The House of Favourite Newspapers

IGP Sirro: Ukishika Bunduki, Aga Familia Yako – Video

0

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, amewataka wale wote wanaofanya uhalifu kwa kutumia silaha kuhakikisha kabla hawajatoka majumbani mwao wahakikishe wameziaga familia zao kwani jeshi hilo haliwezi kuwavumilia.

 

 

Kauli hiyo ameito hii leo Februari 26, 2021, mara baada ya Rais Dkt. John Magufuli, kuzindua Chuo cha Maafisa ya Polisi Kurasini Dar es Salaam, ambapo alitumia nafasi hiyo kutoa taarifa ya mwenendo wa uhalifu hapa nchini na kusema kuwa hali ya usalama ni shwari licha ya uwepo wa changamoto.

 

 

“Hali ya usalama nchini kwetu ni shwari sana ingawa bado kuna matukio machache yanajitokeza kama majuzi umeniuliza utekaji wa baadhi ya maeneo barabarani na nikuhakikishie Rais wale wahusika wote waliofanya yale matukio wamekamatwa.

 

 

“Kuna watu wanafanya mauaji, wanafungwa, wanakata rufaa, wakirudi mtaani hawabadiliki, nataka niwambie awamu hii si awamu ya kuendekeza ujambazi wala ugaidi, wasiotaka kuwabadilisha tutawabadilisha. Huwa nasema kabla hujachukua bunduki yako nyumbani kwako kwenda kusumbua Watanzania uage familia yako kwa sababu habari ya bunduki ukamataji wake huwa ni mgumu, Watanzania walishasahau benki zao kunyang’anywa fedha”.

 

 

“Watanzania na wahalifu watuelewe awamu hii si ya kuendekeza ujambazi wa kutumia silaha na ugaidi, ukiingia kwenye hii biashara usiilaumu serikali, kwahiyo Mh. Rais nikuhakikishie wale ambao hawataki kubadilika tutawalazimisha,” amesema IGP Sirro.

 

 

Aidha, IGP Sirro ameongeza kuwa, “Kwa mwaka 2019 na 2020 tumeweza kupunguza uhalifu kwa asilimia 13.5, makosa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha yameendelea kupungua changamoto tunayoipata kuna watu wanafanya tukio, wanafungwa na kisha wanakata rufaa na akirudi mitaani habadiliki.

 

 

“Wanaoandikiwa makosa barabarani wanakwepa, wanaficha magari gereji na wengine kubadili plate number, kwa wiki mbili tumefanya oparesheni na kukusanya takribani Tsh bilioni 2, lakini nimekuwa nikiwaambia sisi sio TRA.”

Leave A Reply