The House of Favourite Newspapers

Dereva Aliyesababisha Ajali ya Basi la City Boy, Ajisalimisha Polisi

0
Dereva wa Basi la City BoyMMOJA wa madereva waliosababisha ajali ya mabasi ya Kampuni ya City Boy iliyotokea Julai 4, mwaka huu na kutoroka, Boniface Mwakalukwa (37), amejisalimisha mikononi mwa polisi na kufikishwa mahakamani.
Mwakalukwa ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam jana aliunganishwa kwenye mashitaka na dereva mwenzake Jeremiah Semfungwe (34) wote kwa pamoja wakikabiliwa na makosa 30 ya kuua bila kukusudia.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, Joyce Minde ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo Julai 4, mwaka huu saa 8.15 mchana wakati wakiendesha mabasi aina ya Scania yenye namba za usajili T 247 BCD na T 331 DCE kwa kuyagonganisha.
Ilidaiwa kuwa kitendo hicho ambacho kilitokea Kijiji cha Maweni wilayani Manyoni kilisababisha vifo vya abiria 30 na majeruhi 54. Wakili wa Serikali, Petrida Muta alidai kuwa siku ya tukio watuhumiwa wakiwa ni madereva wa Kampuni ya City Boys, bila kukusudia, walisababisha vifo vya abiria hao kinyume na Kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Toleo la Kwanza.
Ingawa Wakili wa washitakiwa, Francis Kitope aliiomba Mahakama iwape wateja wake dhamana kwa kuwa chini ya Kifungu 148 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kosa hilo linadhaminika, Wakili wa Serikali Muta alipinga dhamana hiyo.
Muta ambaye aliwasilisha Hati ya Kiapo mbele ya Mahakama hiyo, alidai kuwa kwa kufanya hivyo usalama wa washitakiwa utakuwa hatarini kwa kuwa ndugu wa marehemu na majeruhi bado wana hasira kutokana na ajali hiyo kuwa bado haijasahaulika.
Aidha, Muta aliendelea kudai kuwa baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo hali zao bado ni mbaya na hatma yao haijulikani, hivyo si vyema washitakiwa kupewa dhamana wakati huu. Kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika, washitakiwa wamerejeshwa rumande hadi Agosti 4, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
Leave A Reply