The House of Favourite Newspapers

Hongera JPM Kwa Kulinda Maadili

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.

ASANTE Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi nyingine ya kuweza kuzungumza na mashabiki wa Barua Nzito, ambao wamekuwa msaada mkubwa katika kukamilisha makala haya.

 

Nimekuwa nikizungumza mambo mengi sana kuhusu wasanii wetu ikiwemo tabia na mienendo yao.

Leo nitazungumza furaha niliyonayo baada ya kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ya kutaka wasanii wanaovaa na kupiga picha za nusu utupu wachukuliwe hatua.

 

Nimefurahi kwa sababu na mimi ni muumini wa maadili hayo aliyoyasema JPM. Kwani uvaaji wa nusu utupu siyo maadili ya Kitanzania, tuwaachie wenyewe.

 

Nikiwa kwenye Uzinduzi wa Filamu ya From Nigeria, nilishuhudia wasanii wakiwa kwenye mavazi f’lani ambayo kidogo yana staha siyo kama yale waliyokuwa wakivaa kabla ya agizo la rais.

 

Nilichokipenda zaidi ni kituo kimoja cha luninga ambacho kilikuwa kinarusha mubashara matangazo yale, kuhakikisha kinawapa mwongozo wasanii na mashabiki ambao walikuwa wamevaa kihasara hasara.

 

Nikiwa jirani na zulia jekundu nilishuhudia mwanadada aliyekuwa akipokea wageni, akimsimamisha mrembo mmoja na kumsawazisha kinguo chake tena kwa maneno.

 

“Mdogo wangu, JPM hataki haya mambo, vaa vizuri tu mbona unapendeza. Kwani hujasikia kauli ya rais, sisi tuko mubashara hatuwezi kuthubutu kukuacha ukaenda hewani ukiwa nusu utupu.”

 

Nilifurahi kuona mbegu ya maadili aliyoipanda JPM imeanza kumea kwa watu wengine.

 

Kuwa na maadili ya nchi yako, huo nao ni uzalendo. Ilikuwa ni jambo la kawaida kwa wasanii kujiachia na kuvaa nguo za nusu utupu ama kwa kuwashawishi watu wafanye nao biashara za ngono au kujitangaza.

Kitendo cha Rais Magufuli kusema kuwa, mamlaka husika wasimamie suala la wasanii ambao wamekuwa wakipiga picha za nusu utupu, wakifanya video au filamu basi lazima sehemu kubwa ya miili yao ionekane. Binafsi nilisikia furaha moyoni mwangu, kuona kumbe hata rais hapendezwi na watu wake kuharibika.

 

Kwa mtindo huu wa JPM naiona nchi nzuri yenye heshima, amani na maadili mema ikirejea tena.

Ingawa mamlaka kama TCRA, Basata na nyinginezo ni kama zilikuwa zimelala, lakini sheria zipo, sijajua ni kwa nini walikuwa wanashindwa kuzitumia katika kukemea na kukabiliana na uchafu wa mapichapicha ya nusu utupu.

 

Hivi wasanii wa kike nani kawaambia hamuwezi kufanya video nzuri bila kuvaa nusu utupu. Nani kakwambia muda wote anahitaji kuona vipaja vyako hovyohovyo. Huko ni kushusha thamani ya mwanamke na kuwafanya wanaume wawe wazinzi kwa kutamani kwako.

 

Mara nyingi nimekuwa nikikemea picha na video chafuchafu za wasanii ambao wamekuwa wakipiga na kuposti.

Niliwahi kuwaandikia Amber Lulu, Gigy Money, Sister Fay, Sanchi na wengine wengi. Sikuwa nina chuki nao bali hili alilolisema Rais Dk John Pombe Magufuli ndilo lililokuwa nalimaanisha siku zote.

 

Zipo tamaduni za kuiga kutoka Magharibi kama teknolojia, maendeleo na elimu lakini si kila kitu tunachukua.

 

Vuta picha mwanamke kama Sister Fay anaibuka sehemu ya umati wa watu akiwa kavaa nguo ya kulalia. Hivi kweli inaingia akilini? Mwanamke mwenye watoto ambao kesho na kesho kutwa wanaweza kuuona utumbo wake alioufanya kwenye mitandao ya kijamii, unadhani watoto wanajifunza nini kama siyo kuwaharibu na kuwabomoa kabisa katika suala zima la maadili?

BARUA NZITO NA GABRIEL NG’OSHA

Comments are closed.