia kwa Gadiel ambaye aliachia mkwaju mkali nje ya 18 na kutinga moja kwa moja wavuni huku kipa Razack akijaribu kuuzuia bila mafanikio. Gadiel alifunga baada ya kupokea pasi kutoka kwa Tshishimbi.

Lakini jambo ambalo lilionekana kuwa zuri kwa pande zote ni lile la wachezaji wa pande zote kuhamasishana pindi ilipotokea wakafanya tofauti na matarajio lakini tatizo lilikuwa kwa Kocha wa Azam, Aristica Cioaba kujibizana na mashabiki wa Yanga waliokuwa jirani na benchi lake.

 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo Mjuni ilishuhudiwa akitoa kadi saba za njano na nyekundu moja kwa kiungo wa Azam, Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ dakika ya 81 baada ya kumsukuma Hassan Kessy ambaye hakuwa na mpira. Wengine waliopata kadi ni Aggrey Morris, Chilunda na Steven Kingue wote wa Azam FC na kufikisha kadi tano ambazo kikanuni wataadhibiwa na Bodi la Ligi faini ya Sh 500,000.

 

Baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema: “Tumeupokea ushindi kwa furaha, nawapongeza wachezaji wetu kwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kupata ushindi.”

 

Naye Kocha Msaidizi wa Azam, Idd Cheche yeye alisema; “Tumekubali matokeo na hivyo ndivyo soka lilivyo.”

Azam; Razack, Himid Mao, Kangwa, Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Sure Boy, Joseph Mahundi, Shaban Idd, Bernard Arthur na Enock Atta.

Yanga; Youthe Rostand, Kessy, Gadiel, Andrew Vincent, Yondani, Said Juma Makapu., Raphael Daud, Tshishimbi, Chirwa, Ajibu na Emmanuel Martin.

Comments are closed.