The House of Favourite Newspapers

Husna, kuibiwa bwana’ko ujitakie mwenyewe!

0

husna (1)MAISHA ya ustaa Bongo yana mambo mengi sana yenye kuchefua nyuma ya pazia. Wakati ule nikila ujana, nilishuhudia mengi katika kumbi za starehe ambazo ziliwahusisha mastaa wa fani mbalimbali hasa muziki na filamu.

Kwa mastaa wa kiume, hasa wa muziki wa kizazi kipya, wengi wao ni watu wa kutumia fedha zao kufanya yao, mitungi, mademu na starehe zingine wanazohitaji. Katika kundi hili wapo pia mastaa wa filamu wa kiume, ni watu wa matumizi!

Wanamuziki wengi wa muziki wa dansi ni tegemezi kwa mapedeshee, wakishawataja majina jukwaani, wakati wa mapumziko watashuka na kuanza kukusanya mishiko, vinywaji na misosi. Pale kwa Papaa Ojuku atachukua, halafu atasogea kwa Pedeshee Kitula na atamalizia kwa ‘mukubwa’ Kambili. Hayo ndiyo maisha yao.

Lakini kwa mastaa wa kike, wa fani zote, ni asilimia isiyozidi kumi ambao utawakuta wanakula maisha kwa fedha za jasho lao, hata wawe na majina makubwa vipi. Hawa nimewashuhudia, ninawajua.

Wengi wanapenda mteremko. Na kama walivyo mademu wa uswahilini, nao wana tabia kama hizo. Leo mmoja atampata mdau anayevutiwa na kazi zake, iwe muziki au filamu, atamwita sehemu ampe juisi. Kutaka kujionesha au kuogopa, atamchukua shosti wake na kuambatana naye.

Watakula bata na kufanya yanayowezekana. Kesho na kesho kutwa shosti anaitwa shemeji na maisha yanaendelea kwa staili hiyo. Lakini kama tunavyojua, masista wetu wanapenda maisha mazuri, kwa hiyo akipatikana mtu anayewezesha kirahisi, atajipatia kirahisi.

Ndiyo maana mastaa wetu wa kike wanaingia sana katika kashfa ya kuchukuliana mabwana kwa sababu ya kuitana kwenye mitoko ya usiku. Na wakware wengi wanapenda ujiko wa kutembea na mastaa wengi kadiri wawezevyo.

Ndiyo maana sikushangazwa sana na madai ya video queen na mshiriki wa Miss Tanzania mwaka 2011, Husna Maulid kwa wenzake, Wolper na Lulu kuwa safari hii wakimchukulia bwana’ke, patachimbika!

Ukifuatilia sana sakata lao, hautakuwa mbali sana na vile nilivyoeleza mwanzo, kwamba kukutana kwao ni kwenye mitoko ya usiku maana ratiba za mastaa wengi wa Bongo zinafanana, kama hawatakutana kwenye kumbi za burudani, tamasha au uzinduzi wa kitu f’lan, basi ni kwenye pati ya pedeshee au mwenzao!

Lakini kama wangekuwa wana maisha ya kujitegemea, hasa kiakili, skendo kama hizi zingekuwa adimu kwao kwa sababu kila mmoja angekuwa anakula bata kivyake na kukutana kungetokea tu kwenye matukio muhimu.

Unaweza kujiuliza kwa mfano, kwani Wolper na Lulu watamuona wapi bwana’ke Husna hadi wamchukulie? Na huyo mwanaume, yukoje hadi hawa wadada wakimuona tu wamrukie na kumchukua?

Labda nimshauri Husna na pengine Wolper na Lulu kwa niaba ya wenzao wote wanaopenda maisha ya kujionesha. Ustaa wao una maana kubwa kwao, hasa kwa kizazi hiki cha sasa.

Huu ni wakati wa kuzitumia fursa wanazokutana nazo, kujaribu kuangalia vipi maisha yao ya kesho yatakuwa. Hata uwe mrembo vipi, maisha ya klabu yana mwisho wake.

Na wanaume wenye nazo hawakauki isipokuwa wanabadilika kutoka kizazi hadi kizazi. Leo zamu yako kugonganisha mabwana, kesho zamu ya bintiyo. Utaishi kumsubiri arudi klabu ili maisha yaende?

Lakini kama utatumia fursa hivi sasa, unao uwezo wa kujijenga kiuchumi na kuepuka maisha ya kukimbiza wanaume sehemu za starehe. Hakuna raha kwa mwanamke kama kutumia fedha zinazotokana na juhudi zako maana hata wanaume huwa na heshima. Lakini kama ni mtu wa kutegemea uzuri, kuna watu wana hela za kuweza kumuonja kila mzuri duniani halafu hawaoi!

Leave A Reply