The House of Favourite Newspapers

Huu ni Undani Ugonjwa Uliomuua Bilionea Bongo

0

DAR: Taarifa za kifo cha mfanyabiashara Ali Mufuruki (60), zimeshtua wengi. Mufuruki anayetajwa kuwa mmoja wa mabilionea Bongo alifariki dunia, usiku wa kuamkia jana nchini Afrika Kusini alikokimbizwa kwa matibabu.

 

Mufuruki ambaye ni mwenyekiti mwanzilishi wa Jukwaa la maofisa watendaji wakuu wa kampuni (CEO Round Table) amekutwa na umauti akiwa na familia yake.

 

Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Mufuruki ni kati ya matajiri wakubwa 10 wa Tanzania akikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani milioni 110 (zaidi ya shilingi bilioni 250 za Kitanzania.

 

Ndiye mmiliki wa Kampuni ya Infotech Investment Group Limited na maduka ya Wolworth.

Oktoba 18, mwaka huu, alijiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania ili kupata muda zaidi wa kuendelea na biashara zake.

 

Mwenyekiti wa sasa wa Ceort, Sanjay Rughan, jana alithibitisha kutokea kwa kifo hicho kilichotokea saa tisa alfajiri katika Hospitali ya Morningside nchini Afrika Kusini.

Sanjay alisema, awali Mufuruki alilazwa katika Hospitali ya AghaKhan, lakini juzi hali yake ilibadilika na kukimbizwa Afrika Kusini.

Sanjay alisema, Mufuruki alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa homa ya mapafu.

 

JPM AMLILIA

Kwa upande wake, Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ alieleza kusikitishwa na kifo cha mfanyabiashara huyo.

“Nimehuzunishwa na taarifa za kifo cha rafiki yangu, Ali Mufuruki (Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Jukwaa la Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni -CEOrt).

“Nitamkumbuka kwa uzalendo na mchango wake katika kukuza sekta ya biashara na ushauri kwa Serikali. Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un,” aliandika JPM kupitia ukurasa wake wa Twitter.

 

UNDANI WA UGONJWA

Akizungumzia ugonjwa uliotajwa kumuua Mufuruki, daktari anayeandikia gazeti hili, Abdallah Mandai alisema homa ya mapafu au nimonia hutokana na kuvimba kwa seli katika moja au mapafu yote.

“Mwishoni mwa mirija ya kupumulia, kuna mifuko midogo. Unapokuwa na homa ya mapafu, mifuko hiyo huvimba na kujaa maji hivyo kusababisha ugumu katika kupumua, homa, kukohoa, kutoka jasho kutetemeka au kupoteza hamu ya kula,” alisema Dk Mandai.

 

DALILI

Dk Mandai alisema dalili za awali za nimonia huanza kuonekana ndani ya saa 24 mpaka 48. “Moja ya dalili hizo ni kukohoa. Mgonjwa anaweza kutoa makohozi mazito ya rangi ya njano au kikohozi kikavu,” anasema na kuongeza;

“Nyingine ni kikohozi kikavu, kutokwa jasho hasa usiku, kichefuchefu, kutapika na maumivu ya misuli. “Mgonjwa anaweza kuhisi mapigo ya moyo na pumzi kwenda kasi, kukata pumzi kukichukua muda mrefu kidogo basi uzito unapungua.

 

“Dalili za hatari zinazohitaji huduma za haraka za daktari ni pamoja na homa kali, kushindwa kupumua na rangi ya ngozi kuwa ya bluu.”

Dk Mandai anasema mgonjwa anaweza kubanwa na kifua, kuhisi maumivu ya kichwa na kupoteza hamu ya kula.

 

KINGA

“Nimonia unasababishwa na bakteria au virusi na namna ya kwanza ya kuuepuka ni kuzingatia usafi. Mgonjwa anashauriwa kutumia kitambaa safi kila anapokohoa au kupiga chafya na kujifuta. “Anashauriwa kukitupa kitambaa kilichotumika kwani wadudu wanaweza kukaa humo kwa muda. Vilevile mgonjwa anashauriwa kunawa mikono ili asiwaambukize wengine vimelea vya ugonjwa.

“Kulinda afya kwa kuepuka matumizi ya sigara kunakoathiri mapafu na kutoa mwanya wa maambukizi kunasaidia kutoshambuliwa na ugonjwa huo,” anasema.

 

TAHADHARI

Wataalam wa afya wanansema ugonjwa huu unatibika endapo muathirika atawahi hospitali na atazingatia ushauri wa daktari.

Stori:Mandishi Wetu

 

Leave A Reply