The House of Favourite Newspapers

Hofu Yatanda Mtoto wa Mwaka Mmoja Kutoweka

0

PWANI: Hofu imetanda baada ya mtoto Shadra (1), mkazi wa Kijiji cha Mwanzo Mgumu, Chanika mkoani Pwani kutoweka ghafla kwenye mazingira ya kushangaza.

 

Familia ya Shafii Njanike, ambaye ndiye baba wa mtoto huyo, iko kwenye sintofahamu tangu mtoto huyo atoweke Agosti 31, mwaka huu, ambapo inadaiwa alikuwa akicheza na watoto wenzake.

 

“Yaani kwa kweli tunaishi kwa hofu, maana mazingira ya mtoto kutoweka tunashindwa kuelewa ni nini hasa kilichomfanya mtoto huyo atoweke ghafla,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Abdul.

 

Akizungumza na mwanahabari wetu baba wa mtoto huyo, Shafii alisema siku ya tukio majira ya saa kumi na moja jioni, alipigiwa simu na mkewe, Swaumu Mwijuma ambaye alimtaarifu kuwa anamtafuta mtoto huyo ambaye kuna muda alimuacha akicheza na wenzake nyuma ya nyumba, lakini ghafla ametoweka na kuwaacha wenzie wakilia.

 

“Baada ya kuambiwa hivyo, nilishtuka na kurudi nyumbani haraka, maana nilikuwa kwenye shughuli zangu ambazo ninapofanyia si mbali na nyumbani.

 

“Nilipofika tuliwauliza watoto wenzake alipokuwa akicheza nao, ambapo kila tulipowauliza walianza kulia na kusema wakiwa wanacheza, kuna mtu alitokea na kumchukua mwenzao.

 

“Kila tulipowauliza, waliendelea kusema hivyo ambapo tulipowaambia watutajie mtu huyo au kutupa maelezo jinsi alivyo, waliishia kuendelea kulia,” alisema baba huyo na kuongeza.

 

“Baada ya kuona zoezi la kuwahoji watoto hao limekuwa gumu, mimi na wanakijiji wenzangu, tulianza kumsaka kwenye vichaka, mashimo na makorongo mbalimbali hapa kijijini na vijiji vya jirani ambavyo na vyenyewe tuliwapa taarifa hiyo na kuanza kusaidiana nao kufanya msako.

 

“Baadhi ya vijiji vya jirani tulivyoshirikiana navyo, ni pamoja na Migambo, Bupu, Bwama, Chungu lakini mpaka sasa bado hatujampata.

 

”Naye baba mkubwa wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Nassoro Njanike, alisema kutokana na tukio lenyewe kuwa na utata, walifanya kila jitihada ikiwemo kwa wataalamu wa mambo ya asilia, lakini bado juhudi zao zimegonga mwamba.

 

“Si kwa wataalamu wa asilia tu, hata kwa viongozi wa kidini kwa mashehe na wachungaji, pia tumehangaika na bado tunahangaika, ukweli tupo kwenye wakati mgumu sana,” alisema Nassoro.

 

Kufuatia sakata hilo, mwanahabari wetu alizungumza na Mwenyekiti wa Kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Jabiri Kibiriti, ambaye alithibitisha tukio hilo kutokea kijiji hapo na kusema, hiyo si mara ya kwanza kutokea.

 

“Hivi karibuni kabla ya huyu kupotea, kuna jamaa mwingine naye alipotea, lakini baada ya muda alipatikana akiwa hai kwenye migomba iliyokuwa nyuma ya nyumba yao akiwa hajitambui.

 

“Kila alipohojiwa alipokuwa, hakuwa na jibu la kueleweka kwa sababu mtu mwenyewe alikuwa kama amechanganyikiwa,” alimaliza kusema mwenyekiti huyo.

 

Taarifa hiyo imeripotiwa Kituo cha Polisi cha Kisarawe, Pwani kwenye jalada lenye KIS/RB/793/2020 ambapo uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

STORI: RICHARD BUKOS, RISASI JUMAMOSI

Leave A Reply