The House of Favourite Newspapers

Idadi ya Vifo Yazidi Kuongezeka Mafuriko China, Mamia Wanaswa Kwenye Treni

0

IDADI ya watu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko makubwa yaliyoikumba China, inazidi kuongezeka huku vikosi vya uokoaji vikifanya kazi ya ziada kuwanasua mamia ya watu walionaswa kwenye treni lililosombwa na mafuriko.

 

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la CNN, mpaka Alhamisi, Juni 22, 2021 zaidi ya watu 33 wameripotiwa kufariki dunia huku watu wengine nane wakiwa hawafahamiki walipo.

Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zilizolipiga Jimbo la Henan kuanzia wikiendi iliyopita na kusababisha maelfu ya watu kupoteza makazi na miundombinu karibu yote, ikiwemo usafiri wa treni, ikiharibiwa vibaya.

 

Mbali na maafa hayo, mafuriko hayo yaliyobomoa kingo za mito kadhaa, yamesababisha maporomoko ya ardhi katika Jimbo la Hunan lenye wakazi zaidi ya milioni 99, wengi wakiwa na hali duni za kimaisha.

Mbali na Jimbo la Henan, jimbo jingine la Zhengzhou lenye wakazi zaidi ya milioni 12, nalo limeathiriwa vibaya na mafuriko hayo na kusababisha vifo vya takribani watu 12 wakikwama kwenye stesheni ya treni jimboni humo.

 

Katika picha na video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zinaonesha magari yakiwa yanasombwa na mafuriko hayo, huku video nyingine za kusisimua zikiwaonesha mamia ya abiria wakiwa wamekwama ndani ya treni, huku maji yakizidi kujaa na kuzua taharuki kubwa kwa abiria hao.

Miongoni mwa stesheni za treni zilizoathiriwa zaidi, ni ile ya Line 5 katika Kituo cha Zhengzhou ambapo maji yalianza kujaa kwenye treni iliyokuwa imejaza mamia ya abiria na kusomba njia zote za treni hiyo.

 

Video hizo zinawaonesha abiria wakiwa wamesimama juu ya siti za treni, wengine wakiwa wananing’inia kwenye mabomba wakijaribu kuokoa maisha yao. Katika video nyingine, miili kadhaa inaonekana ikiwa imetapakaa eneo la kituo hicho cha treni huku mafuriko yakizidi kuongezeka kasi.

Mamlaka nchini China, zinasema zaidi ya abiria 500 waliokolewa katika treni iliyokuwa imejaa maji kutokana na mafuriko hayo huku watu 12 wakipoteza maisha na wengine watano wakijeruhiwa vibaya.

 

Kwa mujibu wa mwanamke mmoja aliyekuwa miongoni mwa watu waliokuwa wamenaswa kwenye treni hiyo, anaeleza kwamba walikuwa kwenye safari za kawaida za treni hiyo, walipofika kwenye kituo hicho, ndipo maji yalipoanza kuingia kwa kasi ambapo mamlaka husika ziliwataka abiria wote kutoka ndani ya treni ili kuokoa maisha yao.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, tangazo jingine likasikika likiwataka abiria wote kurudi ndani ya treni kwani mafuriko yalikuwa yakija kwa kasi kubwa. Anazidi kueleza kuwa baada ya abiria wote kurejea ndani ya treni, maji yalikuwa yamejaa na kufikia viunoni, yakazidi kuongezeka mpaka usawa wa shingo na kusababisha abiria waanze kupanda juu ya viti.

 

Baada ya maji kuzidi kujaa, ndipo vikosi vya uokoaji vilipowasili na kuanza kukata mabati ya juu ya treni na kuwatoa abiria ambao wengine walishaanza kupoteza fahamu huku kadhaa wakipoteza maisha.

Zaidi ya askari wa vikosi vya zimamoto na uokoaji 6000 na wanajeshi 2000 walipelekwa haraka eneo la tukio kwa ajili ya kunusuru maisha ya abiria hao pamoja na watu wengine waliothirika na mafuriko hayo. Utabiri wa hali ya hewa, unaonesha kwamba mvua kubwa zitaendelea kunyesha Alhamisi na Ijumaa na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Leave A Reply