The House of Favourite Newspapers

Idris Anavyowapiga Tobo Kina Kingwendu!

0

DUNIA inapitia mabadiliko makubwa mno ya kiteknolojia. Zamani ilikuwa ni fahari sana kuonekana kwenye runinga kwa sababu watu walikuwa na muda wa kukaa nyumbani kuitazama kwa saa nyingi.

Ila sasa hali hiyo haipo tena. Watu hawana muda. Watu wako busy sana katika mitandao ya kijamii.

Ingia kwenye daladala au kaa baa uone watu walivyo busy mitandaoni. Ugumu wa maisha na kuongezeka kwa mahitaji ya kijamii kumefanya watu wakose kabisa muda wa kukaa nyumbani.

Ni kawaida sasa hivi mtu kutotazama runinga kwa mwezi mzima ila ni ngumu kutoingia kwenye mitandao ya kijamii kwa saa tatu. Ndipo tulipofikia.

Mitandao ya kijamii imekuja na nguvu na kuleta mapinduzi ya aina yake kwenye maisha yetu.

Angalia walioamua kufanya biashara ya sanaa kupitia mitandaoni na wale walioamua kukataa kwenda sawa na mabadiliko haya. Angalia kasi ya ukuaji wao. Wale walioamua kuchagua kwenda na mitandao ya kijamii, wengi wao wanakua haraka kuliko wale walioamua kuwa ving’ang’anizi.

Yote hii ni kwa sababu mitandao ya kijamii imekuja na nguvu na ushawishi wa kipekee.

Nataka kuwazungumzia waigizaji wa vichekesho au ucheshi wa mitandaoni na wale wa kwenye runinga.

Zamani, enzi za kina marehemu Max na Zembwela, Bambo, Senga na Orijino Komedi, hakukuwa na Facebook, Twitter, Instagram au whatsApp. Katika enzi hizo ilikuwa ni lazima kutazama runinga ili kuona kinachopaswa kuonekana.

Ndipo katika kipindi hiki wasanii hao tajwa na wengineo walikuwa wakizungumzwa zaidi.

Ila mambo yamebadilika. Kina Ebitoke wamejulikana kupitia mitandao ya kijamii. Anna Kansiime wa Uganda ni maarufu mno kuliko Bambo ila wao waliamua kujitangaza katika mitandao ya kijamii.

Kule Nigeria kuna Mark Angel. Ni komediani mwenye hadhi na heshima ya kipekee ndani na nje ya Nigeria. Umaarufu wake siyo wa kwenye runinga ila mitandaoni.

Kuna kitu nakiona hapa Tanzania. Waigizaji wengi wa komedi wameshindwa kuiona fursa iliyopo kwenye mitandao na matokeo yake kina Kingwendu wanalalamika kwamba walifanya kazi kubwa kipindi kile ila sasa hawana kitu zaidi ya umaarufu kunuka.

Mabadiliko makubwa ya dunia yanaenda sambamba na ugumu wa maisha na matarajio mengi. Kutokana na hali hii, wengi hupenda wakiwa katika usafiri au muda wa lanchi kuingia mitandao mbalimbali na mambo mengine ili kuangalia mambo ya kufariji na kuburudisha.

Wasanii wa zamani wa vichekesho wameshindwa kuona fursa hii. Ila Jaymond, Dullivan waliiona na kuitumia vizuri.

Nafahamu siyo rahisi sana mtu aliyezoea kuigiza kwa saa moja kwenye runinga kuibuka shujaa katika vichekesho vya mitandaoni. Mfumo wa mitandao uko tofauti sana. Huku unatakiwa kutumia dakika chache mno ila ujumbe wako uweze kufika na kueleweka.

Binafsi naamini wachekeshaji wengi wa runinga hawashindwi kufanya hivi, akiamua kwa dhati na kujua thamani ya kufanya hivi.

Inakera sana kila muda kusikia kwamba wasanii wa vichekesho wakilalamika hawana thamani.

Wengine hufikia hatua ya kusema hata watengeneza filamu wengi hawawachukulii katika uzito unaostahili.

Sidhani kama wachekeshaji wetu wanahitajika kusema haya. Katika dunia iliyo wazi namna hii, katika dunia iliyojaa stresi za kila namna. Stresi za uchumi, mapenzi, siasa hata dini, unashindwa vipi kupenya na kupata unachotaka? Muhimu ni ubunifu na kujua mahitaji ya wakati tu.

Fursa ya sasa hivi iko katika mitandao. Mchekeshaji unasubiri nani akupe thamani ya uwezo wako wakati wenzako wanafanya vema kupitia mitandao? Idris Sultan heshima na umaarufu wake uko juu kwa sababu ya vichekesho vyake. Wengi leo wanamzungumzia kama mchekeshaji kuliko kama aliyewahi kushinda Big Brother.

Inashangaza kuona wachekeshaji kama kina Zimwi hatuwasikii tena. Inatia aibu kuona kina Kingwendu wakitegemea tena kuibuka mashujaa kupitia runingani. Amkeni, kila zama na mambo yake.

Ndiyo, huwezi kukataa nguvu na thamani ya runinga ila ni ukweli ulio bayana ni kwamba kwa sasa runinga siyo kitu pekee unachoweza kukitegemea ili kuonesha umahiri wako wa kuchekesha au kufanya mambo yako.

MAKALA: RAMADHAN MASENGA  

Leave A Reply