The House of Favourite Newspapers

Hivi Hii TFF Inawataka Nini Mashabiki

ISHU sasa ni ushiriki wa aibu wa timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars katika michuano ya Kombe la Chalenji ambayo leo Zanzibar wanacheza fainali na Kenya.

 

Kilichowaumiza mashabiki na wadau wa soka ni Kili Stars kutolewa mapema ikipoteza mechi tatu na kutoka sare moja lakini Zanzibar ambayo haikupewa nafasi kubwa ikicheza fainali.

 

Lakini ukiangalia ishu ya ushiriki wa Stars ni kama TFF inacheza na akili za mashabiki. Ilidharau michuano hiyo huku ikiitumia kumjaribu kocha ambaye alionekana kupwaya.

 

Kinachouma na kuonekana ni dharau kutoka kwa TFF ni kukosekana kwa jibu la moja kwa moja, huku wahusika wakidai watatazama video ili kujua kilichotokea.

 

Ina maana hata Mkurugenzi wa Ufundi anadharau kutazama mechi ya timu ya taifa ikicheza nje ya nchi, ana kazi gani inayomuweka bize kiasi hicho?

 

Hatukatai timu kufungwa laweza kuwa kosa la kimchezo lakini uaminifu wa ghafla wa TFF kwa Kocha Ammy Ninje na kutomuwekea mtu wa kumshitua alipoonekana kukosea.

 

Kama mechi ya kirafiki dhidi ya Benin tayari tatizo lilionekana nyuma ya tatizo hilo Ninje alikuwepo kwani ndiye aliyekuwa mshauri wa Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga.

 

Kwa mfano anayecheza beki namba mbili hakupangwa na badala yake akachezeshwa kiungo namba sita katika nafasi hiyo, kisa tu mshambuliaji wa timu pinzani ana kasi.

 

Ilishindikana vipi beki mbili asibaki katika nafasi yake ila akaongezewa mbinu za kumkabili mshambuliaji mwenye kasi kuliko kumtoa kabisa? Tukafungwa na lawama zikaenda kwa Mayanga.

Mayanga wala hakuweka maneno mengi, akatulia lakini ilifahamika wazi kosa lilitokea kwa Ninje ambaye kidogo soka la Afrika halipo kichwani mwake kwani ametumia muda mwingi nje ya nchi.

 

TFF ilimuamini Ninje mapema sana na kumpa jukumu kubwa kuliko uwezo wake na yawezekana kweli ana elimu kubwa ya soka lakini mazingira yakamkwamisha, kwa hali ilivyo sasa na aina ya mashindano tuliyokuwa tunakwenda kushiriki hakukuwa na haja ya kumjaribu kocha. Angepewa mtu wa kazi akafanye kazi.

 

Kitendo cha TFF kumpa mikoba yote Ninje pia kutotoa tamko la kueleweka baada ya timu kuchemka ni dharau na inaonekana hata yenyewe ilidharau michuano hii kiasi cha kumuamini kocha huyo dhaifu kwa timu za taifa. Kwa aina ya wachezaji tuliokuwa nao walihitaji mbinu tu kucheza fainali, lakini ilionekana kabisa kwamba kwenye benchi hakukuwa na jipya jambo ambalo lilisababisha hata mashabiki kuichukia timu yao kwa sababu za kulazimishwa na TFF.

TFF ilidharau na ikaumbuka baada ya Zanzibar kupitia kikosi chake cha Zanzibar Heroes kufanya vizuri na leo kinacheza fainali.

 

Sasa tunajificha katika kichaka cha Zanzibar kutukana timu ya Bara, sawa ni kosa na hatuwezi kufurahia upuuzi huo, ila jambo la msingi hapa ni kufanya vizuri.

Zanzibar ilijiopanga vizuri na yenyewe ikajibu kwa kuonyesha uwezo wake na hata kama ikifungwa leo watabaki kuwa mashujaa wa Tanzania katika michuano hiyo na wameonyesha nia tangu siku ya kwanza mpaka ya mwisho. Ukiangalkia timu inavyocheza Uwanjani unaona kabisa kuna kitu kinatafutwa lakini kwa Stars ilikuwa na kocha mwenye mtazamo wa majaribio.

 

Kili Stars imeonekana kama timu ya kisela, inayofundishwa na kocha msela, ikachukua wachezaji wa kisela waliocheza kisela na ikatolewa kisela na ikaona kila kitu kinaenda kisela.

Usela wa TFF, kocha na wachezaji ndiyo uliotufikisha hapa tulipo na wanajua Watanzania ni watu wa kuongea siku mbili tatu halafu husahau kila kitu.

Hivi usipochukua Kombe la Chalenji kwa timu kama Kili Stars unataka kuchukua kombe gani? Maana kufuzu Afcon hatuwezi wala Chan hata Kombe la Dunia.

 

Badala ya mambo ya kisela, Kili Stars angepewa kocha kama Mecky Maxime hata Shadrack Nsajigwa au Jamhuri Kihwelo au wote watatu halafu wangepambana na hata kama wangeshindwa tungejua uwezo wao umeishia hapo na wakati mwingine wangekuwa vizuri zaidi.

 

Kama Kombe la Chalenji kilikuwa kipimo cha Ninje ili apewe Taifa Stars, kitakuwa ni kituko cha mwaka ambacho tutajutia miaka yote.

 

Ninje anaweza kuwa kocha mzuri lakini ni aina ya kocha anayetakiwa kukaa na timu kwa muda mrefu ili azoee wachezaji baada ya kuwajua kisha kuweka mbinu zake.

 

TFF ikirudia kufanya usela kama iliyotufanyia katika Kombe la Chalenji kwa kumjaribu Ninje, hawatakuwa tofauti na tawala zilizopita katika shirikisho hilo.

Tufanye mambo siriazi. Tuache kuwajaza hasira mashabiki pasipo sababu. Timu ya Taifa ichukuliwe umuhimu stahiki na ipewe hadhi yake. Si sehemu ya kujaribu watu.

STORI: MICHAEL MOMBURI | SPOTI XTRA

Comments are closed.