The House of Favourite Newspapers

IGP Mangu wanaokuchafua ni hawa

0

mangu_e

NA ERIC SHIGONGO

Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa uhai leo, hakika anastahili kuabudiwa leo na siku zote.

Makala haya nazungumzia utendaji ndani ya jeshi la polisi kwani kuna askari ni wachapakazi kwelikweli lakini pia wapo wachache wanaowaangusha na lawama kumuangukia Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP).

Nasema hivyo nikiwa na mifano kadhaa na nirejee hukumu ya kesi iliyokuwa inamkabili Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa Mkoa wa Iringa,PC  Pisificus Simon aliyemuua Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Chanel Ten, Daudi Mwangosi ambayo iliacha maswali mengi bila majibu.

Kesi hiyo ilisikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ambayo ilisikiza upande wa Jamhuri pamoja na upande wa utetez kisha ikamhukumu askari huyo kifungo jela kwa miaka 15 kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Jaji aliyetoa hukumu hiyo alisema alimhukumu askari PC Simon kutokana na ungamo alilotoa mbele ya mlinzi wa amani lakini siyo ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ambayo ndiyo iliyofungua kesi. Jaji alisema Jamhuri ilishindwa kuwafikisha mahakamani mashahidi muhimu ili kuthibitisha kama mtuhumiwa alitenda kosa la kuua kwa makusudi.

Mashahidi muhimu kwa mujibu wa jaji huyo ni aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, SACP Michael Kamuhanda na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa, Nyegesa Wankyo. Na Upande wa Jamhuri uliwasilisha vielelezo vitano pamoja na gazeti moja lililochapisha picha lakini likapokelewa kama utambulisho na siyo kidhibiti kutokana na kutokidhi vigezo vya kisheria.

Hapo ndipo mimi na wananchi wengine tunajiuliza, polisi walifanya makusudi kutotimiza wajibu wao? Kwa nini mashahidi muhimu hawakuitwa katika kesi hiyo ambayo uhai wa mtu umepotea? Kwa nini Jamhuri lishindwa kumleta mahakamani mpiga picha aliyepiga picha wakati Mwangosi anauawa?

Tukio la maujaji ya Mwangosi lililotokea Septemba 2, 2012 na polisi walitumia nguvu nyingi kukanusha kuhusika kwa askari wao. Taarifa zilipotoshwa na kudaiwa kuwa aliuawa na waandamanaji waliorusha kitu kilichomuua mwana habari huyo. Lakini mara baada ya kuchapishwa picha kwenye gazeti ikionesha askari alivyokuwa akimpiga bomu la machozi Mwangosi, juhudi za kuficha ukweli ziliyeyuka kwa kuwa kila kitu kilikuwa wazi.

Hapo ndipo watu wakaanza kujiuliza,  polisi waliacha kuwapeleka mashahidi muhimu mahakamani kwa sababu hawakutaka ionekane askari yule aliua makusudi au alikusudia? Na kwa kutompeleka hata mpiga picha ile ambaye sasa naye ni marehemu, Joseph Senga, walikuwa na maana gani?

Nimeamua kusema haya kwa sababu hii si mara ya kwanza kwa baadhi ya watendaji wa polisi kuwasilisha ushahidi dhaifu mahakamani kwani mwaka 2006 kuna wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge Morogoro  na dereva teksi wa Dar waliuawa na polisi na viongozi wao wakakanusha kuhusika askari wao lakini tume ilipochunguza ikagundua polisi waliwateka na kwenda kuwaua Msitu wa Mabwepande, Dar.

Mbaya zaidi ni kwamba jeshi la polisi lilipofungua kesi liliwasilisha ushahidi ulioshindwa kumtia hatiani askari yeyote licha ya kuonekana kuwepo eneo la mauaji. Nimeandika haya ili kuwafahamisha viongozi wazuri wa polisi kwamba mambo haya ndiyo yanayosababisha kulalamikiwa na wananchi likiwemo tatizo la kubambikia watu kesi lengo likiwa kula rushwa.

Viongozi safi wa polisi chini ya IGP Ernest Mangu mulikeni hili na hawa wanaofanya haya ndiyo wanaolichafua jeshi zima la polisi.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply